Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli ametangaza kuipandisha hadhi Manispaa ya Mji wa Dodoma kuwa Jiji kuanzia leo Aprili 26, 2018.
Rais Dkt Magufuli ameyasema hayo leo, katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa maadhimisho ya sherehe za miaka 54 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar mjini humo.
Amesema kwa mamlaka aliyonayo ameona vema Dodoma ipate hadhi ya jiji ikizingatiwa kuwa mikakati ya serikali kuhamia katika jiji hilo inaendelea.
“Nilifanikiwa kuiona Dodoma ilivyokuwa. Imejengwa kila mahali, na Dodoma kweli ni Makao Makuu. Tulizoea Dar es Salam ndiyo yalikuwa makao makuu kwa wakati ule, na paliitwa Jiji. Nikaona niangalie katika nchi yetu tuna Halmashauri ngapi, tuna manispaa ngapi na mimi nina mamlaka gani katika kutengeneza majiji au manispaa au kadhalika,” amesema Rais Magufuli na kuongeza kuwa,
“Nikakuta Arusha ni jiji, Tanga ni jiji, nikaambiwa Dodoma ni Manispaa, nikasema haiwezekani. Kwahivyo kuanzia leo Dodoma linakuwa Jiji,”
Vile vile Rais Magufuli amempandisha hadhi Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi kuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kutokana na kupanda hadhi yake.
Hatua hiyo inaifanya idadi ya majiji hapa nchi kufikia sita ambapo Tanzania ina majiji ya Dar es Salaam, Jiji la Tanga, Jiji la Arusha, Jiji la Mwanza, Jiji la Mbeya na Jiji jipya la Dodoma.
Kuna vigezo mbalimbali vinavyotumika ili kuipa manispaa au mji hadhi ya kuitwa jiji. Lakini vigezo hivyo hutofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine. Hata hivyo, baadhi ya mambo ambayo ni muhimu ni upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii, miundombinu ya barabara zinazoingia na kutoka katikati ya jiji. Pia uwepo wa huduma za kiutawala ikiwemo ofisi za serikali.
Dodoma ni mji mkuu wa nchi, lakini tangu Tanzania ipate uhuru 1961; serikali haikupeleka shughuli za utawala katika jiji hilo. Alipoingia madarakani 2015, rais John Magufuli alianzisha kampeni ya kuhamia Dodoma.
Taarifa zilizopo ni kwamba wizara zote, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu tayari wako Dodoma na mwishoni mwa mwaka huu, rais atahamishia ofisi yake na ikulu katika jiji hilo jipya.
Sanamu ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo jijini Dodoma
Historia ya Dodoma
Kulingana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jina la Dodoma lilizaliwa hata kabla ya Mji wenyewe. Zipo hadithi nyingi zinazoeleza jinsi jina hilo lilivyopatikana, lakini hadithi inayokubaliwa na wengi ni hii: Tembo alikuja kunywa maji katika Kijito cha Kikuyu na akakwama matopeni. Baadhi ya wenyeji waliomwona walipiga mayowe na kusema “yadodomela” ambayo kwa lugha ya Kigogo maana yake ‘amezama’.
Na tangu wakati huo mahala hapo pakawa panajulikana kama Idodomya pale mahali
alipozama yule tembo. Haijulikani kwa uhakika lini jina lilianza kutumiwa. Kwa kukisia huenda eneo hilo lilianza kutumika tokea mwaka 1860.
Msafiri wa Kizungu H. M. Stanley ambaye alipitia sehemu hiyo mnamo mwaka 1874 aliliita Dodoma. Lakini hakuna kumbukumbu ya kimaandishi ya zamani zaidi kuhusu jina hilo lilivyopatikana.
Mji wa Dodoma
Miaka mingi iliyopita, wakati wa kipindi cha wahamiaji wa Kiafrika, wakazi wa Dodoma ambao ni wafugaji waliweka makazi yao katika eneo linalojulikana sasa kama Mkoa wa Dodoma. Katika kulinda mifugo yao, wakazi hawa waliishi kwa kutawanyika na hasa ukizingatia kuwa walikuwa wachache mno kwa Idadi.
Mbali na shughuli za ufugaji, walijishughulisha pia na Kilimo cha kujikimu, kutengeneza ala za muziki na usukaji wa vikapu: waliweza pia kuanzisha usindikaji mdogo wa kutengeneza Chumvi, Nta na Samli. Pamoja na kufanya kazi hizo, kikwazo kikubwa kwa wakazi hawa kilikuwa ni hali ya hewa.
Mvua zinaponyesha vizuri wanapata chakula cha kutosha lakini mvua zinapokuwa haba, hali ya chakula inakuwa ngumu sana. Mwaka 1890 Utawala wa Kijerumani uliingia mkoani Dodoma. Na miaka 18 baadaye yaani mwaka 1912, eneo la Dodoma likawa eneo la Utawala wa Wilaya. Mji wa Dodoma ukiwa makazi ya kudumu ulianzishwa mnamo mwaka 1910 kwa
ujio wa reli Kuu ya Kati. Reli Kuu ya Kati ambayo ndiyo hasa ilisababisha kuwepo na kukua kwa Mji wa Dodoma ulitanguliwa na msafara wa Binadamu uliotokana na biashara dhalimu ya Utumwa. Msafara huo ulikuwa kiungo kati ya Bara na Pwani.
Kabla ya Tanganyika kupata Uhuru wake tarehe 09 Desemba 1961, Mkoa wa Dodoma ulikuwa ni sehemu ya Jimbo la Kati (Central Province). Mwaka 1963, Jimbo la kati liligawanywa na kupatikana Mikoa ya Dodoma na Singida. Mkoa wa Dodoma ulianzaishwa kwa Tangazo la Serikali Na.450 la tarehe 27 Septemba,1963.