Makosa ya Kimtandao: Ijue Kesi ya Kikatiba(Namba 9 ya mwaka 2016) ya Jamii Media

Jamii Africa

Tarehe 4 mwezi wa tatu mwaka 2016 Kampuni ya Jamii Media inayoendesha mtandao maarufu wa JamiiForums Ilifungua Kesi ya Kikatiba katika Mahakama Kuu ya Tanzania kesi namba 9 ya mwaka 2016. 

Kesi hiyo inatarajiwa kutolewa hukumu kesho tarehe 22 Febuari saa 6 mchana.

HOJA ZA JAMII MEDIA:

Kesi hii ilikuwa na hoja zifuatazo; 
– Kupinga matumizi ya kimabavu ya kifungu cha 32 cha sheria ya Makosa ya Kimtandao(CyberCrime Act), ambacho kimenainika kutoa nguvu kubwa kwa Jeshi la Polisi kutoa amri ya uchunguzi wa taarifa za siri/binafsi za watumiaji wa mitandao.

– Kupinga matumizi ya kifungu cha 38 cha Sheria ya Makosa ya Kimtadao ambacho kinapingana na haki ya mtu kusikilizwa endapo kifungu cha 32 kitakuwa kimetumika. Kifungu cha 38 kinalipa Jeshi la Polisi uwezo wa kwenda mahakamani na kusikilizwa bila uwepo wa upande wa pili (Exparte).

NINI KINAWEZA KUTOKEA?

Inawezakana Mahakama ikadai kuwa imeona kifungu cha 32 kiko sawa kikatiba ila ikumbukwe Jamii Media wanapinga 'Matumizi mabaya' ya kifungu hicho. Hoja yao inakolezewa kwa madai kwamba Jeshi la Polisi lilianza kutumia kifungu hicho bila kanuni kutungwa. Wanasheria wao wanasema kifungu hicho cha 32 kinakinzana na haki ya faragha, na uhuru wa kujieleza.

YALIYOTOKEA KATIKATI:

Katika hatua za awali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliweka  mapingamizi ya awali ya kisheria sita,  ambapo moja ya mapingamizi mwasheria  wa serikali alisema shauri hilo namba 9 halikustaili kuwa shauri la kikatiba. Tarehe 24 Agusti 2016, Mahakama Kuu iliyatupilia mbali mapingamizi yote sita ya awali na kutoa amri kesi hiyo kuendelea kusikilizwa.

KWANINI KESI YA KIKATIBA?
 
Toka kutungwa kwa Sheria ya Makosa ya Kimtandao 2015, Jeshi la Polisi kupitia Kitengo chake cha Makosa ya Kimtandao "Cybercrimes Unit" na cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai "Criminal Investigation Department(CID)" wanadaiwa kuwa wakituma barua mbalimbali wakimtaka Mkurugenzi wa JamiiForums kuwapa taarifa za siri/binafsi za wateja wake kwa lengo la 'kufanya uchunguzi' na 'kuwafungulia kesi' baadhi ya watumiaji wa mtando huo. Polisi walikuwa wakituma barua hizo chini ya kifungu cha 32 cha Sheria ya Makossa ya Kimtandao.

Katika barua hizo zaidi ya kumi, zote zilikuwa zikitaka taarifa watu walioandika masuala ambayo Jamii Media wanadai zina maslahi mapana ya kitaifa(Public interest) na nyingne zikiwa za kisiasa.

Katika barua zote Jeshi la Polisi ziliweza kujibiwa na wanasheria wa Jamii Media, huku wanasheria wakionesha nia ya kutoa ushiriakiano endapo Jeshi la Polisi lingesema wazi makosa yaliyokuwa yametendeka na kama wangeeleza taarifa hizo za wateja zinaenda kutumika kwa maslahi gani. Hii ilifanyika kwa nia njema (Good faith) ili kuiwezesha JamiiForums kuangalia uhalali wa kisheria kabla ya 'kutoa ushirikiano' kwa Jeshi hilo. Mwanasheria pia alinukuliwa nyakati kadhaa akisema watumiaji wengi waliokuwa wakitafutwa walikuwa wameandika habari au kutoa taarifa za rushwa, ufisadi na ukwepaji kodi na hivyo aliishauri Jamii Media kuwaona kama waibua maovu “Whistle Blowers” wenye nia njema kwa nchi.

KWANINI USHIRIKIANO ULISHINDIKANA!?

JamiiForums ina wajibu wa kulinda taarifa za watumiaji wake kisheria na Kikatiba, lakini pia wanatambua wana wajibu wa kisheria kutoa ushiriakiano kwa Mamlaka kama kuna taarifa watahitaji, lakini  lazima maombi hayo yafanywe chini ya amri zilizo halali na zinazofuata sheria na kuzingatia haki za binadamu.

Pamoja nia ya kutaka kutoa ushirikiano iyoonyeshwa na Jamii Media kwa Jeshi la Polisi katika barua zao zote zaidi ya kumi, Polisi walikataaa kutoa taarifa juu ya nia ya Jeshi hilo kwa wateja wao. Polisi walizidi kutuma barua na mnamo tarehe 4 Februari 2016, Jeshi la Polisi lilimuandikia Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media, ndg Maxence Melo barua ya kuashiria kuwa lina nia ya kumshitaki chini ya kifungu cha 22 kwa kuzia uchunguzi wa Jeshi la Polisi. 

UAMUZI WA JAMII MEDIA:

Baada ya Jamii Media kuona kuna vitisho vya kufunguliwa mashitaka walishauriana na wanasheria wao na kuamua kufungua kesi ya kikatiba. 

Toka kesi ifunguliwe, Jeshi la Polisi walisimama kwa muda kuandika barua hadi mwezi Septemba 2016 walipomhoji Maxence juu ya Barua walizokuwa wakimwandikia na akiwanyima 'ushirikiano'. 

Ulitokea ukimya wa Polisi tena hadi Disemba 13, 2016 walipomkamata ndg Maxence Melo na kumnyima dhamana kwa siku takribani nne(4) na kumfungilia mashitaka chini ya kifungu cha 22 huku Jeshi likijua wazi kuna kesi ya Kikatiba kuhusiana na suala hilo.

KUHUSU HUKUMU:

Hukumu ya kesi hii inasomwa kesho tarehe 22 mwezi Febuari 2017 chini ya jopo la Majaji watatu, wakiongozwa na Mwenyekiti Jaji Mtukufu Koroso. Majaji wengine wanaosimamia kesi hiyo ni Jaji Mtukufu Kitusi na Jaji Mtukufu Khalfani.

 

 

JE, NINI HATMA YA UHURU WA KUJIELEZA MITANDAONI?

Tukutane Mahakamani!

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *