Serikali yakiri utata vifo vya wachimbaji na kufunga mgodi

Jamii Africa

SERIKALI Mkoani Mwanza, imeyafunga machimbo matatu ya madini yaliyopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, baada ya uongozi wa machimbo ya Ishokelahela kutoa kudaiwa taarifa zinazokinzana, kuhusu duara moja lililotitia na kusadikiwa kuua wachimbaji kadhaa.

Machombo hayo yamefungwa kwa muda wa miezi mitatu kuanzia jana Januari 9 hadi Aprili mwaka huu, na kwamba mbali na taarifa hizo za kukinzana, kuanzia sasa wachimbaji hao wadogo wadogo wanatakiwa waunde vikundi maalumu ili Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini iwape leseni kwa ajili ya kazi hiyo ya uchimbaji madini.

RC Ndikilo akiwa na ulinzi mkali wa askari polisi akikagua machimbo ya Ishokelahela muda mfupi kabla hajayafunga machimbo hayo jana

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Evarist Welle Ndikilo ambaye ndiye aliyeyafunga machimbo hayo, alisema jana kwenye mkutano na wachimbaji hao wadogo wa Ishokelahela, aliyataja machimbo yaliyofungwa kuanzia juzi kuwa ni Mwamazengo, Ikuna na Ishokelahela.

Alisema, Serikali imelazimika kuyafunga machimbo hayo kwa lengo la kutaka kuweka utaratibu mzuri wa uchimbaji madini katika maeneo hayo, ikiwa ni pamoja na wachimbaji wenyewe kujiweka katika utaratibu mzuri wa kisheria wa kuunda vikundi na kupewa leseni za uchimbaji madini.

“Kuanzia leo Januari 9 2012, machimbo ya Ishokelahela, Ikuna na Mwamazengo nimeyafunga rasmi. Hii inatokana na Serikali kutaka kuwawekea utaratibu mzuri wa kuwapa leseni muwe wachimbaji halali. Kuitwa wachimbaji haramu mimi inaniuma sana na sipendi muitwe hivyo.

“Lakini, pia Januari 4 mwaka huu tulipata taarifa kwamba kuna ajali hapa ya duara. Nilikuja na wenzangu kutaka kujua ukweli wa mambo, lakini taarifa zilizotolewa na viongozi wenu zinachengana. Lakini kwa hili sitaki tukosane, mkikaidi mimi nitakaa pembeni halafu mkutane na watu wasioongea.

“Huyu anasema waliokuwemo ndani ya duara ni watu wanne, mwingine watu watano, mwingine watu tisa…sasa tumeona kuna tatizo la utoaji taarifa kwa sababu utaratibu unaotumika hapa ni mbovu. Tukianza Aprili muwe kwenye vikundi na leseni zenu”, alisema Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Ndikilo.

Katika hotuba yake ambayo ilionekana kuwagusa wachimbaji hao na kuridhia nayo, Ndikilo alimtaka Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Libelatus Barlow kuhakikisha jeshi lake kuhakikisha hakuna mtu atakayeendelea na uchimbaji katika machimbo ya Ishokelahela, Ikuna na Mwamazengo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Injinia Evarist Welle Ndikilo akifafanua jambo kwa wachimbaji wadogo wa mgodi wa Ishokelahela uliopo Wilaya ya Misungwi mkoani humu jana, kabla ya kuyafunga machimbo ya Ikuna, Mwamazengo na Ishokelahela kwa muda wa miezi mitatu.

Hata hivyo, Mkuu wa mkoa huyo alitoa muda wa kuanzia Januari 9 hadi 14 mwaka huu wachimbaji na vifaa vyao vya uchimbaji wame wameondoka maeneo hayo, vinginevyo hatua kali zitaanza kuchukuliwa kwa yeyote atakayekaidi amri hiyo halali ya Serikali.

“Namtaka Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, asimamie zoezi hili, na awe ananiletea taarifa kila siku kinachoendelea katika machimbo haya. Na ifikapo Januari 16 RPC anipe ripoti ya kwamba hakuna mchimbaji wala vifaa katika machombo yote haya. Ondokeni wengine mkaoe na kuolewa”, alisema RC Ndikilo, huku baadhi ya wachimbaji wakimpigia makofi.

Alisema, Desemba 28 mwaka jana waliketi kwenye kikao na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja wakiwemo wadau wa sekta hiyo na viongozi wa wachimbaji wadogo wa machimbo hayo, kisha Waziri Ngeleja kuridhia Wizara yake kutoa leseni kwa wachimbaji wote watakaojiunga kwenye vikundi katika maeneo hayo.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa wachimbaji wa madini katika machimbo ya Ishokelahela, Hassan Rajab aliwasihi wachimbaji hao wadogo kutii amri ya Serikali bila kushurutishwa, lakini alisema: “Hapa tunaona kama kuna njama ya Serikali au watu fulani kutaka kutuondoa sisi wachimbaji wadogo. Kuna hujuma…ila muda wa miezi mitatu si mwingi tutaondoka”.

Rajab alisema, maelezo yaliyotolewa na Mkuu wa mkoa wa Mwanza yanalengo la kujenga na si kubomoa, hivyo kwa niaba ya wachimbaji wengine wote aliahidi kuondoka maeneo hayo hadi hapo Aprili Serikali itatakapoyafungua, na aliwaomba wachimbaji hao kujiunga vikundi ili wapewe leseni.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *