Kishapu: Haya ndiyo yanayowapata Wanafunzi na Walimu wa Shule ya Msingi Maghalata

Belinda Habibu

Mto Sanga unaokatisha katika kijiji cha Maghalata kwa karibu km 13, huleta usumbufu kwa wanafunzi wanaotakiwa kuvuka wakapate elimu kwa upande wa pili ambako kuna shule.

Kaimu mwalimu mkuu wa shule ya msingi Maghalata kwa siku hiyo tu kwa kuwa kaimu ameenda katika kikao tarafani, mwalimu Cyprian Mabele amesema utoro shuleni hapo unasababishwa na sababu mbalimbali ikiwemo kukosa daraja katika mto Sanga na kuathiri mahudhurio ya wanafunzi shuleni hapo.

MTO-SANGA-MAGALATA

“Wanafunzi wa shule hii robo yake  wanatoka ng’ambo ya mto katika vijiji vya Mwanzugi,Mapumbula,na Mawilo na robo tatu nyingine wanatoka maeneo haya karibu, kipindi cha mvua ikiwa mfululizo basi watoro wanaweza kuwa wengi”alisema mwalimu Mabele.

Ameongeza ikitokea mvua inanyesha na watoto tayari wako upande huu,kwa wale wanaoishi ng’ambo basi italazimu watafute ndugu zao walioko karibu na shule na wasiokuwa nao tunawahifadhi ingawaje ni usumbufu.

Alisema mwalimu mkuu wa shule hiyo aliandika majina ya watoro kwa afisa mtendaji  wa kijiji na kuomba wachukuliwe hatua za kupigwa faini ya sh.1000.

Mwenyekiti wa kijiji  hicho Burugu Mipawa amekiri kulikuwepo kwa tatizo hilo na kusema sasa limedhibiti na jukumu la kukusanya fedha hizo aliachiwa mwalimu mkuu ili zisaidie katika matumizi mbalimbali ya shule.

Kwa mujibu wa barua ya mwalimu mkuu kwa afisa mtendaji iliyokuwepo katika mafaili yaliyopatikana katika ofisi ya kijiji hicho, ilionyesha kila mzazi wa mwanafunzi mtoro alitakiwa kulipa sh.1500 kwa siku ambayo hakuwako shuleni kwa utoro.

Aidha, akizungumzia suala la ufaulu kwa mtihani wa darasa la saba kaimu mwalimu mkuu tena alisema toka aingie yeye mwaka 2010,(miaka mitatu sasa) kuna ongezeko la mwanafunzi mmoja kwa kila mwaka anayefaulu.

Aliongeza kwa kusema mwaka 2010 kati ya waliomaliza darasa la saba waliofaulu walikuwa sita,2011 walikuwa saba na 2012 walikuwa wanane kati ya wanafunzi 32.

“Tumeweka mkakati wa kufundisha muda wa ziada kwa wanafunzi wa darasa la saba bure kwa kuwa wanapata  chakula shuleni.”aliongeza mwalimu huyo.

Nilishuhudia wanafunzi wakiwa wanakunywa uji asubuhi na jikoni chakula cha mchana aina ya makande kikipikwa.

wanafunzi-magalata

Baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Msingi Maghalata wakipata uji

Msaada wa chakula wanaopatiwa shuleni hapo ni kutoka kwa ufadhili wa WWF kama ilivyo kwa sehemu zingine za hapa nchini,wanatoa  chakula shuleni ili wanafunzi wawe wasikivu darasani.

Sambamba na hilo pia kaimu mwalimu mkuu huyo alisema wanaupungufu wa walimu watatu, kwa sasa wapo 13 ila kati yao watatu hawapo mmoja yupo likizo ya uzazi,mwingine ameenda masomoni na mmoja mgonjwa.

“Tungeongezewa walimu wengine watatu ingetosha kwa kuwa idadi ya wanafunzi ni 386 kwa sasa wakike  214 na  wakiume 172.”alisema mwalimu huyo.

Ameongeza walimu tunachagamoto ya ukosefu wa nyumba za kuishi kwa sasa iko moja tu na tungeongezewa nyingine tano zingetosha, kwetu inatupa usumbufu wengi wetu tumetoka mbali na gharama za maisha ziko nyingi.

Naye kaimu afisa mtendaji wa kijiji cha Maghalata bwana Jienze Mwandu alisema sense ya mwaka 2012 katika kijiji hicho ilionyesha kina wakazi 2800 na changamoto ya kijiji katika elimu ni idadi ya wanaojua kusoma na kuandika kutofautiana  kwa makabila makuu ya kijiji hicho.

“Wasukuma wengi wanajua kusoma na kuandika ila watu wa kabila la wataturu hawajui kwa kuwa ni jamii ya wafugaji wanahamahama,suala la shule hawalitilii mkazo”aliongeza Mwandu.

Kwa mujibu wa jiwe la msingi lililobandikwa karibu na ofisi ya walimu,inaonyesha shule ya msingi Maghalata ilifunguliwa mwaka 1999 katika mbio za mwenge zilizopita kijijini hapo kwa mara ya mwisho mwaka huo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *