Lufusi: Mazingira kwanza, mambo mengine baadaye

Kulwa Magwa

KIJIJI cha Lufusi, kilichopo katika wilaya Mpwapwa, kimesema hekta 34 za miti ziliharibiwa mwaka jana, ambapo watuhumiwa 17 walikamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali, ikiwemo kutozwa faini ya jumla ya sh. milioni 1.3.

Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Jonas Mbogo, anasema fedha hizo zilipatikana kutokana na uendeshaji wa kesi za watuhumiwa hao kijijini hapo, ambao walihukumiwa kwa mujibu wa sheria ndogo za utunzaji misitu walizojiwekea.

Kwa mujibu wa mtendaji huyo wa kijiji ambacho kipo takriban kilometa 64 Kusini, waliamua kutunga sheria ndogo mwanzoni mwa miaka ya 2000 ili kukabiliana na uharibifu wa misitu, kutokana kijiji chao kuwa katika mpango wa utekelezaji wa matumizi bora ya ardhi.

kijiji-Lufusi

Bango linalotoa tahadhari dhidi ya uharibifu wa mazingira katika kijiji cha Lufusi

Mbogo anasema, baada ya kuwakamata waharibifu hao na kulipishwa faini, fedha zilizopatikana zilitumika ‘kukarabati’ maeneo yaliyoharibiwa, kupanda miti mingine na uoteshaji wa vitalu vipya vya miti.

Anasema, licha ya wengi kutozwa faini – wachache waliamriwa kupanda miti mingine ambapo wanatakiwa kuisimamia mpaka itakapokua kufikia viwango vya ile waliyoikata au kuiharibu.

Mtendaji huyo anasema, mafanikio yamepatikana kutokana na usimamizi misitu unavyofanyika, ambapo miti imepandwa na iliyokuwepo inaendelea kutunzwa kisheria.

Jonas-Mbogo

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Lufusi, Jonas Mbogo

Kwa mujibu wa kamati ya mazingira ya Lufusi, kijiji hicho kina sheria zinazotumiwa kusimamia rasilimali ya misitu na uharibifu wa mazingira.

Katibu wa Kamati hiyo, Edward Msumali, anasema watu wanaoharibu miti michache kwa kuikata au kuifyeka hutozwa faini kulingana na uharibifu walioufanya, ambapo faini huanzia sh. 10,000 hadi 100,000.

“Lakini wanaokata miti mingi – hao moja kwa moja huwapeleka mahakamani. Huko ndiko huwa tunapambana nao,”anasema.

Vilevile kamati hiyo huwa na adhabu ya kuwashurutisha waharibifu kupanda miti upya na kuisimamia mpaka inapokua kwa kiwango ilichokuwa imefikia.

Adhabu nyingine kwa mtu anayekata miti au kuharibu mazingira ni kufunguliwa kesi mahakamani kwa mujibu wa sheria ya misitu ya mwaka 2002 na ile ya mazingira ya mwaka 2004; ambazo kwa pamoja zinazuia uharibifu wa mazingira.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Beatus Sendwa, anasema usimamizi wa mazingira ni jukumu lao kubwa la kwanza, ambapo kila uongozi wao unapokutana huwa wanajadili kwanza uhifadhi wa misitu kabla ya mambo mengine.

Uharibifu-ardhi

Uharibifu wa ardhi uliofanywa katika kijiji hicho, mwaka jana

Anasema, pia wana vikao vya uhifadhi ambavyo hufanyika kila inapolazimu bila kujali mpangilio wa ratiba, na kwamba hufanya hivyo ili kuonyesha hawana mchezo na suala la uhifadhi wa miti.

“Ukiniuliza jambo moja nililo na kumbukumbu nalo kila wakati, basi nitakuambia nini kinachoendelea kuhusu misitu na mazingira kwa ujumla wake, “anasema Sendwa.

Ofisa Misitu wa wilaya ya Mpwapwa, Devis Mlowe, anasema serikali inaunga mkono jitihada za kijiji hicho katika utunzaji wa mazingira na imekuwa ikifuatilia kwa karibu shughuli zinazofanyika sehemu hiyo.

Anasema, katika ufuatiliaji huo, huwa wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya sheria ya misitu ya mwaka 2012 na kuwataka waisimamie ili kila anayekata miti akumbane na mkono wa sheria.

Kwa upande wake, Ofisa-Mratibu wa TFCG, Mopilio Mwachali, anasema miti inapokatwa hovyo katika kijiji hicho, shirika hilo husaidia kushughulikia mambo hayo kisheria, ikiwa ni pamoja na kuweka mawakili wanaohakikisha haki inatendeka dhidi ya watu waharibifu.

Sheria hiyo inatoa adhabu kali kwa mtu au taasisi inayothibitika kuharibu misitu ikiwemo kifungo na faini na kwamba, iwapo wakati wa hukumu inasomwa na ile ya mazingira ya mwaka 2004, kiwango cha juu cha faini hakipungui au kuzidi sh. milioni 50 au kifungo kisichozidi miaka saba; ama vyote viwili kwa pamoja.

Pia kifungu cha 160 (1) na (2) cha sheria hiyo kinasisitiza mtu, kijiji au taasisi yenye maslahi ya kisheria ya ardhi inawajibika kulipwa fidia, ambapo haki hiyo inapaswa ilingane na thamani ya ardhi au miti iliyopotea au kuharibiwa na kuwa, thamani halisi ya ardhi huzingatiwa chini ya kifungu kidogo cha (1) cha sheria ya ardhi ya mwaka 1967 na sheria ya ardhi ya 1999.

Kutokana na kuwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi, kijiji hicho kiliamua kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Maeneo yaliyotengwa kitalaamu kwa ajili ya mpango huo ni ofisi za taasisi na serikali, mapori ya miombo, maeneo ya malisho, misitu ya hifadhi, visima vya maji/vituo vya maji na bonde la umwagiliaji.

Mengine ni viwanja vya michezo na burudani, eneo la hifadhi ya ufugaji wa nyuki, msitu wa matumizi ya kuni, msitu wa matumizi ya mbao, zahanati, soko, maduka, bucha, ibada (kwa ajili ya msikiti na makanisa), malisho, matambiko, shule na makaburi.

Mbogo anasema, wakati wanatenga maeneo kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi walilenga kuwa na eneo kubwa la misitu, kupanda miti na utunzaji wake – lengo likiwa siku za usoni wauze hewa ya ukaa.

Ili kufanikisha mambo hayo, kijiji hicho kwa kushirikiana na Tanzania Forestry Conservation Group (TFCG), ambalo ni shirika lisilo la kiserikali, wameunda kamati ya usimamizi wa mazingira na wamekuwa wakiunda vikundi kazi kwa ajili ya kufanikisha malengo yao.

TFCG imekuwa ikitoa msaada wa kitaalamu ambapo imeajiri ofisa- mratibu anayefanya kazi na kamati hiyo kwa pamoja na uongozi wa kijiji hicho.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *