Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiForums, Maxence Melo amesema licha ya kuwepo kwa sheria zinazoonekana kuminya uhuru wa mitandao ya kijamii, bado vijana wana nafasi kubwa ya kufaidika na fursa mbalimbali zilizopo kwenye teknolojia hiyo inayokuwa kwa kasi duniani.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika semina iliyofanyika Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) jijini Dar es Salaam, Melo alisema kuna fursa nyingi ambazo zikitumika vizuri zinaweza kubadilisha maisha ya vijana ambao wanatumia mitandao ya kijamii kwasababu Tanzania iko kwenye ramani ya dunia.
“Fursa ni kwamba mitandao imetufungua sana kwa kiwango ambacho Tanzania imeiingia kwenye ramani. Kuna vitu vingi vinatokea ambavyo tunaweza kuvifanya ni innovation (uvumbuzi). Lazima tutengeneze innovation ambazo zinaweza kutusaidia.” amesema Melo.
Amesema fursa ya kwanza ni ya miamala ya fedha inayofanyika kwa njia ya mtandao ambayo inawezeshwa na intaneti ambapo kijana anaweza kupata fedha popote alipo kwaajili ya shughuli zake za kijamii au kiuchumi na kuokoa muda wa kwenda benki au kwenye mashine za kutolea fedha (ATM Machine).
“Miamala mnayoifanya kwa M-pesa isingewezekana bila kuwa na mtandao wa intaneti. Inaweza kufanyika lakini ingeweza kufanya kama inavyofanyika bila mtandao wa intaneti. Intaneti ikikata kabisa hapa nchini, mabenki hayatafanya kazi kwa ufanisi kama ambavyo yanafanya kwa sasa,” amesema Melo.
Amebainisha kuwa fursa nyingine ujio wa sarafu ya digitali (Cryptocurrency) inayowawezesha vijana kufanya biashara ya mtandao ikiwemo kuweka dhamana, kununua hisa. Cryptocurrency ni sarafu iliyojificha ambayo huwezi kuiona kwa macho lakini unaweza kuitumia kwa matumizi ya kila siku.
“Hata kwenye mitandao mnaona kuna kitu kinakuja kinaitwa “Cryptocurrency” ni fursa. Fursa zinaweza kuwa zimegawanyika; fursa ya kupigwa au fursa ya kufanya kihalali kwasababu hata humo katikati wameingia wapigaji. Tumejaribu kuangalia wale wanaosema kwenye “cryptocurrency” na uhalisia wake na jinsi ya kwenda mbele.” Amefafanua Melo.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Kingdom Heritage, Tunu Bashemela akizungumza wakati wa semina hiyo iliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, amewataka vijana kuwa makini na biashara za mtandaoni ili kuepuka matapeli ambao wanatumia teknolojia ya mitandao vibaya, “Ni vema mnapokuwa mnafanya hayo mambo mkajua kabisa kupigwa ni rahisi.”
Ameongeza kuwa mitandao inaweza kuwa njia nzuri ya kuimarisha Demokrasia ya vyama vingi ambapo wananchi wanapewa uhuru wa kuchagua kiongozi wanayemtaka kwa kutumia teknolojia rahisi ambayo itaepusha vurugu za kisiasa na kuongeza ajira kwa vijana.
“Kwa ambao mnafuatilia nchi moja ya kiafrika imetumia ‘Cryptography’ (maandiko ya mficho) kwaajili ya uchaguzi. Inasaidia kuepusha haya mambo ya kusema kwamba si tumeibia kura, kwahiyo kwa yeyote atakayetengeneza teknolojia hiyo ataisaidia Tume ya Uchaguzi, vyama vya siasa kusimamia uchaguzi. Kila kitu kiko wazi aliyeshinda kashinda kihalali. ‘Cryptography’ ndio mustakabali wa kizazi hichi tulichonacho.” Amesema Melo.
Lakini amesema ujio wa Sheria ya Maudhui ya Mtandaoni ya mwaka 2015 na Kanuni zake za mwaka 2018 zimeminya utendaji wa mitandao hasa kwa vijana wanaoendesha majukwaa, blogu hata redio na runinga za mtandaoni kwasababu sio sehemu salama kwa wafanyabiashara na makampuni kutangaza bidhaa au huduma zao.
“Sheria na kanuni zinazotengenezwa na mamlaka hapa niwaambie ukweli eneo hilo sio salama tena. Ninaweza kukuambia wekeza lakini halilipi. Tangu kuingia kwa kanuni za maudhui mtandaoni makampuni yameondoa matangazo”, amesema Melo.
Washiriki wa semina ya Usalama Mtandaoni wakimsikiliza mmoja wa wachangiaji
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Usalama Mtandaoni kutoka kampuni ya Kabolik, Robert Matafu amesema wakati vijana wanatumia fursa za mtandaoni ni muhimu pia wafikirie kujihakikishia usalama wao binafsi na miradi yao.
“Teknolojia ni njia inayokusaidia kurahisisha kazi. Ukitaka kuwa salama ni muhimu ukajenga mfumo thabiti utakaokulinda na hatari zote. Kwasababu kwenye mtandao kunapatikana kila taarifa hata jina lako, makampuni na mashirika ni muhimu kuwa nasera na miongozo “ amesema Matafu.
Amesema ili kujihakikishia usalama zaidi ni kuweka neno la siri (password) kwenye simu na kompyuta ili kutokuruhusu mtu yeyote asiyehusika kuingilia mawasiliano au shughuli zako.
Naye, Dkt. Philip Filikunjombe kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) amesema watumiaji wa mitandao ya kijamii wanatakiwa kuzisoma na kuzielewa sheria na kanuni za Makosa ya mtandao ili kuepuka kuingia kwenye matatizo yasiyo ya lazima.
Amebainisha kuwa vijana wakifahamu sharia itawasaidia kufahamu mambo halali na haramu kwenye mitandao na kuwasaidia kuendeleza miradi itakayowanufaisha kiuchumi na kijamii.
Awali akizungumza katika semina hiyo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Kingdom Heritage, Tunu Bashemela alisema wao kwa sehemu yao wanaunga mkono juhudi za serikali na wadau wa mitandao ya kijamii katika kutoa elimu kwa umma hasa vijana ili kuwahakikishia usalama wanapotumia teknolojia ya mtandao.
“Ili kujua matumizi sahihi na salama vijana mliopo hapa lazima mtambue kuwa sheria ya makosa ya uhalifu wa kimtandao ipo na inafanya kazi lazima tuheshimu na kutii vitu inavyotuzuia kufanya bali tutumie mitandao kwa namna za ubunifu zenye kutuletea fedha na kujiingizia kipato,” alisema Bashemela.
Kampuni ya Kingdom Heritage ni mdau muhimu katika kukuza teknolojia nchini, imekuwa ikiandaa semina na mafunzo mbalimbali yanayolenga kukuza uelewa na ujuzi wa teknolojia ya mawasiliano kwa jamii ya vijana.