Maisha magumu yapunguza kasi kuandikisha darasa la kwanza Dar es Salaam

Jamii Africa

KILIO  cha maisha magumu kinaelezwa kuwa ni sababu kubwa ya kushuka kwa kasi ya kuandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza kwa shule za Dar es Salaam.

Takwimu zinaonesha kuwa katika shule nyingi za Manispaa ya Kinondoni, idadi ya wanafunzi wa darasa la kwanza walioandikishwa mwaka huu imeshuka.

Katika kupata ukweli wa “kelele” hizi za hali ngumu kwa wazazi na walezi, FikraPevu imeamua kuanya ziara za kushtukiza katika baadhi ya shule.

Ingawa ni majira ya saa 4 asubuhi, lakini jua linaonekana kuwa kali wakati ninapowasili katika eneo la Shule ya Msingi Makumbusho iliyoko katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Tofauti na shule nyingi, hasa za pembezoni mwa jiji hilo, ambako kelele nyingi husikika hata wakati wa vipindi, hapa ukimya umetanda katika vyumba vingi vya madarasa ingawa katika baadhi ya madarasa hayo kunasikika kelele za hapa na pale.

Baadhi ya vyumba hivyo vinaonekana vimechakaa kutokana na kutokarabatiwa kwa miaka mingi, lakini hilo haliwafanyi walimu 28 na wanafunzi 1,133 wa shule hiyo wasiendelee na vipindi vya masomo.

“Miaka saba iliyopita usingeweza kukuta ukimya kama huu kwa sababu tulikuwa na wanafunzi wengi kuanzia darasa la kwanza hadi la saba, hicho chumba kimoja tu kilikuwa na watoto mpaka 90,” ananieleza mmoja wa walimu wa shule hiyo ambaye anaomba hifadhi ya jina lake.

Mwalimu huyo anasema idadi ya uandikishaji wanafunzi inapungua kwa kasi kubwa kila mwaka, licha ya serikali kupitisha azimio la elimu bure kuanzia shule ya awali hadi kidato cha nne.

Anabainisha kwamba, kwa mwaka huu pekee, wameandikisha wanafunzi 109 tu wakati mwaka 2016 walioanza darasa la kwanza walikuwa 168, idadi ambayo hata hivyo ilikuwa ndogo kulinganisha na wanafunzi zaidi ya 200 waliokuwa wakiandikishwa katika miaka ya nyuma hata baada ya shule kugawanywa kwa shule hiyo na kuanzishwa kwa shule ya msingi Victoria iliyopo kwenye eneo hilo hilo.

“Darasa la kwanza lina mikondo mitatu ambapo kwa wastani kila chumba kina wanafunzi 36 kwa mwaka huu ikilinganishwa na wanafunzi 56 mwaka 2016,” anasema mwalimu huyo na kuongeza kwamba kipindi cha nyuma hali ilikuwa mbaya zaidi kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi iliyokuwepo.

Mwalimu huyo, ambaye anaishi katika eneo la Makumbusho, anasema sababu kubwa za kushuka kwa idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa darasa la kwanza ni kupanda kwa gharama za maisha, hususan kodi za pango na huduma nyingine za kijamii, jambo lililowalazimu baadhi ya wakazi kwenda kuishi pembezoni mwa jiji.

“Hali ya maisha ni ngumu, kodi za nyumba zimepanda sana kiasi kwamba watu hawawezi kuzimudu, hivyo kuamua kutafuta sehemu zenye unafuu pembezoni mwa jiji, wapo wengine ambao wamejinyima na kuamua kujenga nyumba nje kabisa ya jiji kwa sababu maeneo ya katikati hakuna viwanja,” anaongeza mwalimu huyo na kusema sababu hizo kwa kiasi kikubwa zimewakimbiza watoto wengi mjini ambao wangepaswa kuandikishwa kwenye shule hiyo na nyinginezo.

Tatizo la kushuka kwa idadi ya watoto wanaoandikishwa darasa la kwanza limeikumba pia shule jirani ya Victoria iliyotoka ubavuni mwa shule hiyo ya Makumbusho.

Mmoja wa walimu wa shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 540 na walimu 25, ambaye naye aliomba kutotajwa jina lake kwa kuwa si msemaji, alisema kwamba mwaka huu wameandikisha watoto 68 wakati mwaka 2016 waliandikisha watoto 80, ukiwa ni upungufu wa wanafunzi 12.

Hata hivyo, tatizo la kupungua kwa idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa darasa la kwanza haliko kwa shule hizo mbili tu, bali inaonekana limezikumba shule nyingi za katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, kupungua kwa idadi ya uandikishaji wanafunzi katikati ya jiji kumesababishwa kwa kiasi kikubwa na kupanda kwa gharama za maisha huku wakazi wengi wakielezwa kuhamia pembezoni ambako walau kodi za nyumba na vyumba ni nafuu.

Aidha, sababu nyingi ambayo inatajwa kuchangia hali hiyo ni suala la uzazi wa mpango kwa wakazi wa katikati ya jiji, ambako taarifa zinasema matumizi ya njia za kisasa za uzazi huo ni makubwa kuliko pembezoni, hali iliyopunguza idadi ya vizazi.

Baadhi ya tafiti zinaeleza kwamba, kati ya asilimia 27 ya wanawake wanaotumia njia za uzazi wa mpango nchini Tanzania, asilimia 80 wako mijini. Walimu wa shule za Makumbusho na Victoria, wanahofia kwamba hali hiyo ikiendelea kuna uwezekano wa baadhi ya vyumba vya madarasa kubaki vitupu kwa kukosa wanafunzi.

“Kama uandikishaji umepungua kwa wanafunzi 59 mwaka huu ikilinganishwa na mwaka 2016, maana yake kuna hatari ya kubaki na mikondo miwili tu siku zijazo,” anaeleza mwalimu kutoka Makumbusho. Kwa upande mwingine, shule hizo zinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa walimu huku Manispaa ya Kinondoni ikisema idadi ya sasa inatosha.

Inaelezwa kwamba, kwa miaka takriban minne sasa, Manispaa ya Kinondoni haijaajiri walimu kwa maelezo kuwa waliopo wanatosheleza mahitaji, uamuzi ambao unadaiwa kuathiri ufundishaji katika shule nyingi.

“Hapa tunao walimu 28 na walimu watatu tu ndio wanaofundisha darasa la kwanza, lakini kusema kweli tunatakiwa tupatiwe walimu watano zaidi kwa darasa la kwanza kutokana na wingi wa vipindi,” anaeleza mwalimu kutoka Makumbusho na kuongeza kwamba kwa wastani mwalimu mmoja anafundisha vipindi 5 vya masomo tofauti kwa siku.

Licha ya changamoto hiyo, mwalimu huyo anasema kitaaluma shule hiyo imeendelea kufanya vizuri katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ambapo kati ya wanafunzi 145 walihitimu mwaka 2016, wanafunzi 139 walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2017.

Uchakavu wa majengo ni changamoto nyingine inayozikabili shule hizo mbili zilizoko katika eneo moja.

FikraPevu bado inaendelea kufuatilia ufanisi wa elimu mkoani Dar es Salaam.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *