katika kuelekea siku ya Wazee Duniani, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Mwita Waitara amewataka wazee wa kata katika jimbo hilo kujitokeza katika zoezi la kujiandikisha ili wapate vitambulisho vitakavyowasaidia kupata huduma za matibabu bure katika vituo vya afya.
Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu kuzindua ugawaji wa vitambulisho vya awali 7296 vya matibabu bure kwa Wazee katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es salaam, ambapo alizitaka Halmashauri zote nchini kuiga mfano huo na kuhakikisha zinaandaa mipango ya kuwahudumia wazee wasiojiweza kwa kuwapatia bima ya afya.
Alisema kuwa Wazee ni asilimia 5.6 ya wananchi wote wa Tanzania idadi ambayo kwa kiasi kikubwa inaleta msukumo kwa nchi kuweka mifumo madhubuti ya kuhudumia Wazee ikiwemo kurahisisha upatikanaji wa Huduma katika matibabu.
Taarifa ya zoezi la kuandikisha wazee imetolewa na Ofisi ya Mbunge wa Ukonga baada ya Mbunge Waitara kufanya ziara katika kata 13 za jimbo hilo akihamasisha jamii kuwajali na kuwathamini wazee na kuhakikisha wanapata huduma za afya bila vikwazo.
“ Ni muda muafaka kuwasaidia wazee kwasababu nao walikuwa vijana, hivyo kwakuwa umri wao umeingia katika uzee lazima hatua zichukuliwe kuwasaidia hususani katika suala la matibabu ambayo kimsingi ni ghali sana, hivyo wazee hao hawana uwezo wa kumudu kwa kuwa wengi wao hawana uwezo tena wakujishughulisha” inasema taarifa hiyo.
Amewataka watendaji wa jimbo hilo kuachana na itikadi za vyama na ubaguzi na waweke maslahi ya wazee mbele ili kuwahakikishia usalama wa afya zao.
Baada ya kujiandikisha taarifa ya kupata vitambulisho hivyo itatolewa katika viwanja vya Mnazi Mmoja ambako sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani kwa mkoa wa Dar es salaam zitafanyika.
Kwa upande wake, Mzee Elisha Mwamkinga kutoka shirika la The Good Samaritan Social Services Tanzania (GSSST) ambaye amekuwa akipigania haki za wazee anasema, “Sisi wazee ni binadamu kama binadamu wengine tuna haki ya kuheshimiwa na kupata huduma za afya”
Anasema wanapata usumbufu katika baadhi ya hospitali na kutakiwa kulipia matibabu na wahudumu huwanyanyasa. Kutokana na changamoto hizo anataka uandaliwe utaratibu wa kupata vocha maalumu zitakazogharamia huduma zote za afya.
“Wazee tunadharaulika, hatuthaminiwi na hatupati huduma bora za afya kwasababu hatuna kipato. Tunaiomba serikali itupatie vocha maalum ili tupate huduma za afya kwa wakati” anasema mzee Mwamkinga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkaazi wa shirika la HelpAge International, Smart Daniel anasema licha ya wazee kutopata huduma za afya bado wanakabiliwa na changamoto za usalama, kipato duni na mauaji ya kishirikina.
“Kuna watu wanatoa huduma za afya lakini hawaelewi changamoto za wazee, tumekuwa na tatizo katika jamii yetu kuhukumu wazee kuwa ni wachawi”.
Anaitaka jamii na serikali kuwajali wazee na kuwaandalia mazingira sahihi ya kisheria ya kupata huduma zote za kijamii, kipato na kuwahakikishia usalama wao.
Pia inaelezwa kuwa ni asilimia 4 tu ya wazee wote ndio wana bima ya afya nchini ambapo ni sawa na wananchi wasiozidi milioni moja nchini kote.
Kwa mujibu wa Sensa ya 2012, Tanzania ina wazee milioni 2,449,257 ambao ni sawa asilimia 5.6 ya watanzania wote. Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka ambapo katika kipindi cha miaka kumi ijayo Tanzania inatarajiwa kuwa na wazee milioni 16.
Siku ya Wazee Duniani hufanyika Oktoba 1 kila mwaka ambapo nchi mbalimbali hutathmini hatua zilizopigwa katika kuboresha maslahi ya wazee na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zilizopo.
Mwaka huu maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani, kitaifa yatafanyika Dodoma ambapo Rais John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.