Majanga tena: Tumejiandaaje kukabiliana na kipindupindu jijini Dar es Salaam?

Jamii Africa

HIVI karibuni, mtu mmoja Ramadhan Kiumbo ‘Popo’, mkazi wa Kibada wilayani Kigamboni aliripotiwa kufariki dunia na wengine 12 kulazwa hospitalini kutokana na ugonjwa wa kipindupindu.

Marehemu alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni ya Vijibweni ambako pia wagonjwa hao wengine walikuwa wamelazwa.

Tukio hilo lilisababisha shule zote za Halmashauri ya Kigamboni kufungwa siku ya Ijumaa kwa hofu ya wanafunzi kupata maambukizi.

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa, alithibitisha kuwepo kwa ugonjwa huo ndani ya halmashauri yake na kwamba wengine walikuwa wakipatiwa matibabu.

"Ni kweli ugonjwa huu umeingia, tumechunguza na kugundua umeanzia eneo la Kichangani ambapo watu wote waliomeletwa hospitali waliupatia eneo hilo walipokwenda kwenye msiba,” alisema na kuongeza kwamba maofisa wa afya walikuwa wamechukua hatua kwa kupulizia dawa katika nyumba ili kuua vijidudu vya ugonjwa huo.

Taarifa zilizopo ni kwamba, baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam tayari yamekwishavamiwa na ugonjwa huo, hususan Vingunguti na Temeke.

FikraPevu inafahamu kwamba ugonjwa huo hatari na unaoua haraka kwa miaka mingi umekuwa ukishambulia sana Jiji la Dar es Salaam na kusababisha vifo vingi.

Hata hivyo, hofu iliyopo ni kwamba, huenda ugonjwa huo ukaleta madhara makubwa jijini humo hasa kutokana na kuwepo kwa dalili za kuanza kwa mvua za masika, ambazo kwa kiasi kikubwa husababisha maambukizi kuongezeka.

Katika miaka yote, ugonjwa huo umekuwa ukileta madhara makubwa jijini Dar es Salaam huku jitihada za kupambana nao zikiwa ndogo, achilia mbali mikakati madhubuti ya kuutokomeza.

Mazingira ya jiji hilo ni machafu, miundombinu duni huku wananchi wenyewe wakiwa hawana utamaduni wa kudumisha usafi.

FikraPevu inatambua kwamba, moja ya njia zinazochangia kuenea kwa kipindupindu ni matumizi ya maji machafu, yanaweza kuwa ya visima ama bomba, ambayo hayawekwi dawa kuua vijidudu na kama hayatachemshwa kabla ya kutumika.

Kwa kuwa miundombinu mingi, hasa ya ukusanyaji wa majitaka, ni duni jijini humo, maji machafu, hususan ya mvua, hutiririka na kujaa kwenye visima ambavyo vinatumiwa na jamii kwa shughuli mbalimbali.

Kuziba kwa mitaro, uchakavu wa miundombinu, ujenzi holela unaosababisha kuziba kwa njia za maji, pamoja na tabia isiyofaa ya baadhi ya wakazi kuzibua mabomba ya maji machafu na kuyaelekeza kwenye mitaro na makazi ya watu, ni mambo yanayosababisha vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu (Vibro Cholerae) vinavyoishi kwenye maji yaliyochafuliwa kwa kinyesi, kusambaa na kuleta madhara.

Aidha, FikraPevu inafahamu kwamba jiji hilo lina idadi kubwa ya visima venye vimelea ambavyo vinaweza kusababisha magonjwa ya milipuko, hasa kipindupindu na homa za matumbo.

Maeneo mengi ya Dar es Salaam yanapata huduma hafifu ama kutofikiwa kabisa na maji yanayosambazwa na Kampuni ya Kusambaza Maji Dar es Salaam (Dawasco), hivyo kutegemea maji ya visima ambayo siyo safi wala salama, hasa maeneo ya Buguruni, Kigogo, Yombo, Vingunguti na kwingineko.

Maji mengi ya visima, vifupi na virefu, ambavyo wakazi wa jiji hilo wamevichimba kiholela, mara nyingi huwa hayawekwi dawa za kuua vijidudu, hali ambayo ni ya hatari.

Wakazi wengi wanaotumia maji hayo ya visima wanakiri kuwa hawajawahi kuona maji yanayoingia kwenye matanki na kuuzwa kwa wananchi yakiwekwa dawa ili kuua vimelea, tofauti na ambavyo mamlaka za maji hutakiwa kutibu maji kabla ya kuwafikia wananchi.

Ingawa maji ya visima virefu na vifupi ni muhimu katika kutatua tatizo la maji, lakini hatua stahiki zinastahili kuzingatiwa, hususan katika kuyatibu kabla ya kutumiwa, hali itakayosaidia kupunguza uwezekano wa magonjwa ya milipuko kama kipindupindu na homa za matumbo.

Mamlaka zinazohusika na huduma ya maji ni lazima kuweka utaratibu wa lazima kwa kupima ubora wa maji kila mwaka katika visima vilivyopo na kuhakikisha vipya vinachimbwa baada ya kukamilisha taratibu zote na siyo kuacha kila mmoja kuchimba na kuuza maji holela.

Inawezekana tunatatua shida ya maji kwa kuchimba visima, lakini tunaweza kuwa tunazalisha matatizo mengine makubwa, kama kipindupindu ambacho kimegharimu maisha ya wananchi wengi.

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na Dawasco wanapaswa kuhakikisha miundombinu ya ukusanyaji wa majitaka inaimarishwa ikiwa ni pamoja na kukarabati ile iliyopo na iliyochakaa pamoja na kuweka mingine iliyo bora.

Kinyume chake, kipindupindu kitaendelea kuvinjari jijini humo kila mwaka na kusababisha vifo visivyotarajiwa.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *