Habari ambazo Fikra Pevu imeweza kuzipata usiku wa kuamkia leo ni kuwa kesi ya kubaka ambayo ilikuwa ikimkabili Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) Bw. Dominique Strauss-Kahn inaelekea kuparaganyika baada ya taarifa kuibuka kuwa binti aliyetuhumiwa kubakwa aliwadanganya wapelelezi.
Mtumishi wa usafi wa hoteli ambayo Bw. Strauss-Kahn alikuwa amefikia alidai wiki chache zilizopita kuwa alibakwa na Bw. Kahn, kitu kilichosababisha vikosi vya polisi kuanzisha msako na hatimaye kumuibua Bw. Kahn toka kwenye ndege ya Air France ambayo alikuwa tayari amepanda kuelekea kwao Ufaransa.
Taarifa hizo za jana kutoka kwa wadokezaji waliozungumza na gazeti la New York Times zinadokeza kuwa katika uchunguzi wao wapelelezi wa Jeshi la Polisi la Jiji la New York (NYPD) waligundua kuwa mlalamikaji hakuwa mkweli katika maelezo yake mbalimbali na hivyo kuna dalili kuwa kama siyo kesi nzima kuvunjika basi madai mengi dhidi ya Kahn yanaweza kutupwa na masharti ya dhamana kulegezwa.
Kwa mujibu wa taarifa hizo taarifa mbalimbali ambazo mlalamikaji alizitoa baada ya sakata la Kahn zinakinzana na taarifa alizozitoa kwenye maombi yake ya ukimbizi wa kisiasa na alisikika akizungumzia atakavyonufaika na kesi hiyo ya Kahn katika maombi yake hayo. Kukinzana kwa taarifa hizo kuliwagutusha wapelelezi na kuanza kuangalia simu lake kwa mashaka.
Endapo kesi dhidi ya Strauss-Kahn itavurugika kuna uwezekano mkubwa wa kesi nzima kufutupiliwa mbali kwani maneno ya mlalamikaji yatakuwa yametiwa shaka kubwa. Hata hivyo, wakili wa mlalamikaji amedai kuwa kuna kampeni ya kumchafua mteja wake ili kusaidia kesi ya Kahn. Bw. Kahn atafafikishwa mahakamani tena leo ambapo inatarajiwa kutokana na taarifa hizi mpya masharti magumu ya dhamana aliyopewa yanaweza kulegezwa.
Mwandishi Wetu