Mawaziri walioteuliwa: waapishwa, kuifikisha nchi kwenye uchumi wa viwanda

Jamii Africa

Muda mfupi baada ya kuapishwa katika nyadhifa zao, mawaziri wapya walioteuliwa na Rais John Magufuli waahidi kuwatumikia wananchi kuifikisha nchi kwenye uchumi wa viwanda.

Mawaziri hao wameapisha leo Ikulu jijini Dar es salaam baada ya mabadiliko yaliyofanywa na Rais mwishoni mwa wiki, ambapo  Baraza la Mawaziri litakuwa na wizara 21 na kuongozwa na Mawaziri 19 na Manaibu Mawaziri 21 kutoka 16 waliokuwepo awali  ili kuongeza ufanisi katika utendaji wa serikali ambapo baadhi ya wizara zimegawanywa.

Kwa upande wake Waziri mpya wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. George Mkuchika ameapa kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa katika ofisi za umma nchini na kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wananchi .

“ Kwanza elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya rushwa, nitatumia muda wangu mwingi na ndugu zangu wa TAKUKURU kuhakikisha tunatoa elimu ya kutosha  kwa wananchi kuhusu masuala ya rushwa. Somo linalohusiana na masuala la rushwa lifundishwe kuanzia chekechekea, shule za msingi mpaka chuo kikuu kwasababu watu wengi katika nchi hii wanatoa rushwa kwasababu ya kutokujua” amesema Kapt. Mkuchika.

Pia amesema atapambana na watumishi wazembe ambao wanatumia muda wa kazi kufanya mambo yao binafsi na kuwakosesha wananchi huduma muhimu.  Anasema atarudisha nidhamu mahali pa kazi na kuwaonya wafanyakazi ambao wanapata mshahara lakini hawafanyi kazi kama inavyotakiwa.

“katika kipindi changu nikiwa waziri ujumbe wangu ni huu kwamba wananchi wanapofuata huduma maofisini wawakute watumishi wa kazi wakiwa ofisini. Mara nyingi mtu anaripoti ofisini baada ya muda mfupi anaondoka anasema anakwenda kunywa chai, wananchi  wanatoka vijini wanakaa wanamsubiri mtumishi  ati amekwenda kunywa chai” amesema na kuongeza kuwa,

“ Jambo hili kuanzia leo nitalisimamia na kuhakikisha kwamba watumishi wa umma wanashinda kazini kwao ili kila mtumishi wa umma alipwe kwa kufanya kazi muda wote”.

Kabla ya kuwa waziri, Kapt. Mkuchika alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na amechukua nafasi ya Angela Kairuki ambaye amekuwa Waziri wa Madini.

                                        Waziri wa Madini Angellah Kairuki akila kiapo cha utii mbele ya rais wa                                              Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli  leo  ikulu jijini Dar es salaam

Naye Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesema uteuzi huo unamfanya atafakari sana kwasababu amekabidhiwa wizara yenye changamoto nyingi ambazo kama waziri atahakikisha anaziondoa na kuisaidia nchi kunufaika na mazao ya mifugo na uvuvi.

Kabla ya kuwa waziri, Mpina alikuwa Naibu Waziri wa Muungano na  Mazingira na nafasi yake imechukuliwa na Kangi Lugola.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) amewataka watendaji wa serikali kufanya kazi kwa bidii na kuendana na kasi ya Rais Magufuli ili kuwaletea wananchi maendeleo yaliyokusudiwa.

“Wategemea utendaji mzuri wa kazi, na niwaombe watumishi wote Tanzania lazima wajipange kufanya kazi kwa kasi (speed), tunategemea utendaji wa kazi ubadilike lengo tuisukume nchi yetu kwenye malengo tunayotarajia”.

Waziri Jafo ni miongoni mwa mawaziri watano ambao wamepandishwa vyeo na kuwa mawaziri kamili na anasema uteuzi wake umetokana na imani ya Rais aliyonayo juu yake, utendaji mzuri wa kazi na dhamana aliyonayo kuwatumikia wananchi.

Naibu Waziri mpya wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Abdallah Bulega amesema anamshukuru Rais Magufuli kwa kumpatia nafasi hiyo na anaahidi kutumia maarifa na uwezo wake kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika wizara hiyo.

Pia amesema atashirikiana na mawaziri wengine kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji na kuhakikisha ardhi iliyopimwa inagawanywa vizuri ili kila mtu atumie ardhi hiyo kama ilivyopangwa na serikali.


“Kama wote tunavyoelewa nimepewa imani na Mheshimiwa Rais lazima nithibitishe ile imani kwa kuiweka katika matendo na kuhakikisha watanzania wote katika nchi hii tuwakabidhi kile ambacho ni mategemeo ya Rais, ili tuweze kuzalisha kile watanzania wanachokimudu” – Naibu Waziri wa Kilimo, Mary Mwanjelwa.


Naye Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya ambaye hapo awali alikuwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, amefurahishwa na uteuzi huo wa rais na amewataka watanzania wategemee utendaji uliotukuka ili kuipeleka nchi katika uchumi wa kati.

Pia ameeleza kufufua uchumi na kutengeneza mazingira ya kufanya biashara ili kuongeza uzalishaji na kujenga uchumi wa viwanda.

Mawaziri waliojiuzuru

Mabadiliko katika baraza la mawaziri yamekuja wakati kukiwa na mjadala miongoni mwa wananchi kuhusu kasi ya utendaji ya rais Magufuli ambayo imeonekana kuwashinda baadhi ya watendaji ambao kwa nyakati tofauti walikaa pembeni na kumruhusu rais kuteua watu wengine.

Kabla ya uteuzi huo wa mawaziri wapya na wengine kupandishwa vyeo na kubadilishiwa wizara, mawaziri watatu waliondoka katika nyadhifa zao akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga ambaye alijiudhuru kwa kashfa ya kukutwa akiwa amelewa katika viwanja vya bunge.

Mwingine ni Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye ambaye aliondolewa na rais katika wadhifa wake siku moja baada ya kutoa ripoti ya kuvamiwa kwa kituo cha utangazaji cha Clouds.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene aliamua kujiudhuru baada ya kutajwa katika ripoti ya uchunguzi ya utoroshaji wa madini ya Tanzanite na Almasi ambapo nchi ilikuwa inapoteza fedha nyingi kutokana na viongozi wa serikali kushindwa kusimamia rasilimali za nchi.

Rais afanya mabadiliko katika Baraza la Mabadiliko

Rais amefanya mabadiliko pia katika wizara mbili ambapo wizara hizo zimegawanywa, jambo lililofanya wizara kuongezeka kufikia 21 kutoka 19 zilizokuwapo.

Wizara zilizogawnywa ni Wizara ya Nishati na Madini ambayo imekuwa wizara mbili zinazojitegemea, Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini pamoja na Wizara Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambayo imegawanywa kuwa Wizara ya Kilimo, na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Hapa chini ni orodha ya Mawaziri, Manaibu Waziri wapya walioteuliwa. Baadhi yao ni wapya katika baraza, huku wengine wakipandishwa kutoka manaibu kuwa mawaziri, na wachache wakihamishwa wizara.

  1. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora- George Huruma Mkuchika (Mpya)
  2. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)-Selemani Said Jafo (Amepandishwa kuwa Waziri)
  3. Naibu Waziri wa Wizara Muungano na Mazingira- Kangi Alphaxard Lugola (Mpya)
  4. Naibu Waziri wa Walemavu (Wizara ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu) – Stella Ikupa (Mpya)
  5. Waziri wa Kilimo – John Tizeba (Alikuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi)
  6. Naibu Waziri wa Kilimo- Mary Chuki Mwanjelwa (Mpya)
  7. Waziri wa Mifugo na Uvuvi- Luhaga Mpina (Alikuwa Naibu Waziri Mazingira na Muungano)
  8. Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi- Abdallah Ulega (Mpya)
  9. Naibu Waziri katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano- Elias John Kwandikwa (Mpya)
  10. Waziri wa Nishati- Merdadi Kalemani (Alikuwa Naibu Waziri Nishati na Madini)
  11. Naibu Waziri wa Nishati-  Subira Khamis Mgalu (Mpya)
  12. Waziri wa Maliasili na Utalii- Khamis Kigwangalla (Alikuwa Naibu Waziri Wizara ya Afya)
  13. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii- Japhet Ngailonga Hasunga (Mpya)
  14. Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji- Mhandisi Stella Manyanya (Alikuwa Naibu Waziri Elimu)
  15. Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia akitokea Wizara ya Mifugo- William Ole Nasha (Alikuwa Naibu Waziri Kilimo Mifugo na Uvuvi)
  16. Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo- Juliana Daniel Shonza (Mpya)

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *