Siku ya Saratani duniani inaadhimishwa Februari 4 kila mwaka. Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa, kila mwaka wagonjwa wapya wapatao 50,000 hugundulika na saratani za aina mbalimbali Tanzania.
Kati ya hao, ni wagonjwa 13,000 tu sawa na asilimia 26 ndio wanaofanikiwa kufika Hospitali kupata matibabu. Aidha, wagonjwa walio wengi (takribani asilimia 70) hufika Hospitalini kwa ajili ya matibabu wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa (hatua ya 3 na ya 4), hali ambayo hupunguza uwezekano wa wagonjwa hao kupona.
Takwimu za kimataifa zinaonesha kwamba kila mwaka kuna wagonjwa wapya milioni 12 wa saratani ambapo wanaofariki kwa ugonjwa huo ni milioni 8. Tanzania ni miongoni mwa nchi barani Afrika ambazo zina wagonjwa wengi wa saratani.
Takwimu za mwaka 2016/17 kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road zinaonyesha kwamba Saratani zinaoongoza nchini ni: Saratani ya Kizazi (32.8%), Matiti (12.9%), Ngozi (Kaposis Sarcoma) (11.7%), Kichwa na Shingo (7.6%), Matezi(5.5%), Damu (4.3%), Kibofu cha Mkojo (3.2%), Ngozi (2.8%), Macho (2.4%) na Tezi Dume (2.3%).
Takwimu hizo zinaendelea kuonyesha kuwa wagonjwa wa saratani walioripoti katika Taasisi ya saratani ya Ocean Road (ORCI) waliongezeka kutoka 3,776 mwaka 2013 hadi 4,195 mwaka 2014. idadi hiyo inaongezeka kila mwaka ambapo mwaka 2015 wagonjwa 5,529 waliripoti katika hospitali hiyo na kufikia 6,340 mwaka uliofuata wa 2016.
Mkurugenzi wa Idara ya Kinga Taasisisi ya Kansa ya Ocean Road, Dk. Chrispin Kahesa wakati akihojiwa na kituo cha BBC alieleza sababu za saratani kuwa tishio kwa mataifa yanayoendelea, “Sababu ya kwanza inaweza kuwa mabadiliko ya tabia za maisha kwa wananchi wa nchi zinazoendelea ikiwemo kwamba watu wengi hawafanyi mazoezi na wanakula vyakula vinavyoongeza uzito na pia kuongeza maambukizi ya Saratani ikiwemo matumizi ya pombe”.
“Saratani ya shingo ya kizazi imeshamiri sana kwa kina mama na kuongezeka kwake ni kutokana na maradhi yanayopatikana kwa njia ya zinaa kutoka kwa kirusi cha Papiloma na maradhi haya yameshamiri sana kwenye nchi za ukanda wa Afrika ambapo maambukizi ya UKIMWI ni makubwa sana”, amesema Dk. Kahesa na kuongeza kuwa,
“Kwa upande wa tezi dume kwa wanaume ni saratani ambayo inawashika watu wenye umri mkubwa yaani miaka zaidi ya 50 na kuendelea”.
Saratani inachukua nafasi ya tano kwa nchi zote za Afrika ikiwemo Tanzania katika maradhi yanayosababisha vifo vingi vya watu. Kwa Tanzania saratani ya mlango wa kikazi ndio inashika nafasi ya pili kwa kusababisha vifo vingi.
“Karibu asilimia 38 ya wagonjwa wanapokelewa katika kituo hiki wanaugua saratani ya mlango wa kizazi hivyo ni saratani ambayo ipo kwa kiwango cha juu sana nchini Tanzania”, amesema Dk. Kahesa.
Katika kuadhimisha Siku ya Saratani Duniani Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema, “Ninatoa wito na kuhimiza kila mmoja wetu kupima ugonjwa wa Saratani. Saratani inatibika endapo itagunduliwa mapema”.
Mwishoni mwa mwaka 2017, Waziri Ummy alipokea mashine 100 za tiba mgando (cryotherapy), mashine 9 za upasuaji mdogo (LEEP) kwa matibabu ya awali ya saratani kwa wanawake na mitungi 173 ya gesi ya ‘Carbon dioxide’ itakayowezesha mashine hizo kuweza kufanya kazi.