Wasichana milioni 68 hatarini kukeketwa ifikapo 2030 duniani

Jamii Africa

Ulimwenguni kote inakadiriwa kuwa wanawake na wasichana milioni 200 wamekeketwa na kuwaachia madhara ya kisaikolojia, kiafya na kijamii.

Kwa mujibu wa shirika la Idadi ya watu la Umoja wa Mataifa (UNFPA), wasichana milioni 3.9 walifanyiwa ukeketaji mwaka 2015; inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2030 wasichana milioni 68 watakuwa kwenye hatari ya kukeketwa.

Takwimu za shirika hilo zinaeleza kuwa mila na desturi za baadhi ya jamii zinachochea ukeketaji na inaelezwa kuwa kuna uwezekano mkubwa  wa wasichana milioni 4 kukeketwa ndani ya mwaka 2018.

Afisa Programu wa UNFPA nchini Tanzania, Ali Haji Hamad amesema ukeketaji umepungua kutoka asilimia 18 mwaka 1996 hadi asilimia 10 mwaka jana.

Amebainisha kuwa mikoa iliyokuwa inaongoza kwa matukio ya ukeketaji, vitendo hivyo vimepungua kwa kiasi kikubwa mpaka kufikia asilimia 50 ukilinganisha na miaka ya nyuma.

UNFPA inashirikiana na nchi mbalimbali duniani kutokomeza ukatili huo na kuhakikisha wanawake na wasichana wanalindwa na kuheshimiwa. Kutokana na elimu na hamasa inayotolewa na UNFPA dhidi ya ukeketaji, mwaka jana jumuiya 2,959 za Afrika na wakazi milioni 6 walitangaza kuacha kukeketa wanawake.

Januari 6 mwaka huu ambayo ilikuwa siku ya kupinga ukeketaji duniani, jumuiya zaidi ya 1,000 nchini Sudan zimeacha kufanya ukeketaji ambapo zimebaini kuwa hauna faida za kiafya na ni kitendo tu kinachoendelea kukiuka haki za binadamu.

                                                              Msichana akikeketwa

 

Ukeketaji ni nini?

Ukeketaji ni uondoaji wa viungo vya uzazi vya nje vya msichana, yaani kisimi au sehemu ya ndani na nje ya mashavu ya uke. Huu ndiyo ukeketaji au kutahiriwa kwa mwanamke.

Ukeketaji unaweza kusababisha madhara makubwa sana kiafya, ikiwa ni pamoja na kumwaga damu nyingi mpaka kupelekea kufa, maambukizi ya magonjwa na kusababisha matatizo wakati wa kujifungua.

Zipo njia nne zinatotumika kuwakeketa wanawake ambazo zimebainishwa na Shirika la afya duniani(WHO) na kutofautisha kati ya aina moja na nyingine. Aina ya kwanza ni ile ambayo ngariba huondoa kinyama na sehemu inayozunguka au nyama ndogo sehemu za siri.

Aina ya pili ni ile ambayo mkeketwaji hukatwa eneo linalozunguka nyama na midomo ya ndani au sehemu yake. Shirika  la Afya duniani limetaja aina ya kwanza na ya pili kuwa hufanyika duniani kote kwa kiwango cha asilimia 80.

Aina ya tatu ni ile ambayo hugusa sehemu yote ya siri ya nje ambapo  hushonwa ili kuzuia kujamiiana na kuachwa tundu dogo kwa ajili ya mkojo na hedhi ambayo imeonekana kufanyika kwa asilimia 15.

Aina hii ya tatu hulazimu mwanamke aliyekeketwa kufunguliwa kabla ya kushiriki ngono au kujifungua hali ambayo humsababishia mwanamke maumivu.

Aina hii imetajwa kuwa ni kati ya aina mbaya zaidi ya ukeketaji ambayo imeenea katika pembe ya Afrika na maeneo yake jirani Somalia, Djibouti na Eritrea, na katika baadhi ya maeneo ya nchi ya kaskazini mwa Sudan na kusini mwa Misri.

                                                                                Baadhi ya vifaa vinavyotumika kukeketa

 

Aina ya nne ambayo  hufanywa kwa asilimia 5 ni ile ambayo mwanamke huunguzwa, kutoboa, kukata au kukaza sehemu ya siri ya ndani.

 Wakati baadhi ya jamii zikiendelea kukumbatia ukeketaji kama suala la ‘kiutamaduni’, Shirika la Afya Duniani (WHO)  linaeleza kuwa ukeketaji husababisha matokeo mabaya katika kipindi kifupi ikiwa ni pamoja na mshituko, kutokwa na damu nyingi na matatizo katika njia ya mkojo.

Pia huleta matatizo ya muda mrefu ambayo huweza kumpata mwanamke aliyekeketwa kuwa ni maambukizi ya VVU,  matatizo wakati wa kujifungua, kuongezeka kwa hatari ya vifo vya watoto wachanga, maumivu wakati wa kujamiiana, matatizo ya kisaikolojia na kifo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *