Mashine za kuvuta maji ‘zinazochimba dhahabu’

Kulwa Magwa

NIMEAMKA mapema na kufika katika kijiji cha Kibangile, kilichoko wilayani Morogoro. Umbali kutoka kijiji cha Mtamba, nilipolala, hadi Kibangile kwa pikipiki ni dakika zisizodi saba na daladala hutumia kama dakika 15 hivi.

Nimefika Kibangile kabla ya saa 1:00 asubuhi nijue na kuona mambo yanayoanza kutendeka muda huo, ambapo katika vijiji vingi nchini huo ni wakati wa kwenda shamba kwa wakulima; na kwa mijini watu huwahi vibaruani au ofisini.

Kwa muda niliofika, nimewahi sana maana watu wengi hawaajamka na wachache naowaona hawajaondoka majumbani kwenda kwenye kuhangaika. Natumia muda huo kuzunguka huku na kule kuangalia mandhari nzuri ya kijiji hicho, kwani ni kijiji kilichozungukwa na misitu minene yenye miti mizuri.

Ni katika kijiji hicho ndipo ulipo msitu wa Kimboza, mojawapo wa misitu ya zamani sana nchini iliyohifadhiwa kwa mujibu wa sheria. Huo ni msitu uliohifadhiwa kwa sheria ya usimamizi wa misitu na una walinzi wake.

Hata hivyo, kama ilivyo ada kwa nchi yetu, watu hawaachi kufanya mambo yao, maana ukataji miti na usafirishaji mbao na magogo unafanyika ‘kwa sana’.

Baada ya kutembea huku na kule, narejea katika barabara kuu ya magari, jirani kabisa na zilipo ofisi za serikali na shule ya msingi ya kijiji hicho.

Hapo nawakuta vijana waliopumzika mithili ya watu wasiokuwa na kazi. Kwa muda ule matarajio yangu ilikuwa kuwaona wakiwa na majembe mikononi. Naungana nao, tunaendelea kupiga soga!

Kwa dakika chache za kukaa nao nagundua kwamba kundi lile la vijana saba wenye umri wa kati ya miaka 15 – 25 hivi, walikuwa wakiwasubiri wenzao waende kwenye mihangaiko, maana muda mwingi walikuwa wakiwasiliana nao kwa simu na wakati mwingine kuwagombeza kwa kuchelewa.

Pili, nagundua kwamba eneo hilo la jirani na ofisi ya kijiji na shule linatumiwa na vijana kama kituo cha kusubiriana kabla hawajaenda katika shughuli yao – shughuli ya uchimbaji madini katikati na kandokando ya mto Wami/Ruvu, unaotegemewa na mamilioni ya wakazi wa mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es salaam.

wami-river-morogoro

Mandhari ya mto Wami ambayo haijaathiriwa na uchimbaji madini katika kijiji cha Kibangile, mkoani Morogoro

Mto huo pia unategemewa na wadau wengine kufanikisha biashara zao zikiwemo kampuni za vinywaji zinazofanya kazi zake katika mikoa hiyo.

Tatu, nagudua kuwa kumbe miongoni mwa vijana wanaokutana sehemu hiyo, wamo wanaovuta ‘sigara kubwa’ (bangi), kwani kwa dakika chache nilizokaa nao s hapo wamevutana kando mara kadhaa ‘kulipuliza’.

Hata hivyo, wakati hayo yote yakiendelea, kundi moja la vijana 13 linaonekana mbali likija kwa kasi. Vijana wanatembea mithili ya wanaofukuzwa, huku mikononi wamebeba zana za kazi kama majembe, makoleo (chepe), makalai na mabeseni.

Nashtuka – lakini siwaulizi nilio nao. Nabaki kukodoa macho. Niliokaa nao wanaendelea kuwahimiza wajao kwa kuwapigia miluzi na kelele wakiwataka wawahi.

Hatimaye vijana wale wanafika na kutusalimia. Wenzao wanawatupia ‘madongo’ kwa kukiuka makubaliano yao ya jana, ambapo walikubaliana wakutane kabla ya saa 1:00.

Kilichofuata, wenyeji wangu wananiaga. Wanaondoka zao huku wakigeuka geuka nyuma kana kwamba kuna kitu wanachokizungumza juu yangu. Kwa haraka kabla ya kuagana nao, nilihesabu majembe 10, makala saba na makoleo 11. Hata hivyo, hatimaye wanatokomea msituni.

Baada ya muda, naona pikipiki mbili zikiwa zimebeba mashine za kuvuta maji zikienda upande waliokwenda vijana wale. Hizo ni mashine ambazo nimezowea kuziona zinatumiwa kuvuta maji kutoka shimoni, mtoni na ziwani ambazo wakati mwingine hutumiwa kumwagilia shambani.

Nafikiria zinakokwenda wapi mashine hizo. Najiuliza hivi kijiji hiki kidogo watu wanafanya kilimo cha umwagiliaji? Mwisho naamua kufuatilia zilikokwenda nikajione kilimo kinavyofanyika.

Njiani nakutana na pikipiki zile zinarejea zilikotoka, lakini kwa mbali nawaona vijana wengine tisa hivi wanaokwenda niendako wakitoka upande mwingine wa kijiji, miongoni mwao wakiwa wamebeba makoleo matatu, makalai manne huku mmoja akiwa na jembe.

Nikiwa mbali kidogo na vijana wale waliokuwa mbele yangu, nakutana na mzee mmoja wa makamo akiwa na jembe. Namsalimia – anageuka na kuniangalia, nami namsimamisha.

Najitambulisha kwake na kumtajia kazi nayofanya kuwa ya utafiti wa misitu, namwambia ni mwanafunzi wa chuo kikuu – kisha namuuliza kuhusu misafara mingi ya vijana niliowaona inakokwenda.

Naam, mzee huyo anasita! Ananiuliza kulikoni niulize kuhusu vijana wale, ilhali natafiti misitu? Namjibu kwa kifupi kwa kuwa nimewaona wengi na mimi nakwenda waendako ndiyo maana nataka kujua.

Mzee yule ‘ananiamini’. Ananiniambia wale ni wachimba dhahabu wanaofanya shughuli zao mtoni na kwamba, hata ngurumo nazosikia kwa mbali za mashine zinatoka waliko.

Kwa kuwa ‘ameniamini’ namuuliza kulikoni wawe na mashine kana kwamba kuna migodi, ananiambia ndizo wanazotumia kupunguzia maji sehemu wanazofanyia kazi zao.

Hata hivyo, mzee huyo ananionya huko waendako na waliko watu hao si vizuri nikaenda, maana katika siku za hivi karibuni wamekuwa wanajihami kwa visu na mapanga tangu serikali ilipozuia harakati zao kwenye mto huo.

Mzee huyo ananiambia zaidi kwamba watu wale wanaweza kunifanya lolote kwa kuwa hawanijui, na huenda wakaniona kuwa mpelelezi anayefuatilia nyendo zao. Baada ya maongezi na mzee huyo, nageuka nyuma na kuanza kurejea nilikotoka. Njiani naendelea kukutana na vijana waliobeba ‘zana za kazi’.

Hata hivyo, kwa mbali nimesikia ngurumo za mashine inayoashiria kwamba ziko nyingi. Narudi kijijini kuonana na uongozi wa kijiji kujua harakati za uchimbaji dhahabu mtoni zinavyoendelea.

affected-wami

Mandhari ya mto Wami yaliyoathiriwa na uchimbaji wa dhahabu katika kijiji cha Kibangile, mkoani Morogoro

Ofisa mtendaji wa kijiji, George Malecela, ambaye ni mgeni akiwa na siku 10 tu ofisini ananiambia katika majibu yake kwamba uchimbaji wa dhahabu katika mto huo umepungua.

“Ungefika mwezi wa kumi (Oktoba, mwaka jana) ungekuta mto mzima wamejaa (wachimba dhahabu) na ungeshangaa kuona kila hatua 10 ndani ya mto kuna mashine ya maji inayowapunguzia maji, lakini tangu wapigwe marufuku na serikali wamepungua. Unaowaona mmoja mmoja wasikutishe, “anasema Malecela.

Uchungu nilio nao wa mto huo unanisukuma kubishana na mtendaji. Namwambia nimekutana na msururu wa vijana wanaofikia 30 wakienda kazini. Jibu lake linanikata makali; “mbona wachache? – hao tu?”

Nazungumza naye kwa kina – kisha naongea na viongozi wengine. Naaga na kuondoka. Hata hivyo, swali langu halijapata jibu hadi leo; “kumbe hata mashine za maji zinachimba dhahabu?”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *