Usalama wa wanahabari na rushwa: Mjadala uliokwama

Jamii Africa

Leo tarehe 27 Machi 2013 ilikuwa siku nyingine ambapo wanahabari wameshindwa kufikia muafaka juu ya suala la usalama wao.

Mjadala huu uliandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) lengo likiwa ni kutafuta mbinu ya kujilinda hususani baada ya kushambuliwa kwa mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Absalom Kibanda. Mada ilikuwa “Usalama wa Waandishi wa Habari Tanzania”

Kwa sura iliyojitokeza leo ni kwamba wanahabari wanapenda kuwakosoa watu wengine lakini hawapendi kujikosoa wao wenyewe wala kukosolewa.

Mjadala ulichochewa na mtoa mada Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Bi Valerie Msoka ambaye alianza kuchanganua adui wa mwanahabari ni nani hasa.

“Nimebahatika kufanya kazi na vyombo mbali mbali vya habari kama vile BBC na hata Umoja wa Mataifa kila niendako kama mwanahabari niliweza kumfahamu adui yangu ni nani, kwa hapa Tanzania ni vigumu kumfahamu adui yangu mimi kama mwanahabari” anasema.

Akifafanua zaidi kauli yake hiyo anasema katika nchi alizopata kuzitembelea wale waliokuwa ‘maadui wa watu’ au wa wananchi katika ujumla wao ndiyo pia walikuwa maadui wa wanahabari.

Anasema hali ilikuwa hivyo Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Uganda Kaskazini, Sudan ya Kusini, Iraq na hata Libya, lakini kwa Tanzania anasema inakuwa vigumu sana kujua namna ya kujikinga kutokana na aina ya mashambulizi yanayofanywa.

“Je adui yangu ni nani? FFU, Usalama wa Taifa, vyama vya siasa? Nauliza kwa sababu wala sijui ni chama gani kinatuma watu ili kuwashambulia wanahabari, hali hii inanitatiza sana,” anasema Msoka. 

Anakumbusha mauaji ya Daud Mwangosi, Issa Ngumba, na hata mashambulizi kwa wanahabari yaliyofanyika Mtwara hivi karibuni kwa kile kilichodaiwa kwamba wanaripoti kwamba mgogoro wa gesi umekwisha wakati bado upo.

Anauliza  je adui yangu ni mmiliki wa chombo cha habari? Mwisho anasema anachokiona ni woga na anawaasa waandishi watafute namna bora ya kuripoti inapotokea mwanahabari amedhuriwa kama ilivyokuwa kwa Mwangosi kwani tukio hilo liliripotiwa katika namna ya kuwaogofya na kuwavunja moyo wanataaluma wengine husuani wanawake.

Baada ya Msoka alikuja mualikwa mwingine Prof. Nicholls Boas, Mtanzania anayefundisha taaluma ya habari nchini Marekani ambaye alionekana kutema sumu ambayo ilileta mzozo kidogo ukumbini hapo New Africa Hotel.

Msomi huyo anasema kwamba vyombo huru (binafsi)  vya habari ndivyo vyenye uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko katika nchi yoyote. Anasema vyombo vinavyomilikiwa na serikali kama TBC na Daily News ni kwa ajili ya propaganda za serikali ambazo zinaweza zisiwe na manufaa kwa wananchi wote katika ujumla wao.

Zaidi ya hayo msomi huyo anasema kwamba katika nchi nyingi zilizokuwa katika mfumo wa chama kimoja kinachojiona kimo hatarini kung’olewa madarakani ni kawaida kutumia jeshi la polisi, maafisa wa usalama wa taifa na hata mahakama ili kubakia madarakani. Na vivyo kuwatisha na hata kuwaua wanahabari huwa ni mkakati wa kuzimisha sauti pinzani.

Mwanasheria mbobevu profesa wa sheria na Mwenyekiti wa Umajumui wa Kiafrika (Pan-Africanism) Issa Shivji anasema haitoshi kuzungumzia usalama wa waandishi wa habari wakati wanajamii wote wapo hatarini anakumbushia tukio la hivi karibuni ambapo askari polisi alimuua kwa risasi mwendesha boda boda na yeye (polisi) akauawawa kwa mawe.

Wakati mjadala ukiendelea ilionekana kuna kauli  iliwakera baadhi ya wahariri waliopata kufanya kazi Daily News na wale ambao bado wameajiriwa na kampuni anayochapisha gazeti hilo. Wa kwanza alikuwa mhariri mmoja mkongwe nchini aliyesema kwamba hakuna serikali yoyote duniani isiyokuwa na chombo cha habari ikiwamo Marekani na VOA, Uingereza na BBC.

Baadaye alisimama mhariri wa Daily News Bw. Deo Mushi akasema vyombo vya serikali ndivyo vinazingatia maadili zaidi kwa sababu waajiriwa wake wanalipwa mishahara na haki zingine stahiki.

Kinyume chake baadhi ya makampuni binafsi hufikisha hadi miezi mitatu kabla hayajawalipa waandishi mishahara yao hali ambayo husababisha wengine wakiuke maadili yao na kuanza kuchukua hongo hivyo kuidhalilisha taaluma hiyo adhimu.

Hoja hiyo ilimuibua Katibu Mtendaji wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), mhariri mkongwe Mzee  Henry Muhanika ambaye alisema mjadala ulikuwa umeandaliwa kwa ajili ya masuala ya usalama na wala siyo maadili wala maslahi ya wanahabari.

Mara Prof. Boas aliibuka na kusema maslahi ni sehemu ya usalama wa wanahabari. “mwandishi hawezi kuwa na usalama iwapo ana njaa, njaa tu yenyewe ni tishio la usalama wa wanahabari.

Akionekana kumuunga mkono profesa huyo alikuwa Lilian Timbuka kutoka magazeti ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyesema kwamba baadhi ya magazeti ya kampuni binafsi yanaandika sana habari za kununuliwa (pr stories) hali inayoonyesha kwamba habari hizo hupikwa na wale wanaozilipia kwa wanahabari.

Lakini Prof akaibuka tena na kuvitetea vyombo binafsi kwa nguvu zote. Ndipo yule mhariri mkongwe aliyepata kuwa Daily News akaamuka na kusema prof. asiongee kama kibaraka wa nchi za magharibi na kwamba anajua tu nadharia lakini hajawahi kufanya kazi katika chumba cha habari hivyo hana haki ya kuyasema yale ayasemayo.

Kidogo amani ipotee hivyo ilibidi mhariri aondoke ili kulinda amani katika mdahalo huo. Mhariri Godfrey Lutego anasema adui namba moja wa wanahabari ni wanahabari wenyewe kwa kukosa maadili na kukubali kutumiwa na wanasiasa wenye tamaa ya madaraka wakiwamo mafisadi.

Lutego anasema taaluma nyingine zote zina viwango na mtu akishindwa kuvifikia anaondolewa katika orodha au daftari la wanataaluma lakini kwa wanahabari hali ni tofauti, “ mtu anaweza kuwa dereva wa  taxi na kesho akaitwa mwanahabari kwa sababu tu anaweza kuandika, hili ni jambo la hatari kubwa,” anasema Lutego.

Naye mhariri Deodatus Balile alisema siyo sahihi kuwashambulia tu waandishi na wahariri bali tuwajengee uwezo wa mafunzo ya usalama ndipo tuanze kuwakosoa kwa kile kinachoonekana kwamba wamekosa maadili.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Uhuru wa Habari Kusini mwa Afrika-Tawi la Tanzania (MISA-Tan) Tumaini Mwailenge anasema ‘njaa’ za wanahabari zisiwafanye wakaiweka rehani taaluma yao.

Akifunga mjadala huo afisa mwandamizi wa MCT, Austerius  Banzi anasema wanahabari wa Tanzania sasa wawe makini kwani kuteka, kutesa, kubaka na hata kuua ni sehemu ya siasa chafu.

================

Vidodoso kwa fikra zako msomaji

  1. Mkurugenzi aliyepita wa TBC Bwana Tido Mhando inadaiwa alinyimwa kuongeza mkataba katika wadhifa wake kwa sababu alitoa haki sawa kwa CCM na CHADEMA na vile vile kwa kuruhusu mgombea wa wa CCM, Jimbo la Ubungo, Bi Hawa Ng’umbi kudhalilishwa na wapinzani wake.
  2. Mhariri wa Daily News aliandika tahariri tena ukurasa wa mbele wakati wa Uchaguzi Mkuu, mwaka 2010, akimlenga Dkt. Slaa na kuandika Padri huyu (Slaa) hawezi kuwa rais wa tano wa Tanzania!

Tafakari mambo haya mawili katika muktadha wa mjadala wa leo

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *