Yusuf Manji aondolewa Quality Plaza, apewa siku 14 kulipa deni

Jamii Africa

Hatimaye Makampuni matano yanayomilikiwa na Mfanyabiashara Yusuf Mehbub Manji yameondolewa katika Jengo la Quality Plaza linalomilikiwa na Shirika la Hifadhi ya Jamii PSPF.

Jengo hilo lipo Kitalu Na. 189/2 na liko mkabala na Barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam.

Sababu inayotajwa ya Makampuni hayo kuondolewa katika jengo hilo ni deni la kodi ya pango linalofikia kiasi cha Shilingi bilioni 13.

Hatua ya kung'olewa makampuni hayo katika jengo hilo ambalo ni mali ya Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma ni baada ya mpangaji kushindwa kuondoka kwa hiari baada ya kupewa saa 24.

quality_plaza

Makampuni yaliyondolewa ni Quality Group Company Limited, Gaming Management Limited, Q-Consult Limited, Quality Logistics Company Limited, na International Transit Investment Limited.

Jeshi la Polisi lilisimamia wakati kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart ikizihamisha kampuni hizo za Yusuf Manji.

Inadaiwa kuwa Mfuko wa PSPF kwa muda mrefu umekuwa unaidai Kampuni ya Quality Group fedha hizo za upangaji, lakini kila inapotakiwa kulipa imekuwa ikikwepa na kukimbilia mahakamani kuweka pingamizi la kulipa ili iendelee kukaa bure na kwamba uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa Novemba 24, umemtaka aondoke ndani ya saa 24 na kulipa deni analodaiwa.

Pia mmiliki wa kampuni hizo, japo amekwisha ondolewa katika jengo hilo amepewa muda wa siku 14 kisheria awe amelipa deni hilo na kama atashindwa kulipa mali zake zitakamatwa na kuuzwa ili kupata fedha za kulipa deni analodaiwa na PSPF.

SAKATA LILIANZIA KWENYE KAMATI YA BUNGE YA POAC IKIWA CHINI YA ZITTO KABWE

Sakata hili lilianza mwaka 2011 kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) enzi hizo ikiongozwa na Mwenyekiti wa wake Mbunge Zitto Kabwe, kipindi hicho Shirika hilo lilikuwa na hali mbaya kifedha kiasi cha Serikali kuombwa na POAC kuwekeza kwenye shirika hilo ili kulinusuru.

Katika barua ya PSPF mwaka 2011 kwenda kwa kampuni ya Image Properties & Estate inayosimamia uendeshaji wa Quality Plaza, mfuko huo uliitaka kampuni ya Quality Group Limited kuondoka mara moja katika jengo hilo vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa.

“Unaelekezwa kuitimua haraka Quality Group Limited kwa kushindwa kutimiza masharti ya mkataba wa pango,” inaeleza sehemu ya barua hiyo ya Aprili 1, 2011 iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi Adamu Mayingu, kwenda kwa Image Properties & Estate.

Jengo hilo ni mali ya PSPF na Manji alipanga baada ya kuliuza lakini akawa halipi kodi.

Katika maelezo ya wakili wa PSPF (kwa wakati huo), Benitho Mandele, ambayo iliwasilishwa mahakamani ilieleza kwamba Manji anadaiwa kodi ya kuanzia Aprili, 2009 hadi Desemba 2010, hivyo jumla ya deni lote kwa mwaka 2011 lilikuwa dola 2,335,189.06 za Marekani, wakati shauri hilo lilipowasilishwa mahakamani na sasa limefikia shilingi za kitanzania bilioni 13.

Mjadala kuhusiana na suala hili unaendelea katika Mtandao wa JamiiForums

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *