Kesi namba 457 inayoikabili JamiiForums, kuhusu kampuni ya CUSNA Investment ambayo ilidaiwa kufoji nyaraka bandarini, kukwepa kodi na kuwatesa wafanyakazi wazalendo na kupendelea wageni toka nje ya nchi, imeanza kusikilizwa leo kwa shahidi wa Jamhuri kutoa ushahidi wake.
Katika kesi hiyo, Polisi walitaka JamiiForums iwapatie taarifa za mwanzisha mada na mchangiaji mmoja ili waweze kuwakamata na kuwahoji kutokana na ukiukwaji wa taratibu, JamiiForums inadaiwa kuwa ilikataa kutoa taarifa binafsi za mwanachama wake kwa kuamini kuwa chanzo hiki cha taarifa kilikuwa na nia njema hivyo kutaka kwanza iwepo Hati ya Mahakama inayoridhia kukamatwa kwa mhusika na kuelezwa kosa lake.
Kesi ipo chini ya Hakimu Godfrey Mwambapa na inasikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam. Upande wa utetezi unawakilishwa na Mawakili Jebra Kambole na Jeremia Mtobesya na upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili Mutalemwa Kisenyi ambapo ulimleta shahidi mwingine ili kutoa ushahidi wa shauri hilo na mahajiano yalikuwa hivi:
Wakili wa Serikali: unaitwa nani?
Shahidi: Naitwa ASP Fadhili Bakari. Ni Afisa Polisi, Kanda maalum Dar es Salaam tangu Machi 2016.
Wakili wa Serikali: Majukumu yako ni yapi?
Shahidi: Ni Mkuu wa kitengo Cha uhalifu wa kifedha Kanda maalum ya Dar es Salaam, pia kitengo cha uhalifu wa makosa ya kimtandao kipo chini yangu.
Mnamo tarehe 10/05/2016 nikiwa ofisini alikuja mpelelezi wa Kesi, Assistant Monica na jalada la uchunguzi linalohusiana na tuhuma zilizoletwa ofisini na Mkurugenzi wa Wakala wa Forodha CUSNA Investment na Ocean Link kwamba kuna taarifa zimesambazwa kwenye mtandao wa JamiiForums kwamba kampuni tajwa inajihusisha na wizi, ukwepaji Kodi na kughushi vitendo ambavyo vimeisababishia Serikali hasara.
Tuhuma zilizoletwa na watu wawili ambao ni Amrish Puri na Kwayu. Taarifa zilizodaiwa kusambazwa mnamo 08 Desemba 2015. Inspekta Monica alikuja kwangu ili niweze kuwasiliana na Mkurugenzi wa JamiiForums ili tupate details za wateja zitakazosaidia kwenye Kesi/uchunguzi.
Niliandika barua kwenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa JamiiForums ikimtaka anipe Ushirikiano wa kunipa information (Namba za simu na taarifa za usajili za watu hao). Baada ya kuandika barua na kuisani nilimpatia mhusika kufikisha kwa anaehusika, Inspekta Peter Kayumbi aliniambia siku ya pili kuwa barua imepokelewa na kusainiwa na aliyeipokea.
Sikuweza kupata information nilizokuwa nazitaka ambazo zingenisaidia kwenye kesi (Shahidi anaonyeshwa kielelezo na anasema anaitambua kuwa ndio yenyewe na kuiomba mahakama iipokee kama kielelezo). Wakili wa utetezi (Jebra Kambole) anakubali ipokelewe na hakimu anaikubali.
Shahidi anaisoma barua ambayo alimuandikia Mkurugenzi Mkuu wa JamiiForums kuhusu taarifa inayoihusu kampuni za CUSNA Investment na Ocean Link ya kuomba taarifa za usajili na namba za simu walizotumia kipindi wanajisajili kwenye mtandao wa JamiiForums.
Anasema Barua ilipokelewa na Chrispine Muganyizi siku moja baadae, Shahidi anaulizwa kuhusu taarifa zilizopo kwenye barua na kusema kulikuwa na makosa ya kiuandishi kwenye mwaka. Shahidi anaendelea kusema hakupatiwa taarifa zozote kama alivyoomba.
Mkurugenzi wa Jamii Media, Maxence Melo (katikati) akizungumza na Wakili Jebra Kambole (aliyevaa koti) pamoja na watu wengine wakitoka nje ya Mahakama ya Kisutu mapema leo baada ya kesi 457 kusikilizwa.
Baada ya Wakili wa Serikali kumaliza kumuhoji shahidi, alifuata Wakili wa utetezi, Jebra Kambole na mahojiano yao yanaendelea;
Wakili: Umesema unamsaidia mkurugenzi wa upelelezi?
Shahidi: Sahihi
Wakili: Kwa uelewa wako wewe humfahamu mmiliki wa JamiiForums?
Shahidi: Simfahamu
Wakili: Unafanya kazi JamiiForums?
Shahidi: Hapana
Wakili: Una uhakika gani taarifa ulizoomba walikuwa nazo?
Shahidi: Nina uhakika walikuwa nazo.
Wakili : Una ushahidi?
Shahidi: Sina ushahidi mwingine
Wakili: Kwa kuwa hauna ushahidi, inawezekana huyo mtu taarifa ulizoomba alikuwa nazo au hakuwa nazo!?
Shahidi: Haiwezekani
Wakili: Kwa kuwa barua iliandikwa kwa Mkurugenzi Mtendaji, akiwemo mtu mwingine atakuwa ameonewa?
Shahidi: Siwezi kujua maana mimi sikuhusika kwenye ukamataji
Wakili: Kifungu Cha kumi hakikupi mamlaka ya kudai taarifa. Mtoa taarifa alitenda kosa gani?
Shahidi: Hili ni jalada la uchunguzi
Wakili: Hamkuona haja kuitaarifu TRA kuhusu mtu anayekwepa Kodi?
Shahidi: Haihusiani na hii kesi. Binafsi sikuwapa.
Wakili: Unajua mtu asikupokupa taarifa unaenda mahakamani kuomba amri?
Shahidi: Sijui.
Wakili Mtobesya: Naomba nipatiwe exhibit P1. Nawasilisha ombi hili kwa mujibu wa kosa la jinai na makosa ya mtandao.
Wakili Mtobesya anaendelea kumuuliza maswali shahidi;
Mtobesya: Unaelewa kama washtakiwa wanashtakiwa kwa kosa gani hapa mahakamani?
Shahidi: Sijui
Mtobesya: Nitakuwa sahihi kama nitasema Polisi hamjui mlitakiwa kufanya nini wakati mnatafuta taarifa?
Shahidi: Mimi nilitaka nipate details
Mtobesya: Kwa hiyo taarifa ulizokuwa unazitaka zilikuwa kwenye mtandao?
Shahidi: Ndiyo
Mtobesya: Naomba niishie hapo
Wakili wa Jamhuri: Uliwahi kupata majibu kutoka uongozi wa JamiiForums?
Shahidi: Sikuwahi kupata
Baada ya shahidi kuwasilisha ushahidi wake mbele ya Jaji Mwambapa kesi imeahirishwa mpaka kesho ambapo upande wa Jamhuri unakusudia kuwaleta mashahidi wengine.
Mwenendo wa Kesi
ASP Fadhili Bakari anakuwa shahidi wa pili baada ya shahidi wa kwanza, Inspekta Msaidizi Monica Pambe toka Jeshi la Polisi Kitengo cha Makosa ya Mtandao kutoa ushahidi wake mnamo Agosti 24, 2017 ambapo alidai Polisi hawana utaalamu wa kuingia mawasiliano ya kimtandao. Katika maelezo yake anasema aliagizwa na shahidi wa pili kuandika barua kwa uongozi wa JamiiForums ili wapate taarifa za wateja wa mtandao ziwasaidie katika uchunguzi wa kashafa ya kuchafuliwa kwa kampuni ya Cusna Investment na Oceanic Link.
ikumbukwe kuwa mwishini mwaka 2016, Maxence Melo alikamatwa na kushikiliwa na Jeshi la Polisi katika kituo kuu cha polisi, Dar es Salaam, kwa madai ya kugomea agizo la muda mrefu la jeshi hilo kupewa taarifa za watumiaji JamiiForums bila mafanikio. siku chache zilizofuata alifikishwa mahakamani kuachiwa kwa dhamana.
Tangu wakati huo kesi inaendelea na inaelezwa kuwa kesi hiyo inatarajiwa kutolewa uamuzi mwishoni mwa mwaka huu.