Pendekezo la “Ukanda mmoja, Njia moja” lafikisha hariri na kauri mpya barani Afrika

Fadhili Mpunji

Kwa wenye uelewa wa ndani juu ya historia ya dunia, bila shaka watakuwa wanafahamu kwamba katika kipindi fulani kwenye historia ya dunia (207 BC–220 AD), China ilikuwa ni moja ya nchi muhimu duniani, na ilikuwa na mchango wa kipekee kwa dunia uliohimiza maingiliano ya kibiashara kati yake na nchi nyingine. Wakati huo kulikuwa na bidhaa mbili muhimu kutoka China kwenda katika mabara mengine, nazo ni vyombo vya kauri na vitambaa vya hariri.

Umuhimu huo ndio ulifanya jina la kichina la China liundwe kwa herufi mbili za kichina, 中国 (Zhong Guo). Herufi ya kwanza yaani 中 ina maana katikati au kiini, na herufi ya pili 国(Guo) ina maana “Nchi ya Kiini”.

Kulikuwa na njia mbili kuu za kusafirisha bidhaa hizo. Njia ya kwanza ilikuwa ni kutoka kusini kupitia bahari ya Hindi na kufika kwenye nchi ikiwa ni pamoja na Indonesia, India na hata pwani ya Afrika Mashariki, hiyo iliitwa ‘Njia ya hariri ya baharini’. Njia ya pili ilikuwa ni njia ya barabara kupita sehemu ya kaskazini magharibi mwa China, na kuelekea uajemi, mashariki ya kati hadi Ulaya. Njia hii ya Ulaya ibebe jina la ‘Njia ya hariri’, kwa kuwa hariri ilikuwa ni moja ya bidhaa muhimu iliyosafirishwa kwenye njia hiyo.

Kutokana na kuwa wakati ule, bahari na njia za ardhi zilikuwa ndio njia pekee za mawasiliano. Tunaweza kusema kuwa China ilitumia njia hizo kujiunga vizuri na dunia. Na kutokana na kuwa kauri na vitambaa vya hariri vilifika katika sehemu mbalimbali duniani, tunaweza kusema China haikuwa na choyo kwa nchi nyingine kutokana na uvumbuzi wake.

Hali ya dunia ya sasa imebadilika sana ikilinganishwa na miaka ya 207 BC–220 AD. Dunia imepiga hatua kubwa kimaendeleo na vyombo vya kauri na vitambaa vya hariri, havina nafasi tena kwenye biashara. Lakini, njia ya hariri baharini bado ipo na njia ya hariri ya kaskazini magharibi pia ipo.

Mabadiliko makubwa pia yametokea kwenye uchumi wa China na kufanya nafasi yake duniani irudi kama ilivyokuwa wakati wa ‘Nchi ya kiini’.

China sasa imekuwa ni nchi ya pili kwa nguvu ya uchumi duniani, na umuhimu wa bidhaa zake duniani umekuwa ni zaidi ya ule Kauri na Hariri. Kwa sasa mbali na bidhaa kama nguo, vifaa vya elektroniki, na vifaa vya ujenzi, nchi hii sasa imekuwa ni chanzo cha teknolojia, mikopo, misaada na hata masoko kwa nchi nyingi duniani. Hizi ni hariri na kauri mpya kutoka China, zinazoifanya iwe mhimili muhimu wa uchumi wa dunia.

Uwingi wa bidhaa zilizopo China kwa sasa, umeleta mahitaji ya kupanua njia za ushirikiano. Ndio maana pendekezo la ‘Ukanda Mmoja na Njia Moja’ lilitolewa na serikali ya China mwaka 2013, limekuwa na maana pana zaidi na kuleta manufaa zaidi kwa nchi zinazoshiriki, ikilinganishwa na njia ya hariri na njia ya hariri baharini ya mwaka 207BC.

Serikali ya China imekuwa ikisema mara kwa mara, haitakuwa na uchoyo na maendeleo yake. Hatua nyingi zimechukuliwa na serikali hii kufanya maendeleo yake yanufaishe nchi nyingine.

Mbali na njia ya hariri na njia ya hariri ya baharini kuboreshwa na kuwa na ufanisi zaidi kwenye kusafirisha bidhaa nje na kuagiza bidhaa, kumekuwa na njia mpya kama vile mawasiliano ya habari (ICT) na mawasiliano kwa njia ya ndege ambayo yamehimiza biashara.

Ya hivi karibuni, ni kuanzisha Benki ya Uwekezaji kwenye maendeleo ya ujenzi wa miundo mbinu AIIB, na kumekuwa na mabaraza mbalimbali ya kuhimiza ushirikiano na maendeleo na nchi na sehemu nyingine, kama vile FOCAC, na hata kumekuwa na mifuko ya kuendeleza maendeleo na pande mbalimbali, kama vile CAD FUND (China-Africa Development Fund).

Mwishoni mwa juma hili, mkutano wa ‘Ukanda Mmoja na Njia Moja’ unafanyika hapa Beijing. Viongozi wa nchi mbalimbali na wawakilishi watahudhuria kujadili maendeleo ya utekelezaji wa mipango ya pendekezo la ‘Ukanda Mmoja na Njia Moja’.

Kumekuwa na manufaa mengi ya pendekezo hilo kwa nchi mbalimbali. Mifano ya wazi ni kama mradi wa ujenzi wa reli ya SGR nchini Kenya, mipango ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo na mji wa viwanda mkoani Tanga, Tanzania.

Baada ya mkutano huo inatarajiwa mengi zaidi kuhusiana na manufaa ya pendekezo hilo yatafahamika na tutaleta mwendelezo hapa FikraPevu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *