Mauaji ya Viongozi wa Dini: Maaskofu Mbeya waishukia CCM na Serikali yake!

Thompson Mpanji

MAASKOFU  mkoani Mbeya wametoa tamko zito kwa serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kufuatia mfulululizo wa matukio ya mauaji ya viongozi wa dini na vurugu zinazoendana  na vita ya kiimani kuwa ni matokeo ya serikali ya Chama cha mapinduzi (CCM) kuibeba dini ya kiislamu.

Maaskofu hao wa jukwaa la wakristo mkoani Mbeya wanaoundwa na mabaraza ya madhehebu  ya TEC, CCT na PCT wametoa tamko hilo leo, (Februari 18, 2013) mbele ya waandishi wa habari katika ukumbi wa kanisa la Pentekoste,jijini hapa kuwa kutokana na ukimya wa serikali ya chama cha mapinduzi katika matukio dhidi ya wakristo viongozi hao wanatarajia kutoa ujumbe huo wa hekima kwa waumini wao siku ya ibada ya jumapili, Februari 24, 2013 ili waamue la kufanya juu ya Chama Cha Mapinduzi.

"Ushahidi  wa CD na DVD za sheikh Ilunga na ndiyo matokeo haya lakini serikali ni kama imebariki vitendo hivi na leo tumeshuhudia Padre Evaristi Mushi  wa kanisa Katoliki Parokia ya Minazi Miwili Zanzibar ameuawa kwa kupigwa risasi,Mchungaji Mathayo Kichila wa Geita aliyechinjwa,padre wa kanisa Katoliki Zanzibar aliyepigwa risasi mwezi  disemba, makanisa yamebomolewa na vitu vya thamani kuharibiwa,lakini serikali ipo kimya,"alisema Katibu wa Jukwaa  hilo. Askofu Damianos  Kongoro wa kanisa la Pentekoste.

Alisema kwa nini wasite kusema kwamba serikali ya chama cha Mapinduzi inaibeba dini ya kiislamu kwa kuwa jukumu la serikali  ya chama tawala  ni kuhakikisha wananchi wote  wanaishi kwa amani na utulivu lakini haipo hivyo kwa serikali ya awamu ya nne.
 
Limesema sehemu ya tamko hilo kuwa mshukiwa wa kwanza anayejuwa kila kitu ni Sheikh Ilunga aliyesambaza CD na DVD kuhusu mikakati ya kuwauwa wachungaji,mapadre na Maaskofu na matokeo yake yameanza kuonekana lakini bado yupo huru  na madhara yameanza kujitokeza.
 
"Serikali inatushangaza kwa viongozi wa kikristo wakiuawa na kufanyiwa vurugu inasema ni wahuni lakini wakifanyiwa unyama viongozi wa kikristo  inasema tuvumiliane wakati mchungaji ameuawa Buselesele mkoani Geita na kikundi kinachodhaniwa ni wanaharakati wa kiislamu wenye jazba na ghadhabu kali inayodaiwa kutokana na mvutano wa wakristo na waislamu kuhusu nani mwenye haki kisheria kuchinja nyama,hatua zilizochukuliwa haziridhishi wala kukidhi matakwa ya wananchi wapenda amani,"walisema.
 
Wametolea  mifano ya Mwenyekiti wa CCM Rungwe ,John Mwankenja aliyeuawa baada ya kupigwa risasi kwa mambo yanayodhaniwa ni ya kisiasa serikali ilichukuwa hatua madhubuti na kutuma wachunguzi kutoka Dar es saalam na wananchi waliridhika na uchunguzi huo iweje kuchukulia kiurahisi suala la viongozi wa kikristo..
 
"Ili wakristo wote nchini warudishe imani yao kwa serikali ya CCM mambo yafuatayo ni lazima yachukuliwe hatua za haraka iwezekanavyo, serikali izingatie utawala wa sheria kulingana na ahadi yake katika kushughulikia masuala ya kijamii na siyo vinginevyo, suala la kuuwa lisichukuliwe kama mazoea na inapotokea serikali lazima ichukuwe hatua inayostahiki kwa kuzingatia utawala wa sheria,tunataka serikali itueleze ni ushahidi gani zaidi inayoutaka kuliko ule uliopatikana kwenye CD na DVD zilizotolewa na sheikh Ilunga kama kweli inazingatia utawala wa sheria,"wamesema.
 
Wameongeza"tunataka serikali iwajibike kutolea ufafanuzi kauli ya waziri wa Nchi Steven Wasira inayohusu haki ya kuchinja kwa waislamu kama inatokana na sheria gani ya nchi,kama serikali inatekeleza utawala wa sheria tunataka wakristo tuwe na machinjio na bucha zetu kulingana na imani yetu,"
 
Viongozi hao wamesema kama serikali haitachukuwa hatua za makusudi katika kutekeleza madai yao kama viongozi wa dini ya kikristo watachukuwa hatua ya kuwaambia waumini wao kwamba serikali ya CCM inaibeba dini ya kiislamu na wao watajuwa la kufanya.
 
Hata hivyo Maaskofu hao  wamesema Pamoja na kutaka utekelezaji wa haraka kutoka kwa serikali bado wamewaomba wakristo wawe katika hali ya maombi na utulivu kwa wakati huu ambapo wapo  katika vita ya kiroho ili mungu awaimarishie amani ambayo ni nguzo ya taifa na kwamba tamko hili rasmi la jukwaa la wakristo mbeya lisomwe katika makanisa yote siku ya Jumapili Febrauri 24, 2013.
 
Tamko hilo limesomwa kwa Mkuu wa Mkoa kwa niaba ya Rais ambapo nakala zimesambazwa kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Tanzania Christian forum Taifa, Mwenyekiti wa the Tanganyika Law Society, Wabunge wa Mkoa wa Mbeya na vyombo vyote vya habari mkoani Mbeya.

=========

TAMKO:

MHESHIMIWA NDG. ABAS KANDORO,

KAMA MKUU WA MKOA NA MWAKILISHI WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE MKOA WA MBEYA, TUNAPENDA KUSOMA MBELE YAKO TAMKO RASMI LA JUKWAA LA WAKRISTO MKOA WA MBEYA (TCF).

NDUGU MKUU WA MKOA,

“HAKI HUINUA TAIFA BALI DHAMBI NI AIBU YA WATU WOWOTE” (Mit. 14:34).

Katika mkutano wa jukwaa la Wakristo Tanzania mkoa wa mbeya ulionyika tarehe 12/02/2013 Jijini Mbeya, wajumbe tulitafakari kwa undani juu ya hali inayoendelea kujitokeza katika nchi yetu na hasa katika mahusiano baina ya dini mbili kuu UKRISTO NA UISLAMU.

Jukwaa hilo lilijumuisha taasisi zake kuu (yaani mabaraza ya Madhehebu ya Kikristo) Tanzania Episcopal Council (TEC), Christian Council of Tanzania (CCT) na Pentecostal Council of Tanzania (PCT).

Mbali na mambo yake ya kawaida jukwaa hilo lilitafakari utekelezaji wa Serikali juu ya tamko Rasmi la jukwaa la Wakristo kitaifa lililotolewa tarehe 06/12/2012 na kusomwa katika makanisa yote ya Kikristo nchini kwenye sikukuu ya Krismas tarehe 25/12/2012. Katika tafakari letu jukwaa la Wakristo wa Mkoa wa Mbeya tumeona kuwa kunabaadhi ya mienendo inayojitokeza katika nchi yetu ambayo kama isipodhibitiwa na kukomeshwa na Serikali italeta athali kubwa na hata kuondoa amani na uthabiti (Stability) wan chi.

Katika kutafakari kwa jukwaa juu ya athari zinazoweza kujitokeza, kumekuwepo na mambo yanayotendeka waziwazi yenye athri kubwa kwa amani na usitawi wan chi na wanchi wake kwa ujumla. Kwa mfano, uchochezi, kashfa, matusi na uchokozi wa wazi unaofanywa na baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu kupitia vyombo vya habari vya kidini (rediona magazeti), mihadhara, kanda za video, CD na DVD pamoja na kauli zinazotolewa na viongozi wa dini hiyo kwenye baadhi ya nyumba zao za ibada(ushahidi upo kama vile uhamasishaji wa Sheikh Ilunga) pasipo serikali kuchukua hatua stahiki na badala yake kubaki kimya au kupambana na wanaofichua harakati hatarishi kwa utulivuwa nchi.

Miongoni mwa harakati hatarishi zinazosambazwa kwa njia ya CD na DVD za Sheikh Ilunga, kuhusu kuua Wachungaji, Mapadri na Maaskofu zimeanza kuwa matokeo mabaya; kwani Padri kule Zanzibar alipigwa risasi na watu walioitwa na serikali wahuni na sasa kifo.

Kimetokea na mchungaji Mathayo Kachila kule Buselesele Mkoani Geita na kikundi kinacho dhaminiwa ni wanaharakati hao wa kiislamu wenye jazba na gadhabu kali inayotokana na mvutano uliopo kati ya wakristo na waislamu kuhusu nani mwenye haki kisheria KUCHINJA WANYAMA. Hatua zinazochukuliwa na Serikali hazilizishi wala kukidhi matakwa ya wananchi wapenda amani.

Tuna mifano kadhaa ya matukio kama haya yaliyojitokeza kwa wanchi wenzetu moja ni ile ya wenzetu aliyepigwa risasi kule Rungwe Ndg. John Mwankenja (Mwenyekiti wa CCM Rungwe) aliyepigwa risasi kwa mambo yanayodhaniwa kuwa ni ya kisiasa) Serikali ichukuwe hatua madhubuti kwa kutuma wachunguzi kutoka Dar es salaam kwa swala hilo na wote tuliridhika kwa hatua hizo madhubuti. Hatua kama hizo mbona hazichukuliwi katika masuala haya ya kidini na badala yake Serikali inakaa kimya au ina chukua hatua ambazo kimsingi hazitatui tatizo ili wananchi waridhike na Seeikali yao? Je tuseme Serikali inaangalia haiba (Personality) za watu au aina ya vikundi? Swala la uchinjaji lilipo jitokeza kule Mwanza waziri wan chi ndg. Steven Wasira alienda na kutoa majibu mepesi katika swala zito je, tuseme aliyoyatamka huko yalikuwa ni KAULI YA SERIKALI au kauli yake mwenyewe? Na kama yake mwenyewe mbona Serikali haijakanusha waziwazi? Na kama ni kauli ya serikali hiyo haki ya kuchinja kwa waislamu inatokana na sheria zipi za nchi? Je huo ndio utawala wa sheria tuliyoahidiwa na serikali ya awamu ya nne kuwa itatenda kazi kwa kuzingatia utawala wa sheria.

Kupigwa risasi kwa Pdri na kuuwawa kwa mchungaji kunathibitisha hazma halamu na batili ya “Ua, chinja” mapadri, wachungaji na maaskofu iwe kwa siri au kwa wazi iliyohasisiwa na Sheikh Ilunga ambayo sio tu inahatarisha amani ya nchi lakini pia inavunja haki za kuishi za binadamu zilizoainishwa katika katiba ya serikali ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania. Aidha harakati hizi zina muelekeo wa kudhoofisha ukristo Tanzania kama sio kuumaliza kabisa.

Pamoja na mambo mengine kinachosikitisha ni namna ambavyo serikali inavyoyashughulikia mambo mazito yanayotikisa amani na utulivu wan chi. Utasikia mala ikisema “Mtu haruhusiwi kujichukulia sheria mkononi” na ndipo kikundi Fulani kitaibuaka na kuvunja mabucha na kuchoma nyama iliyomo humo hapo tena utasikia serikali hiyohiyo ikitowa kauli kwamba “Mvumiliane” je tunakwenda wapi?

Kwa misingi hiyo kwanini tusite kusema kwamba serikali ya chama cha mapinduzi (CCM) inaibeba dini ya kiislamu? Kwakuwa jukumu la serikali ya chama cha mapinduzi ni kuhakikisha kuwa wananchi wote wa Tanzania bila kujali dini zao, makabila yao na hata rangi zao wanaishi katika misingi ya uhuru, haki, udugu na amani kama raisin a watendaji wake walivyotoa kiapo mara baada ya kupewa dhamana ya kuiongoza nchi na wananchi wake kwa ujumla pasipo na ubaguzi wowote.

HITIMISHO: Ili wakristo wote nchini warudishe imani yao kwa serikali ya chama cha mapinduzi mambo ya fuatayo ni lazima yachukuliwe hatua za haraka iwezekanavyo:

Tunataka Serikali izingatie utawala washeria kulingana na ahadi yake katika kushughulikia maswala ya kijamii na sio vinginevyo. Kwa kuzingatia sheria maswala ya imani na dini yapo wazi kabisa kama zilivyoanishwa kwenye katiba ibara ya 19 (1), (2) (3) (4) na kufanya vinginevyo ni uvunjifu wa sheria.

Swala la kuua lisichukuliwe kama mazoea ya kawaida na inapotokea popote ni lazima Serikali ichukuwe hatua inayostahiki kwa kuzingatia utawala wa sheria kwakuwa wote wako sawa mbele ya sheria ibara ya 12, 13 (1) –(5).Usawa huo ni lazima uonekane katika swala la mauaji ya Mchungaji Mathayo Kachila na kama hatua zilivyochukuliwa katika mauaji ya aliyekuwa mwenyekiti wa halmashauri na mwenyekiti ya CCM Wilaya ya Rungwe Ndg. John A. Mwankenja. Hiyo ni haki ya msingi kkwa kila mtantania bila kuangali haiba (Personality) yake kama katiba ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania inavyoainisha haki xza kuishi, kulindwa na kushughuklikiwa kisheria katika ibara ya 14 na 15 pamoja na vifungu vyake viwili vidogo.

Tunataka Serikali itueleze ni ushahidi gain zaidi inayoutaka kuliko ule unaopatikana kwenye CD na DVD zilizotolewa na Sheikh Ilunga kama inazingatia utawala utawala wa sheria.

Tunataka Serikali iwajibike kutolea ufafanuzi kauli ya waziri wan chi Ndg. Steven Wasira inayohusu haki ya kuchicha kwa waislamu kama inatokana na sheria gain ya nchi?

Kama Serikali inatekeleza utawala wa sheria, tunataka wakristo tuwe na machinjio na bucha zetu kulingana na imani yetu.

Kama Serikali haitachukuwa hatua za makusudi katika kutekeleza madai yetu sisi kama viongovi wa dini ya kikristo tutachukua hatua ya kuwaambia waumini wetu kwamba Serikali ya chama cha mapinduzi inaibeba dini ya kiislamu na wao watajua la kufanya.

Pamoja na kutaka utekelezaji wa haraka kutoka kwa Serikali bado tunawaomba wakristo tuwe katika hali ya maombi na utulivu kwa wakati huu ambapo tumo katika vita vya kiroho ili Mungu akatuimarishie amani ambayo ni nguzo kuu ya Taifa letu. Tamko hili rasmi la jukwaa la wakristo Mbeya lisomwe katika makanisa yetu yote siku ya juma pili tarehe 24/02/2013.

Tunakuambatanishia na nakala ya Tamko Rasmi la TCF Taifa la tarehe 6/12/2012.

NDUGU MKUU WA MKOA NAWASILISHA.

Nakala kwa:

Mwenyekiti wa CCM Mkoa.
Tanzania Christian Furum Taifa
Mwenyekiti wa the Tanganyika Law Society.
Vyombo vya habari TV, Redio na magazeti

8 Comments
  • Nasikitika sana, ninapo ona mbio za kuikimbia amani zinaongezeka!!!!!Ndugu zangu waislam, tulisingizia muungano tukachoma kanisa, tukadai hak ya kuchinja mnyama tukamchinja mchungaj,leo hii tunadai kuonewa tumemuua padre!!!!Hv ndivyo Allah anavyotaka tuish?…..Jiulize kingetokea nn iwapo angeuwawa Sheikh? Ikiwa mtoto alipokojolea Quran yalitokea yale? mungu ilaze roho ya Marehemu Padre.Evarist Mushi…Amina…..MUNGU IBARIKI TANZANIA,MUNGU IBARIKI AFRIKA 

  • Ndugu  zangu, ni mawazo gundi ambayo  yakishika  yameshika,kuna  lipi  linaweza  likawa  suluhu  kati  ya  kumwua  mtu  ili  kuimalisha  imani  yako  na  hivyo  kuwashawishi  watu  wangine  waingie  kwenye  imani  yako  kwa  kuua? Tuache  hizo  bali  tueleweshane ili  tuwe  na  mfumo  mzuri  wa  kuishi  nyumba  moja  dini  tofauti.

  • Ndg zangu wakristo,tusiwe BIASE kiasi hicho.mbona mnataka kuumba vitu viso vya kweli na kujitwsha jukum la vyombo vya usalama? hivi nani kathibitisha kuwa huyo padri MUSHI kauawa na waislam?Jaman mbona kana kwamba mlikuwa mmesubiri hili?Sisi tulioko buselesele tunawashangaa sana wakristo na vyombo vyao vvya habari kusema kuwa huyo mchungaji kauwawa kwa kuchinjwa na kisha kutenganishwa kichwa,jamani mbona huu ni uongo?kwan huyo mzee alifariki akipelekwa hospitali na majeruhi wengine.Embu tusubir Vyombo vya usalam vituletee wahusika.

     

    • hongera kwa kutokwenda na wakati ndugu yangu, unatakiwa kujua ni nini kinachoendelea kwa wakati ulioao!!!

       

  • Du! jamani sasa na sisi wakristo tumechoka kuonewa, kudhalilishwa. Dini ni amani na si kuua.

    TUAMKENI WAKRISTO WA TANZANIA!

  • mwisho wa ubaya kuona haya hao wanaofanya ivyo kwa kisingizio cha dini mungu atakuja kuwaumbua na ikibidi tutawashughulikia waache kutuchezea na sis ni watu cio miti

  • hao wanaofanya ivyo kunasiku kitageuka na tutawashughulikia wasidhan sis ni miti sis ni watu tena tunauelewa mzuri dawa yao ipo

  • Ndugu zangu inasikitisha kuona kiongozi wa dini anaagiza waumini kuua waumini wa imani nyingine.UWEPO WA MUNGU HAPO WATIA MASHAKA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *