Athari za Ukataji wa Miti katika Msitu wa Shengena…

Belinda Habibu

“Biashara ya kupasua mbao ambayo inahatarisha kumaliza msitu wa Shengena haiwezi kwisha kwa kuwa kila siku watu wanakata miti hiyo na kuuziana wenyewe kwa wenyewe.”

Mmoja kati ya wazee wa eneo la Chome, bwana Richard Lukwaro aliyasema hayo na kuongeza,huwezi  kuingia tu msituni bila kuwa na ruhusa kutoka kwa bwana misitu, na atakwambia ulipie shilingi 5000 kwa msumeno mmoja kwa watu wawili,je ikiwa misumeno hamsini atapata shilingi ngapi?

Kwa upande mwingine bwana Lukwaro alisema  uwelewa wa watu ni mdogo katika kutunza mazingira,utakuta mtu analima hadi katika chanzo cha maji, anakata misitu, na hapandi miti kulingana na uharibifu alioufanya.

Ameongeza kuwa  katika maeneo haya ya Chome,kati ya mwaka 1968-70 palikuwa teketeke na ziwa lilikuwepo lakini sasa ni ukame ukipita huku mtu ana msumeno wake anakata miti, hii ndio hali halisi ya hapa.

Mkazi mwingine Clement Mshighati alisema toka enzi za babu zetu tunategemea msitu huu kwa shughuli mbalimbali, ikiwemo kupata miti ya kujengea,dawa,maji na hata kulishia mifugo yetu.

Afisa mtendaji wa kata ya Chome bi Niwael Naftal alisema kwa sasa mtu hawezi kukata mti kwa shughuli yoyote mpaka apate kibali kutoka serikali ya kijiji na wilaya baada ya kujadiliwa kwa miezi mitatu,ili ofisi ijiridhishe kuwa kweli miti ni yake na unatumia kwa mfano katika shughuli za ujenzi.

Ameongeza kuna uhamasishaji wa wananchi katika kupanda miti na kuna vitalu vya miti na mwanakijiji huuziwa kila mche shilingi mia mbili ama shilingi mia tatu.

Kwa mujibu wa sheria ya misitu Na.14 ya mwaka 2002 hairuhusiwi kuvuna miti katika misitu ya hifadhi ya vyanzo vya maji, ardhi  na bioanuai.

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Same,bwana James Nshare amesema Changamoto iliyokuwepo kwa miongo miwili katika halmashauri hii, ni ukataji wa miti kwaajili ya mbao katika msitu wa hifadhi ya asili wa Shengena.

Alisema  wilaya ya Same ina hali ya hewa ya nusu jangwa ,hivyo wananchi hutegemea maliasili zilizopo kukidhi mahitaji yao ya  kila siku kiuchumi.

“Wananchi waling’oa kahawa ambayo ilikuwa inawaongezea kipato hapo awali kutokana haikuwa na soko na sasa wamehamia katika matumizi ya maliasili zilizopo za msitu,uchimbaji madini ya dhahabu” anakazia bwana Nshare.

Kaimu afisa maliasili wa halmashauri ya wilaya ya Same bwana Kitwana Mungi  amesema maeneo ya vijijini,baadhi ya wananchi huwa hawafuati sheria ila wanapaswa kupata kibali kutoka serikali yao ya kijiji kwa shughuli yoyote katika msitu huu wa Shengena.

Mkutano mkubwa wa Umoja wa mataifa uliohusu mazingira na makazi ya watu uliofanyika huko Sweden mwaka 1972,mjini Stockholm,ulitoa tamko rasmi  lililosisitiza pamoja na mambo mengine umuhimu wa kuhifadhi mazingira ya mwanadamu ambayo ni chanzo kikubwa cha uhai wake.

Sheria ya misitu 2002 tena , inasema kila atakayetaka kuvuna mazao ya misitu atatakiwa kupata barua yenye idhini ya serikali ya kijiji, baada ya kujadiliwa na kukubaliwa na wajumbe wa serikali hiyo.

 

Katika taarifa fupi ya utendaji kazi ya ofisi ya hifadhi ya mazingira ya asili chome (Shengena) iliyopatikana nakala yake,wakati wa  ziara ya mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro ya  tarehe 24/06/2012 inasema hifadhi hii ndio chanzo pekee cha mito yote katika wilaya ya Same.

 

Asilimia 90% ya watu wa Same hutegemea mito hiyo kwa umwagiliaji na matumizi mbalimbali ya nyumbani.

 

Taarifa hiyo imeendelea kusema hifadhi hii imezungukwa na vijiji 27 (vyenye wakazi 60,916 sawa na theluthi ya wakazi wa Wilaya ya Same (Sensa 2002).

 

Kwa mujibu wa mtandao wa gazeti la Mwananchi,unasema hifadhi ya mazingira asilia ya Chome ambayo inafahamika zaidi kama msitu wa Shengena uliopo Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, ina aina 17 ya miti ambayo kama itatunzwa vizuri ina uwezo wa kutibu ugonjwa wa Saratani

Mkutano mwingine wa umoja wa mataifa miaka ishirini baada ule wa Sweden,ulitoa tamko lake, (The Rio Declaration) na  ulisisitiza juu ya maendeleo endelevu ikiwa ni pamoja na kujali utunzaji wa mazingira kwa ajili ya vizazi vya sasa na vya baadae.

Kwa mujibu wa mtandao wa Making it happen,ulisema mkutano huo pia, ulijadili uharibifu uliokithiri wa mazingira na dunia ilijikuta ikikabiliwa na changamoto za kina kama vile:-Mabadiliko ya tabia ya nchi (Climate change), upotevu wa bio-anuai (Bio-Diversity loss), hatari za majagwa ( desertification) na uharibifu wa vyanzo vya maji safi.

Sheria ya  uhifadhi wa mazingira ya mwaka 2004,inataka ushiriki wa wananchi wa eneo tarajiwa la mradi wowote kuhusishwa moja kwa moja katika hatua zote za kutathimini athari za kimazingira zitakazoletwa na uanzishwaji wa mradi unao tarajiwa kuanzishwa.

Tarehe 29 June 2012,akichangia bajeti ya  Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2012/2013 – Ofisi ya Waziri Mkuu na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Anne Kilango Malecela alisema Mheshimiwa Spika, Msitu wa Shengena umeharibiwa kabisa na majangili wanaovuna dhahabu kwa njia haramu. Msitu wa Shengena umesheheni miti mikubwa sana na ni Msitu wa asili.

Madhumuni ya Sera ya Taifa ya Mazingira ya 1997 ni yafuatayo;  kuzuia na kudhibiti uharibifu wa ardhi, maji, mimea na hewa ambayo ndiyo husaidia mfumo wa uhai wetu.

Pia kuhifadhi na kuendeleza urithi wetu na ule unaotengenezwa na binadamu, ikiwa ni pamoja na maisha ya viumbe wa aina mbalimbali na vya pekee nchini Tanzania

Kwa mujibu wa mkuu wa operesheni ya msitu wa Shengena Bwana Frank Mahenge,amesema  msitu huu unajumla ya hekta 14,283,kati ya hizo hekta 16 zimeharibiwa na shughuli za uchimbaji haramu wa madini ya dhahabu na ukataji wa  miti ya mbao.

 

————————————————————————————————————–

 

 

4 Comments
  • Pongezi za zati kwako unaeumia na kuguswa na mali asili zinavyotumiwa vibaya. Kweli inauma kuona msitu wa shengena unaisha. Ukame uliopo leo chome na vitongoji vinayoizunguka ni sababu ya kupotea kwa shengena.Hata hivyo serekali ni KIPOFU kwani leo inakamata wananchi wadogo ikiwa udongo ulisafirishwa ikiwa imefunga macho. Ni jukumu letu kurudisha uoto wa asili wa shengena.

        Dada usirudi nyuma.

  • Napennda kurejea kauli ya mbunge mmoja wakati  akichangia bungeni alisema: huwezi kutatua matizo kwa kiwango kimoja cha kufikiri (the same level thinking)

    Zile serikali za vijiji wamepewa dhamana watu waliolingana uwezo wa kufikiri, kwa nama hiyo tutasingizia tu serikali -serikali lakini ukweli serikali pale ni wale wale wanaoathirika na uchafuzi huo wa mazingira. Yaani wanajichoma kisu wenyewe bila kujijua.

    Sasa chakufanya, hasa wewe ulilyetafiti hili na kulifikisha hapo, pamoja na wadau wengine, natutafute wadau ambao watatusaidia kuhamasisha na kuelimisha zile serikali 27 zinazozunguka msitu ule. Mkuu wa mkoa ndugu yetu na mkuu wa wilaya mliopewa dhamana ya kuwaongoza watu hawa naomba msiishie hapo tu, kazi zenu ni kuhimiza pamoja na mambo mengine, uhifadhi wa mazingira. Wale wazee naamini wakielimisha na hasa kuhamasishwa wataamka na kusaidia kunusuru kizazi kijacho. Mabadililko ya hali ya nchi ni majanga baadae muda mfupi ujao.

  • Licha ya kukata miti na kupasua mbao katika msitu wa shengena, lipo kubwa sana la kusafirisha udongo unaoaminika una madini kwenda nchini kena unaofanywa na mfanyabiashara mmoja kwa kusaidiwa na mkuu wa wilaya ya Same, tafadhali hapa inahitajika nguvu ya ziada ikibidi waziri mkuu maana huenda kuna usaidizi kutoka juu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *