Mabadiliko ya tabia nchi yatishia kahawa

Merali Chawe

WAKATI uzalishaji wa zao la kahawa nchini unatarajia kuongezeka  hadi kufikia  tani 80,000  kwa mwaka ifikapo mwaka 2016 ili kukidhi masoko ya ndani na nje ya nchi, ongezeko hilo huenda lisifikiwe kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mabadiliko ya tabia nchi yamesababisha kuwepo kwa mbadiliko ya hali ya hewa ikiwemo ukosefu wa mvua, hali ambayo kwa kiasi kikubwa imeanza kuathiri kilimo cha kahawa katika baadhi ya mashamba kutokana na mimea yake kukauka kwa kukosa maji. 

Baadhi ya wakulima wa Wilaya ya Mbeya wakizungumzia mabadiliko ya tabia nchi, wamesema athari zake zimeanza kuonekana wazi kutokana na kupungua kwa kiwango cha mvua huku maeneo mengine yakikosa mvua kabisa na kusababisha miche ya kahawa kuathirika kwa ukame.

Wanasema kuanza kukauka kwa miche hiyo kutayumbisha uchumi wa kaya nyingi ambazo zinategemea zao hilo kwa ajili ya kusomesha watoto, kuongeza pato la familia, kumudu huduma za kiafya pamoja na kushiriki katika kuchangia shughuli za kijamii.

Gibson Mposa, mkulima na mkazi wa Kijiji cha Idugumbi wilayani Mbeya, anasema kahawa ni moja ya zao kubwa la biashara linalotegewa wilayani humo hivyo wanaiomba Serikali kulinusuru kwa kuwajengea miradi ya maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

“Kahawa pia inachangia kiasi kikubwa katika pato la Halmashauri ya wilaya,” anaongeza.

Rose Mwakatwila, mkazi wa Kijiji cha Msiha, anasema ukosefu wa mvua za kutosha pamoja na athari zinazotokana na kuathirika kwa zao la kahawa inaweza kuhatarisha amani na usalama katika maeneo anayoishi.

“Shughuli za kilimo cha kahawa ndizo zinategemewa na wengi, hivyo athari zake zinasababisha kukosekana ka mapato, kuna uwezekano watu, hasa vijana, wakajiingiza kwenye uhalifu na pia vita ya kugombea maji baina ya wakulima,” alisema.

Alisema ipo haja kwa kuanzia serikali za vijiji na serikali kuu kuanza kuweka mikakati ya kujenga miundo mbinu ya kilimo cha umwagiliaji pamoja na uhifadhi maji.

Ofisa Kahawa wa Wilaya ya Mbeya, Lupakisyo Masuba, alisema mabadiliko tabia nchi yanayosababishwa na kasi kubwa ya uharibifu wa mazingira, ni miongoni mwa chanzo kikubwa kinachochangia kupunguza kiwango cha mvua na kuleta ukame.

Meneja wa Mradi wa Kuboresha na Kuongeza Uzalishaji wa Kahawa katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, unaofadhiliwa na shirika la Hanns R. Neumann Stiftung la Ujerumani, Webster Miyanda, alisema ili kuepukana na athari hizo ni lazima wakulima kuzingatia na kufuata mafunzo ya kilimo hifadhi mazingira ili kuhifadhi uoto wa asili.

Alisema wao wanachofanya ni kutoa elimu na kuwawezesha wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuboresha uzalishaji wa zao la kahawa ambalo mahitaji yake ni makubwa kuliko uzalishaji.

 

Meneja wa Nyanda za Juu Kusini wa Kituo cha Utafiti wa Kahawa (TaCRI), kilichopo Mbimba wilayani Mbozi, Isaac Mushi, alisema wameanza mpango wa utafiti ambao utawawezesha wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Alisema mabadiliko ya hali ya tabia nchi yameathiri uzalishaji wa zao la kahawa kutokana na hali ya hewa isiyotabirika na mvua zisizotosheleza mahitaji.

“Katika kukabiliana na changamoto hiyo tumezalisha mmea mpya wa kahawa ambao na unakabiliana na ukame, utafiti unafanyika katika kijiji cha Bora na umeweza kudumu kwa miaka miwili,” alisema na kuongeza utafiti unaweza kuchukua miaka mitano hadi saba kukamilika.

Mushi alisema wakulima wadogo ndio wanaoathirka zaidi na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwa hawawezi kumudu kuendesha kilimo cha umwagiliagi na kwamba wanaomudu ni wakulima wakubwa tu.

Aliongeza kusema kuwa wakulima wa kahawa kwa mikoa ya nyanda juu kusini wanategemea mvua zinazoanza mwezi septemba kufanya shughuli zao hali ambayo uzalishaji umekuwa sio mzuri kutokana na ukosefu wa mvua za uhakika.

Mratibu  wa Siku ya Wakulima wa Kahawa  wilayani Mbozi, Mtemi Miya, alisema ubora wa kahawa  katika Mkoa wa Mbeya sio wa kuridhisha kwani kahawa nyingi bado iko kwenye madaraja ya chini kwani msimu wa 2012/2013 karibu asilimia 96.4  ya kahawa yote ilikuwa katika daraja la tisa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *