Ni wakati sahihi kwa Tanzania kutumia roboti kwenye matibabu ya binadamu?

Jamii Africa

Licha ya kuimarika kwa huduma za afya nchini China bado wagonjwa wanaoenda kutibiwa katika hospitali nyingi wanalazimika kukaa kwenye foleni kwa dakika kadhaa kabla ya kumuona daktari na kupata matibabu. Lakini hospitali moja katika mji wa Kusini wa Guangzhou imeanza kushughulikia tatizo hilo kwa  kuvumbua mashine mpya ya kompyuta inayotumia roboti kutoa huduma.

Kwa mujibu wa Hospitali ya Kati ya jimbo la  Guangzhoua imejumuisha mfumo huo wa mashine zinazoendeshwa kwa kompyuta katika shughuli zake ikiwemo huduma ya kwanza, vipimo (CT Scans), utunzaji wa kumbukumbu za wagonjwa na usambazaji wa vifaa na dawa.

China ambayo  ni mshindani mkubwa wa Marekani duniani katika ukuaji wa teknolojia hasa ya mashine za kisasa (Artificial intelligence) – inaamini kuwa  matumizi ya roboti yanaweza kupunguza tatizo la uhaba wa madaktari kwenye vituo vya afya na hospitali.

Taarifa za kitabibu za mwaka 2016 zinaeleza kuwa nchini humo madaktari 2 huudumia wagonjwa 1,000 ukilinganisha na Switzerland ambayo ni madaktari 4 kwa wagonjwa 1000 na Uingereza (3/1000). Teknolojia hiyo inatarajiwa kutumika zaidi katika nchi ambazo zina idadi kubwa ya wazee ambao wanahitaji uangalizi wa karibu wa madaktari.

Teknolojia hiyo imevumbuliwa na kutolewa na kamapuni ya Titan Tencent na iFlytek ambazo zinafanya kazi na hospitali hiyo kuunda mifumo ya kompyuta ambayo itafanya kazi ambazo zingefanywa na watu ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma za afya kwa wananchi wa jimbo la Guangzhoua.

Pia wametengeneza program maalum ya mtandao wa WeChat ambayo inawawezesha wagonjwa kuingia kwenye akaunti ya hospitali na kusajili taarifa zao. Mtandao huo umeunganishwa na daktari roboti ‘intelligent doctor’ ambaye anafanya mahojiano na mgonjwa na kushauri vipimo anavyopaswa kufanyika.

Mfumo huo unasaidia wagonjwa kuepukana na foleni ya kuwasubiri madaktari wa kawaida. Mtumiaji wa program hiyo aliyejulikana kwa jina la Zeng aliulizwa maswali 24 kuhusu afya yake. Zeng alifikiri maumivu ya kongosho aliyonayo yanatokana na tatizo la mfumo wa chakula, lakini mashine hiyo ilimuambia anatakiwa kumuona daktari anayeshughulikia magonjwa ya uzazi kwa wanawake.

Taarifa za hospitali hiyo zinaeleza kuwa walitumia karibu miaka 2 kutafiti zaidi ya kumbukumbu  100,000 za dijitali za matibabu ambazo zinaweza kutumika kwa miaka 12 ijayo. Programu hiyo pia imeunganishwa na data zingine milioni 300 kutoka hospitali zingine kutoka 1990 ili kuhakikisha mashine hizo za kompyuta zinafanya kazi ya matibabu kwa ufanisi mkubwa unaofikia asilimia 90 na kutibu zaidi ya magonjwa 200 bila kuwepo daktari wa kawaida.

Pia Hospitali hiyo inatumia utambuzi wa sura kutengeneza mafaili hasa kwa wagonjwa wanaotibiwa kwa mara ya kwanza. Baada ya kurekodi video fupi, mfumo unalinganisha sura ilitochukuliwa kwenye video hiyo na ile iliyopo kwenye mfumo wa taifa wa kutunza kumbukumbu za wananchi.

Licha ya kuanza kutumika kwa mfumo huo mashine za kisasa hasa roboti katika baadhi ya hospitali za China, lakini changamoto inabaki kuwa ni nani atawajibika ikiwa mfumo huo utafanya makosa au utatoa matibabu yasiyoendana na mgonjwa.

Hata hivyo, matumizi ya mfumo huo wa roboti kwenye hospitali yanahitaji daktari wa kawaida kusaini ripoti na maelekezo ya kitabibu.

 

Ni wakati sahihi Tanzania kutumia teknolojia hiyo?

Tanzania kama zilivyo nchi zingine duniani, bado inakabiliwa na uhaba mkubwa wa madaktari ambapo umekuwa ni tatizo sugu kwenye sekta ya afya.

Kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa Tanzania bado ina uwiano usioridhisha wa daktari kwa wagonjwa ambapo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita ilikuwa katika nafsi ya mwisho duniani kwa kuwa na uwiano wa daktari mmoja kwa wagonjwa 50,000.

FikraPevu imelezwa kuwa kwa sasa uwiano kati ya daktari na wagonjwa nchini ni daktari mmoja kwa wagonjwa 25,000, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko uwiano wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo linaitaka Tanzania kuwa na daktari mmoja kwa wagonjwa 8,000.

Kulingana na takwimu za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa sasa Tanzania ina upungufu wa madaktari unaofikia zaidi ya asilimia 49. Hadi 2017 upungufu huo ulifikia watumishi wa afya 95,059 ambapo waliopo ni 89,842 ili kukidhi mahitaji yote wanahitajika watumishi 184,901 katika vituo vya afya na zahanati.

Uvumbuzi wa teknolojia hiyo ya kisasa inaweza kuwa mbadala wa tatizo la uhaba wa madaktari nchini lakini changamoto inabaki, kama taifa tumejiandaje kupokea na kutumia mfumo wa roboti kwenye matibabu? Kwasababu mfumo huo unahitaji umakini na rasilimali fedha na watu wa kuendesha mitambo hiyo ya kisasa.

Serikali inashauriwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuvumbua teknolojia ya kisasa itakayosaidia kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya afya ili kuhakikisha afya za wananchi zinalindwa na kuboreshwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *