Wakati Tanzania ikitajwa kuwa miongoni mwa nchi duniani zenye mahitaji makubwa ya maji, serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inatekeleza miradi mbalimbali kulinda vyanzo vya maji ikiwemo mito.
Mapema mwaka huu Tanzania na serikali ya Malawi waliingia kwenye makubaliano ya kuendeleza Bonde la Mto Songwe ambalo ni chanzo kikubwa cha maji katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na baadhi ya mikoa ya Malawi.
Makubaliano hayo yamejikita katika kutekeleza Programu ya Maendeleo ya Bonde la Mto Songwe (SRBDP) ambayo ina lengo la kulinda chanzo hicho cha maji ili kuhakikisha maji safi na salama yanapatikana kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa umeme, kilimo cha umwagiliaji na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Programu hiyo ambayo imepitia hatua za awali za upembuzi yakinifu, usanifu wa mradi lakini wakati huu iko kwenye hatua ya utekelezaji wa ujenzi wa bwawa ambalo litakuwa mahususi kukusanya maji kutoka katika mto Songwe ili yatumike kwa shughuli za kiuchumi.
Mradi huo wa SRBDP unagharimu Dola za Marekani milioni 829 na kukamilika kwake kutatua tatizo la mafuriko ambayo hutokea kila mwaka kwa wakazi wanaoishi pembezoni mwa mto Songwe. Mafuriko hayo husababishwa na kingo za mto kutokuhimili maji ambayo hutapika na kuingia kwenye makazi ya watu na kuharibu miundombinu na mazao.
Inaelezwa kuwa zaidi ya watu laki 1 huathirika na mafuriko ya mto Songwe kila mwaka ambao ni mpaka wa nchi za Tanzania na Malawi. Ili kuhakikisha maji yanatumika kwa matumizi endelevu, nchi wahisani kwa kushirikiana na sekta binafsi wamejikita kuwekeza miradi mbalimbali ya kiuchumi itakayokuwa na manufaa kwa wananchi wa nchi zote mbili.
Daraja la mto Songwe linalotenganisha mpaka wa Malawi na Tanzania
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ambayo ni mshirika muhimu imetoa Dola milioni 72 kuanza utekelezaji wa awamu ya tatu ya kujenga bwawa ambalo litazalisha umeme wa megawati 180.2 na kilimo cha umwagiliaji ambapo hekta 6,200 zimetengwa kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali.
Maji yatakayopatikana yatasambazwa kwa wananchi, ujenzi wa miundombinu ya jamii (bararabara, shule, na vituo vya afya). Miradi mingine ni uanzishaji wa viwanda vidogo na vya kati, uvuvi, utalii na uboreshaji wa mazingira, hususan kuimarisha kingo za mto ambao ni mpaka wa nchi zetu mbili.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa wakati huo, Mhandisi Gerson Lwenge amesema mradi huo utakuwa na manufaa mbalimbali ya kiuchumi na kijamii, “Kwanza kabisa, tunajenga bwawa ambalo litakuwa na matumizi mbalimbali. Tunatumaini kupitia bwawa hilo tutazalisha umeme wa maji na kuendeleza skimu za umwagiliaji” amesema.
Mpaka wa mto Songwe ni mpaka wa kimataifa ambao unatenganisha Tanzania na Malawi na sehemu kubwa ya mpaka inaundwa na Mto Songwe ambao chanzo chake kinapatikana katika upande wa Kusini Magharibi mwa mlima Rungwe na mji wa Tukuyu.
Mto Songwe ukipata maji unajaa haraka na kutapisha maji nje ya kingo zake na kutengeneza mifereji ambayo husababisha kubadilika kwa mipaka. Ili kuhakikisha mipaka inabaki mahali pake, bwawa linajengwa ili maji yote yakusanywe pamoja na kuwalinda wananchi dhidi ya mafuriko.
Mpaka huo wa mto Songwe unaelekeza maji yake kwenye Ziwa Nyasa ambapo linakutana na nchi tatu za Malawi, Msumbiji na Tanzania. Mto Songwe una urefu wa kilomita 200 na ardhi yenye rutuba ya kilomita 4,200 ambao ina manufaa kwa zaidi ya wakazi 52,000 wa nchi zote mbili.