Maxence: Rais Magufuli anafanya vyema katika Mapambano dhidi ya Ufisadi lakini tunahitaji Taasisi imara

Jamii Africa

Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiForums, Maxence Melo akihojiwa na vyombo vya Reuters na Sauti ya Amerika(VoA) amesema Serikali ya Rais Magufuli imeonesha dhamira ya kisiasa ya kupambana na vitendo vya ufisadi na rushwa vilivyokuwa vimekithiri nchini lakini akataadharisha bila taasisi imara vita hii inaweza kukwama.

Maxence ameyasema hayo jana katika mahojiano ambayo FikraPevu pia ilikuwepo baada ya kumalizika kwa mdahalo wa kwanza wa Demokrasia Yetu ulioandaliwa na Asasi ya Kiraia ya Twaweza.

Amesema rushwa na ufisadi viliichafua nchi na ilifika wakati hadi watanzania wakaaminishwa kuwa kuna watu hawagusiki lakini tangu Rais Magufuli na Serikali yake waingie madarakani hali imekuwa tofauti kitu ambacho kimepelekea hata tafiti za Twaweza kuonesha kuwa wananchi wanaona kinachotokea kuwa kitu kizuri na cha kupongezwa.

Katika mahojiano hayo, mwandishi alitaka kujua hali ya vitendo vya kifisadi na rushwa nchini na hatma ya uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari chini ya Serikali ya awamu ya tano.

Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiForums, Maxence Melo (Katikati) akiwa na Mwakilishi wa Mtandao wa Kutete Haki za Binadamu, Deogratius Bwire (kushoto) na Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Valerie Msoka (Kulia) kwenye Kongamano la Demokrasia Yetu lililoandaliwa na Taasisi ya Twaweza, jijini Dar es Salaam jana.

 

Hali ya Rushwa na Vitendo vya Kifisadi

Maxence alipongeza jitihada zinazooneshwa na serikali ya awamu ya tano lakini akasisitiza bila taasisi imara vita hii itakwama na kuonekana kama ilikuwa gia ya kisiasa tu.

Alitolea mfano ziara za Rais John Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa bandarini na jinsi ambavyo  wamekuwa wakibaini michezo michafu na kutoa onyo kwa watendaji lakini michezo hiyo imekuwa ikijirudia hata baada ya hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wahusika.

“Fikiria, Waziri Mkuu ameenda pale bandarini mara kwa mara na kila ziara yake ya kushtukiza amekumbana na madudu. Rais pia amefika pale na kubaini michezo ile inaendelea. Imefika wakati hadi Rais analazimika kutoa karipio la wazi mbele ya vyombo vya habari kwa IGP kwa kushindwa kufanya kazi yake vema ingawa alimwamini sana wakati anamteua” alisema Maxence.

Maxence aliongeza kuwa Ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2013 aliyoitaja kama “Opening the Gates: How the port of Dar es Salaam can transform Tanzania” ilionesha kuwa Bandari ya Dar es Salaam ikisimamiwa vyema na kupanuliwa inaweza kuendesha uchumi wa nchi kwani pia ni tegemeo kubwa kwa mataifa jirani ya Malawi, Zambia, Burundi, Rwanda, Uganda na mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Alibainisha kuwa Taasisi kadhaa za Serikali zinahitaji kujengewa uwezo na watendaji wanaowekwa kufanyiwa “vetting” ili wawe na dhamira ya kweli ya utendaji na sio wale wanaoamini kupata nafasi hizo ni kupata ulaji.

Amezitaja baadhi ya taasisi kama TAKUKURU, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP), Jeshi la Polisi na Mahakama kuwa zikiweza kuendana na kasi ya Rais Magufuli basi Tanzania njema itawezekana.

Ameonyesha kuwa na mashaka na wale waliokamatwa wakituhumiwa na makosa mbalimbali yakiwemo ya utakatishaji fedha na waliohusishwa na sakata la Tegeta Escrow huenda wakaishia kufutiwa mashtaka kama upande wa mashtaka usipoandaliwa vyema na mwisho wa siku wananchi wakaamini wamepigwa ‘changa la macho’.

 

Uhuru wa Vyombo vya Habari na Uhuru wa Maoni nchini

Kuhusu Uhuru wa Vyombo vya Habari na Uhuru wa Maoni, alisema Serikali ya Awamu ya Tano haifanyi vyema na jitihada za wazi zinahitajika kuboresha upande huu.

Pia alionesha kutoridhishwa na kufungiwa kwa magazeti kadhaa kwa kauli ya Waziri tu na uvamizi uliofanywa kwenye kituo cha runinga cha Clouds Media.

Alisema takwimu za Twaweza zimebainisha mwaka 2015 pekee watu 358 walikamatwa kwa kutoa lugha mbaya na mwaka uliofuatia, 2016 watu 911 walikamatwa kwa kosa hilohilo. Akasisitiza, Serikali iwe tayari kusikiliza hata wanaoongea yale ambayo haikutaka kuyasikia.

Hata hivyo, Maxence alisema Rais Magufuli na Serikali yake wanavihitaji Vyombo vya Habari na Asasi za Kiraia katika kuwezesha mapambano dhidi ya Ufisadi hivyo ni vyema kutoa nafasi kwa wadau hawa kushiriki kikamilifu katika kulisukuma gurudumu la maendeleo ya Tanzania.

“Hadi sasa tunapambana na ufisadi wa awamu zilizopita, uhuru wa kuongea na Bunge huru vimesaidia haya kuibuliwa awamu zilizopita, awamu hii ikitoa uhuru wa kutosha basi Rais hata kabla hajarudi bandarini Dar es Salaam vyombo vya habari vitakuwa vimeshaibua mengine makubwa ambayo yatachangia juhudi za kupambana na ufisadi.” alisema Maxence.

Kongamano la Demokrasia Yetu limefanyika kwa mara ya kwanza likiwa limeandaliwa na Taasisi ya Twaweza na Mkurugenzi wa Taasisi hiyo ametabainisha kuwa watajitahidi kuandaa kongamano la pili ndani ya miezi 6 hadi 9 ijayo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *