SERIKALI ya Mkoa wa Lindi ikishirikiana na wadau mbali mbali wa elimu ndani na nje ya mkoa, imeazimia kufanya mabadiliko makubwa kwenye ufaulu wa wanafunzi hasa wale wa kidato cha pili na cha nne.
Hali hiyo imetokana na matokeo mabaya ya mitihani ya kidato cha nne iliyofanyika mwaka 2016 yaliyosababisha mkoa huo, hususan Wilaya ya Nachingwea, kushika nafasi ya mwisho kitaifa.
Mkoa huo umeazimia kufanya mikakati ya kufutilia mbali historia iliyodumu kwa muda mrefu kuwa mkoa huu upo nyuma kwa kila kitu, hasa elimu, ambapo imeamua kufuatilia kwa karibu maendeleo ya elimu kuanzia ngazi ya shule hadi ya mkoa.
Nje ya Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi, Katibu Tawala wa Wilaya na Ofisa Elimu Wilaya.
FikraPevu iliwahi kuripoti kuhusu hali duni ya elimu mkoani Lindi pamoja na sababu kadha wa kadha zinazochangia mkoa huo kufanya vibaya kwenye matokeo ya mitihani hiyo ya kitaifa.
Katika kutafuta suluhisho la changamoto hiyo, viongozi waandamizi wa sekta ya elimu mkoani humo wakiwemo wakuu wa shule za sekondari, maofisa elimu wa wilaya na mkoa, wakuu wa wilaya sambamba na mkuu wa mkoa walikutana katika nyakati tofauti kuchambua taarifa za tathmini za ufaulu kwa shule mbalimbali.
FikraPevu imearifiwa kwamba, mambo yaliyojadiliwa kwenye vikao hivyo ni pamoja na kupanga mikakati mbalimbali ya kupandishi viwango vya ufaulu.
Sababu za kutofanya vizuri zabainika
Akisoma taarifa ya tathmini ya ufaulu, Ofisa Elimu (W) Nachingwea, Makwasa Bulenga, alisema sababu za ufaulu mdogo mkoani humo ni kutowepo kwa uwajibikaji na usimamizi imara wa ngazi mbalimbali za elimu kuanzia Ofisa Elimu Mkoa, Maofisa Elimu wa Wilaya zote, wakuu wa idara za elimu, wakuu wa shule pamoja na walimu na jamii kwa ujumla.
Aidha, Bulenga alibainisha kuwa uwajibikaji na usimamizi huo mdogo unachangia kuwepo kwa ushirikiano mdogo hali inayokwamisha utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kishule na hata ile ya serikali.
“Wazazi wanakuwa wagumu kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni wakiamini jukumu hilo ni la mwalimu, walimu nao wanasahau jukumu lao kwa jamii, serikali, kwa taaluma yao na hata kwa mwanafunzi,” alisema.
Aliongeza kusema kuwa, wakuu wa shule nao wanasahau jukumu lao la kusimamia mwenendo wa elimu shuleni hali inayowajengea mazingira magumu wanafunzi.
Hata hivyo, FikraPevu inatambua kwamba, zipo pia changamoto ambazo hazikubainishwa katika tathmini hiyo lakini kimsingi zinaendelea kuziumiza shule nyingi, hususan za Kata.
Changamoto ya uhaba wa walimu bado inaendeshwa kisiasa huku serikali ikiendelea kuiaminisha jamii kuwa walimu siyo tatizo na kwamba idadi yao inajitosheleza.
FikraPevu imebaini kwamba, uhaba wa walimu ni changamoto hasa katika maeneo mengi ya mikoa ya kusini.
Shule ya Sekondari Nachingwea ni miongoni mwa shule kubwa ambapo tayari imepewa hadhi ya kuwa shule ya halmashauri, lakini shule hiyo inakabaliwa na uhaba mkubwa wa walimu hasa wa masomo ya Hisabati, Fizikia, Kemia na Baolojia, ambapo kwa sasa shule hiyo haina mwalimu wa somo la Baolojia kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.
Taarifa zinasema, hali hiyo inaifanya shule hiyo itegemee zaidi walimu wa kujitolea na wale waliopo kwenye mazoezi ambapo kutokana na ukata wa fedha wakati mwingine shule hiyo hushindwa kumudu gharama za kuwalipa walimu hao.
Halmashauri zajipanga
Wadau mbalimbali waliokutana na viongozi wa Mkoa wa Lindi.
Katika kukabiliana na changamoto ya ufaulu mbovu, halmashauri zote zimeamua kuandaa mikakati thabiti ya ufuatiliaji wa elimu ambapo zimetakiwa kuhamasisha uanzishwaji wa makambi ya wanafunzi shuleni kwa vidato vyote vya mitihani, yaani kidato cha 2 na cha 4.
Katika kufanikisha azma hiyo, kila halmashauri imetakiwa kutenga kiasi cha Shs. 130 milioni kutoka kwenye bajeti za ndani katika kugharamia uendeshaji wa makambi hayo.
FikraPevu imeelezwa kwamba, kiasi hicho cha fedha kimetengwa katika mchanganuo wa mafungu mawili ambapo fungu la 1 (takriban Shs. 76 milioni) litaelekezwa kwenye gharama za chakula kwa wanafunzi wote watakaokaa katika makambi hayo sambamba na motisha kwa walimu watakaohusika katika ufundishaji, wakati fungu la 2 (takriban Shs. 54 milioni) litatumika kutoa motisha kwa walimu na kwa shule zote zitakazofanya vizuri kwenye matokeo ya kitaifa mwaka ujao.
Aidha, wakaguzi waliopo kwenye kila halmashauri watatakiwa kufanya ukaguzi wa ndani utakaohusisha shule zote huku wakiangalia na kutathmini mwenendo wa ufundishaji sambamba na changamoto zinazowakabili walimu katika ufundishaji.
Maazimio ya kimkoa
FikraPevu imeelezwa kwamba, maazimio ya kimkoa ni pamoja na kuzitaka shule zianzishe utaratibu wa kufanya mitihani ya kutosha kila mwisho wa mwezi ambapo ripoti za mitihani hiyo zitawasilishwa kwa Ofisa Elimu wa Wilaya husika ambaye ataziwasilisha kwa Ofisa Elimu wa Mkoa.
Aidha, wazazi pia watawajibika kulipa faini zitakazohusisha gharama za uandaaji wa mitihani kwa wazazi wale tu ambao watoto wao hawatafanya mitihani hiyo.
Kwa mwaka wa masomo 2017 shule zote za sekondari mkoani humo, hususan kwa vidato vyote vya mitihani, zitatakiwa kufanya mitihani ya dhihaki (mock) katika awamu mbili.
FikraPevu imeelezwa kwamba, awamu ya kwanza itakuwa ni mwezi Mei na awamu ya pili ni mwezi Agosti.
Sambamba na hilo, kila halmashauri itatakiwa kupanga mitihani ya 'kabla ya mtihani wa taifa' (pre-national examinations) ambayo ripoti zake kwa ujumla zitawasilishwa kwa Ofisa Elimu wa Mkoa.
Ofisa Elimu huyo pia amewaagiza wakuu wote wa shule kusimamia zoezi hilo na kuhakikisha linatekelezwa na akawaomba walimu wote kufuatilia matokeo mabaya ya mitihani ya kidato cha pili mwaka jana, wawasilishe ripoti za tathmini za masomo yao zikiambatana na barua za maelezo ya kwanini wanafunzi wafaulu/hawajafaulu kwenye somo husika.
Hali kadhalika, Bulenga alisema kwa kuwa imefahamika kuwa kwenye shule nyingi wakuu wa shule hawafanyi majukumu yao ipasavyo, serikali ya mkoa imeazimia kuwawajibisha wale wote watakaobainika na tuhuma hizo.
“Wakuu wengi wa shule za sekondari ndio wanasababisha utendaji kazi mdogo kwa walimu na watumishi wengine shuleni, wakati mwingine hata kushusha maadili ya kiutumishi kwa walimu hao,” alisema.
Alitolea mfano mwaka 2016, ambapo Mkuu wa Shule ya Sekondari Matekwe iliyopo nje kidogo ya mji wa Nachingwea, Bwana Mapunda, alisababisha sintofahamu na uvunjifu wa maadili shuleni hapo kutokana na kushindwa kusimamia ipasavyo kanuni za kiutumishi kwa walimu, ambao baadhi yao walikuwa wakijihusisha na mahusiano ya mapenzi na wanafunzi.
Licha ya serikali kutia mkazo suala la wanafunzi kutojihusisha ama kutohusishwa kwenye mahusiano ya kimapenzi yanayoweza kuwasababisha kukatisha masomo yao, lakini mwalimu mmoja wa shule hiyo (jina linahifadhiwa) alijikuta akikiuka maadili ya taaluma yake na kuwa kwenye mahusiano na mwanafunzi wa kidato cha nne shuleni hapo.
FikraPevu imeelezwa kwamba, mwalimu huyo huyo alikuwa kwenye mahusiano na mwalimu mwingine wa kike (jina linahifadhiwa) ambaye alikuja kufahamu kuwa kuna mwanafunzi ana uhusiano wa kimapenzi na 'mpenzi' wake.
Hali hiyo inaelezwa kwamba, ilijenga chuki baina ya mwalimu wa kike na mwanafunzi huyo ambapo mwalimu huyo akishindwa kujizuia hata wakati mwingine kumfukuza mwanafunzi darasani, hali iliyokuwa inapingwa vikali na wanafunzi wenzake huku wakitishia kuwa endapo mwanafunzi huyo atatolewa darasani na wao watatoka.
Mapema mwaka 2017 Ofisa Elimu wa Mkoa wa Lindi alimbadilishia kituo cha kazi mkuu wa shule hiyo, lakini hakuna hatua zozote za kinidhamu zilichokuliwa dhidi ya walimu hao wawili.
Ukiukwaji wa maadili ya utumishi pia umetokea katika Shule ya Sekondari Nambambo iliyopo wilayani Nachingwea ambapo walimu wa shule hiyo wanatambuana kwa makundi waliyoyaunda wenyewe nje ya utaratibu wa kazi.
Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, ndani ya makundi hayo ndimo uhasama na chuki baina ya walimu hao unaanzia ambapo madhara yake ni kupunguza uwajibikaji.
Hali hiyo pia ilimlazimu Ofisa Elimu wa Mkoa kumbadilishia kituo cha kazi mkuu wa shule hiyo, Dickson Mwansele, na kupelekwa Shule ya Sekondari Naipanga iliyopo wilayani humo.
Mbali na shule hizo, FikraPevu imeelezwa kwamba, zipo shule nyingi nchini ambazo watumishi wake kwa makusudi wanakiuka maadili ya utumishi wao lakini hakuna hatua zozote za kinidhamu zinazochukuliwa dhidi yao.
Hatua ya kubadilisha vituo vya kazi kwa wakuu wa shule wasiowajibika ni kama kulisogeza ama kulihamisha tatizo kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.
Katika hatua nyingine, mkoa umeazimia kuanzisha mpango wa chakula shuleni ambapo wazazi watatakiwa kuchangia gharama kwa watoto wao pindi wawapo shuleni.
Hali hiyo imeelezwa kuwa ni hatua nzuri, kwani zipo baadhi ya shule za sekondari mkoani humo, kama vile Shule ya Sekondari Nachingwea ambayo mwanafunzi anatakiwa kufika saa 12:00 asubuhi na kuondoka saa 12:00 jioni huku kukiwa hakuna utaratibu wowote wa kuwawezesha kupata chakula.
Changamoto pekee iliyopo mbele ya mkakati huo ni kubadilisha dhana ya elimubure waliyo nayo wazazi wengi huku wakiamini kuwa hawatakiwi kuchangia chochote.
Kupitia mfuko wa elimu, idara za elimu pia mkoani Lindi zimepokea fedha kiasi cha Shs. 79 milioni kila idara ambapo Shs. 23 milioni kati ya hizo zitatumika kwa ajili ya msawazo wa watumishi wake na kuwabadilishia vituo vya kazi watumishi wake.
Kupitia mikakati hiyo, Mkoa wa Lindi unaweza kuongeza kiwango cha ufaulu kwa kuboresha elimu, lakini jitihada hizo ni lazima zipate ushirikiano wa kutosha kutoka kwenye mamlaka za juu za elimu kama vile Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Utumishi na Baraza la Mitihani la Taifa.
Katika kuboresha ufaulu wa wanafunzi kidato cha pili, Baraza la Mitihani ni lazima libadilishe mfumo wa mitihani unaotumika darasa la saba kwani haumjengei mtoto weledi na ubunifu hasa kwenye somo la Hisabati ambalo mwanafunzi huchagua majibu.
Aidha, mfumo wa 'kuwabeba' wanafunzi kwa kuwapa majibu ili shule ionekane imefaulisha pia unaua vipaji vingi vya watoto hali inayoongeza idadi kubwa ya watoto wasiojua kusoma wala kuandika.
FikraPevu iliwahi kushuhudia mwalimu mmoja wa Shule ya Msingi Nangowe wilayani Nachingwea kwenye mitihani ya darasa la saba mwaka 2016, akiwapa majibu watahiniwa kupitia dirishani huku msimamizi akiwepo.
Kwanini walimu hawa wadanganyifu wanapokutwa na hatia wasifukuzwe kazi kwani ndio wanaoigharimu serikali?
Kwa upande wake, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ipange bajeti ya kutosha kwani fedha za mpango wa elimubure pekee hazitoshelezi.
Shule nyingi zina madeni yanayotokana na upungufu wa fedha, hivyo Wizara inatakiwa kuweka mafungu kwa ajili ya motisha kwa walimu, posho za vikao na gharama za kuandaa mitihani ya ndani.
Walimu wanasemaje
Baadhi ya walimu waliohojiwa na FikraPevu wameipongeza serikali kwa kuchukua hatua hiyo na kusema baadhi vya vilio vyao vimepata majibu, hususan suala la motisha na malipo wakati wa msawazo na kubadilisha vituo vya kazi.
Pia wameipongeza hatua ya serikali kuiwajibisha jamii kwenye suala la mitihani ya kujipima.
Hata hivyo, wameiomba serikali kushirikiana na walimu katika kuzitambua na kuzifanyia kazi changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa majukumu na isiwe mara baada ya mkoa kufanya vibaya kwenye mitihani ndipo serikali inawageukia walimu.
Maoni ya wazazi
Imani kubwa ya wazazi ni katika walimu kwani kwao mwalimu ndio mhimili mkubwa wa mabadiliko ya taaluma na nidhamu ya mwanafunzi. Hivyo, pamoja na kuipokea mikakati hiyo ya serikali, wamewaomba wakuu wa shule kuwa wakali kwa walimu hasa katika ufundishaji.
Wazazi wengi wameonesha kuafiki mkakati wa uchangiaji wa chakula shuleni utakaoendeshwa na halmashauri za wilaya zikishirikiana kwa karibu na wazazi na shule.