Kwa mujibu wa utafiti mpya uliofanywa nchini Marekani, watu wanaopoteza utajiri au mali zao ghafla wana uwezekano mkubwa kufa mapema kuliko wale ambao wanafirisika taratibu.
Utafiti huo ulifanywa na watafiti wa Chama Cha Tiba cha Marekani ambapo walibaini kuwa kama mtu atapoteza asilimia 75 au zaidi ya utajiri wake, ana uwezekano kwa asilimia 50 kufa mapema kuliko mtu wa kawaida.
Ripoti ya utafiti huo imechapishwa kwenye Jalida la JAMA la nchini Marekani ambapo watafiti walichunguza jinsi uwezo wa kifedha ulivyo na matokeo kwa afya ya binadamu katika siku za kuishi kwake duniani.
Mtafiti, Lindsay Pool ambaye pia ni Mhadhiri wa Shule Kuu ya Afya ya Feinberg ya Chuo Kikuu cha Northwestern akiwa na wenzake waliwachunguza watu 8,700 walio na umri wa miaka kati ya 51 na 61 kwa miaka 20. Watafiti hao walichunguza kwa kiasi gani ‘mshtuko hasi wa utajiri’ unaotokana na kupoteza nyumba, biashara au pensheni unavyoathiri afya ya mtu na kumsababishia mauti.
Kwa miaka 20 ya kufuatilia maisha ya watu waliopoteza utajiri au mali zao ghafla waligundua kuwa kati yao ambao ni 25% walipata mshtuko na walikuwa katika hatari kubwa ya kufa. Asilimia hiyo inahusisha wanaume na wanawake.
“Hili ni jambo ambalo watu wengi wanapitia,” amesema Pool. “Ni tukio linatokea mara kwa mara.”
Lakini hatari hiyo sio tu kwa matajiri lakini hata watu masikini wenye kipato kidogo wanaweza kupata tatizo la kufa mapema. Walipotathmini kundi la watu wazima wenye kipato kidogo, hatari ya vifo vyao kwa miaka 20 ilikuwa 67%.
Kwa muktadha huo masikini wana uwezekano wa kufa mapema zaidi kuliko matajiri kwasababu matajiri 5 kati ya 10 wanakufa kwa kupoteza utajiri ghafla. Lakini masikini 7 kati ya 10 wanapata vifo vingi kuliko watu ambao wanapoteza mali zao ghafla.
Umasikini kwa muda mrefu umekuwa ukidhaniwa kuwa ndio chanzo kikubwa maradhi na vifo, lakini jambo la kushangaza ni kuwa watafiti hao wamesema kupoteza utajiri kuna matokeo yanayofanana na kufa mapema kwa mtu ambaye hana utajiri.
Hata hivyo, utafiti haukuangalia kwa kiasi gani kupoteza utajiri kunahatarisha moja kwa moja ya afya ya mtu. “Dhahania iliyojengwa hapo ni kuwa mshtuko wa utajiri ni tukio la msongo wa mawazo au mkazo (stress), na mkazo wa muda mrefu unaweza kuathiri kila kiungo cha mwili,”, amesema Pool.
Matokeo ya utafiti huo yanaweza kuwa na mahusiano na watanzania ambao wanakabiliwa migogoro ya fedha. Kama matatizo yao hayatatuliwa kuna uwezekano idadi ya vifo ikaongezeka. “Watu hawataki kupoteza kazi zao,” amesema Pool. “Ni kazi ya watunga sera kutafuta namna ya kutatua changamoto hizo.”