Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema kukithiri kwa mauaji, utekaji, uteswaji, ukatili, kuminywa kwa uhuru wa kutoa maoni, kukusanyika na kujumuika ni matukio makubwa yaliyovunja zaidi haki za binadamu nchini kwa mwaka 2017.
Akiwasilisha ripoti ya Haki za binadamu Tanzania (2017), Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dkt. Hellen Kijo Bisimba amesema ukiukwaji wa haki za binadamu kwa mwaka 2017 uliongezeka zaidi ukilinganisha na mwaka 2016 ambapo hatua muhimu zisipochukuliwa inaweza kuvuruga amani na demokrasia iliyojengwa kwa muda mrefu na waasisi wa taifa.
“Haki za kiraia na kisiasa zilivunjwa zaidi, hasa haki ya kuishi, haki dhidi ya ukatili, haki ya kuwa huru na usalama wa mtu, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kukusanyika na uhuru wa kujumuika. Kuminywa kwa haki hizi pia kuliathiri haki ya kushiriki katika utawala/serikali hususan haki ndogo ya kushiriki katika muasuala ya siasa.” Amesema Dkt. Hellen
Ripoti hiyo imebainisha kuwa haki iliyovunjwa zaidi ni haki ya kuishi kutokana na kuendelea kwa mauaji ya kujichukulia sheria mkononi, mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola na mauaji yatokanayo na imani za kishirikina.
“Mpaka kufikia Disemba 2017, idadi ya vifo vilivyotokana na na wananchi kujichukulia sheria mkononi ilifikia 917 ambavyo ni vifo 5 zaidi ya vile vilivyoripotiwa mwaka 2016. Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kwa matukio ya kujichukulia sheria mkononi, ukifuatiwa na Mbeya, Mara, Geita, Tanga na Kigoma.” Imeeleza ripoti hiyo.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa mauaji yaliyotekelezwa na vyombo vya dola ikiwemo akatili dhidi ya askari polisi yalikuwa 9 ambayo ni 5 zaidi ya yale yaliyokusanywa 2016.
Dkt. Hellen amesema haki nyingine iliyovunjwa zaidi 2017 ni kushambuliwa na vitisho kwa wanahabari, kufungiwa kwa vyombo vya habari na kutumika vibaya kwa sheria kuhusu uhuru wa kujieleza ikiwemo Sheria ya Huduma za Habari ya 2016.
Anafafanua zaidi kuwa “ Uvamizi wa ofisi za Clouds Media uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na vitisho na ukamataji kinyume na sheria wa wanahabari 10 kwa amri ya mkuu mmoja wa wilaya mkoani Arusha. Jumla ya magazeti 4 yalifungiwa na kulipishwa faini kwasababu tofauti ikiwemo chini ya sheria kandamizi ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ya mwaka 2016.”
Amebainisha kuwa kutekwa na kupotea kusikojulikana kwa mwandishi wa habari kutoka kampuni ya Mwananchi Novemba 2017, Azory Gwanda kuliitia doa nchi katika kulinda wa haki za binadamu hasa uhuru wa vyombo vya habari.
Haki ya kuwa Huru na Usalama wa Mtu
LHRC inaeleza kuwa ilikusanya matukio takribani 38 ya uvunjifu wa haki ya usalama wa raia, ikiwemo watu kutekwa au kupotea katika mazingira ya kutatanisha; miili ya watu ambao inaonekana waliuwawa na kuwekwa kwenye mifuko ya sandarusi ikielea kwenye fukwe za bahari ya Hindi.
“ Shambulio la Rais (aliyemaliza muda wake)wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu Mkuu wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu; na mauaji ya raia, viongozi na askari wa polisi kule Kibiti na maeneo mengine ya Mkoa wa Pwani ambapo watu wasiopungua 40 wakiwemo askari wa polisi 12 wameuawawa tangu mwaka 2015.” Imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.
LHRC pia imegusia haki ya kutokuteswa ambapo ilibaini matukio yasiyopungua 22 na mengi (15) yalikuwa ni hukumu ya kifo- ambayo ni uteswaji kwa mujibu wa Mkataba dhidi ya Uteswaji . Mfano ni tukio la kutekwa na kuteswa kwa msanii Roma Mkatiliki na wenzake mapema mwaka huu.
Amezitaja haki zingine ambazo zilikiukwa ni pamoja na haki ya kukusanyika na kujumuika ambapo vyama vya siasa vimezuia kufanya shughuli zao ikiwemo mikutano ya hadhara, maandamano na hata vikao vya ndani kwa kile kinachodaiwa kuwa ni wakati wa maendeleo.
Hata hivyo, Dkt. Hellen amesema uvunjaji wa haki 5 zilizobainishwa kwenye ripoti ya LHRC ni kiashiria tosha kuwa usalama wa nchi uko shakani na hatua za makusudi zinahitajika kutetea na kulinda raia na mali zao ili amani izidi kushamiri kwenye jamii ya watanzania.
Viongozi wa LHRC na washiriki wa hafla ya uzinduzi wa ripoti ya Haki za Binadamu 2017, katika picha ya pamoja leo jijini Dar es Salaam.
Wadau watoa maoni yao
Akizungumza baada ya uzinduzi wa ripoti ya LHRC, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume amesema msingi wa amani katika nchi yoyote ile ni kuheshimu na kulinda haki za raia hasa haki ya kuishi na kutoa maoni.
Amesema ikiwa tunataka kuifikisha nchi kwenye uchumi wa kati ni lazima haki za binadamu zipewe kipaombele na watawala kwasababu maendeleo hayawezi kuja kama raia hawapati stahiki zao.
“Huwezi kujenga amani kama unavunja haki. Ni muhimu kulinda haki ya kuongea maana ndiyo msingi wa maendeleo yetu. Kuna uhusiano mkubwa kati ya haki ya kuongea na kukutana,” amesema Fatma na kuongeza kuwa,
“Yale mabadiliko ya fikra ya maendeleo yatapatikana vipi kama hukutani na wenzako kubadilishana mawazo? Msingi wa kuleta maendeleo yote ni haki ya kuongea na kujumuika, ukitoa hizo unabakiwa na mfumo ule ule huwezi kuleta maendeleo.”
Kwa upande wake, Mwanaharakati wa Haki za Binadamu, Richard Mabala amesema ripoti hiyo imetoa mwanga wa hali halisi ya nchi yetu na kuna haja ya kufanya tathmini ya maeneo yaliyo na changamoto katika kulinda haki za raia.
Ameshauri kuwa serikali inapaswa kuweka mazingira wezeshi kwa raia wote kuwa huru kufanya shughuli zao bila kuwepo vitisho vya kisiasa, maisha ili kuhakikisha amani iliyopo inadumu daima.
Naye, Mtetezi wa Haki za Wanawake kutoka taasisi ya Equality For Growth (EfG), Jane Magigita amesema ili matukio ya kuvunjwa kwa haki za binadamu yapungue ni lazima jamii ielimishwe juu ya madhara ya ukatili ambao umeota mizizi kwenye ngazi ya familia.
Amesema watu wakifunzwa kupendana na kuheshimu wengine, tutajenga jamii iliyostaarabika yenye maendeleo endelevu.
Akihitimisha kutoa maoni yake, Wakili na Mtetezi wa Haki za Binadamu kutoka LHRC, Imelda Lulu Urio ameshauri kuwa iundwe tume huru itakayochunguza matukio yote yaliyotokea mwaka 2017 ili kubaini kiini cha tatizo na kutoa suluhisho ambalo litakuwa msingi wa kukomesha matukio ya uvunjaji wa haki za raia kwa siku zijazo. “Kiundwe chombo huru kitakachoangalia matukio yote na kuja na suluhisho”.