Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Geita, Upendo Peneza amesema anakusudia kuzuia uchaguzi mdogo wa marudio katika majimbo ambayo wabunge wake wamejiuzuru na kujiunga na vyama vingine ili kuokoa fedha za wananchi.
Kauli ya Mbunge huyo kijana wa kuteuliwa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imekuja siku moja baada ya Mbunge wa Siha, Dkt. Godwin Mollel kujiuzuru nafasi yake na kuomba kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuibua mijadala miongoni mwa wananchi juu ya fedha zitakazotumika katika uchaguzi wa marudio utakaofanyika.
Ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam mbele ya Waandishi wa Habari ambapo amesema fedha ambazo zinaenda kutumika katika uchaguzi wa marudio zingeelekezwa kwenye shughuli za maendeleo na anakusudia kutumia vifungu vya katiba kuweka pingamizi la uchaguzi huo ili usifanyike mpaka utata wa kuhama kwa wabunge hao utakapotatuliwa.
“Nilikuwa napitia katiba ya nchi kuona kama kuna kipengele ambacho naweza kutumia kwenda mahakamani ili walau katika haya maeneo tusifanye uchaguzi kwanza ili uchunguzi ufanyike tuone kweli sababu za wao kuacha katika hayo maeneo”,
“Lakini kama mtu anataka kugombea kwa chama kingine alikuwa mwakilishi wa pale basi hawa watu wasiruhusiwe kugombea kwa maana ya hiki kipindi kwasababu wamevuruga nafasi zao na wananchi ndiyo tunaingia gharama ambayo ingesaidia katika kujenga vituo vya afya”, amesema Mbunge huyo.
Ameongeza kuwa hamahama ya wabunge na madiwani inawaweka wananchi katika joto la kisiasa na kuwatoa katika jitihada za kujiletea maendeleo.
“Tuna wabunge watatu ambao wameondoka ndani ya vyao, suala hili ni kwamba taifa na wananchi tunaingizwa katika ‘pressure’ ya uchaguzi kabla ya muda. Watanzania wanahitaji maendeleo”, amesema Mbunge huyo na kuongeza,
“Watanzania tuchague tunataka nini? Kama kweli tunahitaji kuonyesha tunakubalika wananchi kiasi gani wamekwisha pokea maendeleo mpaka sasa hivi. Pesa ambayo tunakwenda kuitumia kwenye uchaguzi ingejenga hospitali kuepukana vifo vya mama na watoto”.
Wimbi la kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine lilishika kasi baada ya Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM) Lazaro Nyalandu kuhamia CHADEMA, ambapo siku chache baadaye wabunge wawili, Abdallah Mtulya (CUF) wa Kinondoni na Godwin Mollel (CHADEMA) jimbo la Siha kujiuzuru nyadhifa zao na kuingia CCM.
Ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi, Tume ya Uchaguzi (NEC), imetangaza uchaguzi mdogo wa marudio katika majimbo ya Singida Kaskazini, Songea Mjini na Longido ambao utafanyika Januari 13, 2018. Inaelezwa kuwa kuna uwezekano wa kuongeza majimbo ya Siha na Kinondoni ambayo yako wazi kutokana na wabunge kujiuzuru nafasi zao.
Upendo Peneza amebainisha kuwa hana mpango wa kuondoka CHADEMA kwasababu anawajibika kwa wananchi anaowatumikia na kitendo cha kuhama kwa wabunge hakubaliani nacho.
“Mimi sijashawishika, nilivyogombea mwaka 2015 nilikuwa na akili zangu timamu na niligombea CHADEMA na nilijua CCM ipo, namuomba Mungu anisaidie muda wangu wa ubunge nimalize salama na nitoe utumishi uliotukuka”, amesema.
Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Upendo Peneza akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam
Upendo Peneza anakuwa Mbunge wa pili kukanusha tuhuma za kuhamia CCM baada ya Mbunge wa Ubungo, Said Kubenea kufanya hivyo kutokana na taarifa zilizokuwa zinasambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai wabunge wengine wa upinzania watahama vyao.
Hata hivyo, Mbunge huyo amekiri kuwa ndani ya vyama vya siasa kuna migogoro lakini isiwe sababu ya kuchukua maamuzi ya kuhama, “Ninaelewa ndani ya vyama vya siasa kuna changamoto zake, lakini pale ambapo watanzania wameingia gharama kwa sababu yako, tusidie baada ya miaka mitano, ikiisha achana nao bila gharama”.
Gharama za uchaguzi
Wananchi wa kada mbalimbali wamekuwa wakitoa maoni yao kutokana na wimbi la wabunge na madiwani kujiuzuru nafasi zao na kuhamia vyama vingine. Wamekiri kuwa ni haki yao kikatiba lakini wanapaswa kuhesabu gharama zinazoenda kwenye uchaguzi ikizingatiwa kuwa walichaguliwa ili wakawajibike kwa wananchi.
Kelvin Stanley ameandika kwenye ukurasa wa Twitter, “Na hii ndo Tanzania kwa hiyo ukiwa upinzani unajenga nchi tofauti why usimuunge mkono rais hata ukiwa upinzani. Hizi gharama serikali haioni wao wanachoona ni kuvimba tu kichwa”.
Naye Zero Unit wa Mtandao wa JamiiForums ameandika “mtu huwezi kutumikia taifa lako tu popote ulipo kwa nafasi uliopewa na wananchi. Mpaka mtukatishe tamaa sisi wengine ambao mapenzi yetu makubwa na matumaini yetu yapo upinzani. Hivi mnapotangaza kwamba mnahamia CCM kwasababu serikali yake inafanya kazi nzuri mnatufundisha nini sisi wengine?”
Kwa upande wake, Erick Kalemela anaandika katika ukurasa wa JamiiForums, “Kumekua na hali ya Sitofahamu ndani ya Chadema ikiwemo kutokuaminiana baada ya kujiuzulu kwa Dr. Godwin Moleli aliyekua Mbunge wa Siha haijulikani nani atafuata, Dr.Mollel amerejea kwenye Chama chake cha Zamani alikuja kwa Mafuriko ya Lowasa muda huo huo akaaminiwa na kuteuliwa kuwa mgombea kisha akashinda. Ipo haja ya kuwa na Utaratibu maalumu kwa watu wanaohama vyama vyao wakati wa Uchaguzi”.
Maria Sarungi Tsehai, Mwanzilishi wa taasisi ya ChangeTanzania ameandika, “Nilivyosema nilipotoka BMK kuwa mchakato wa katiba uliharibiwa na wanasiasa wengi hawakunielewa na walitetea upande mmoja walioonekana ni watetezi until 2015 ndiyo ikawa clear it’s all about power for politicians”.
Hata hivyo, mapendekezo ya wananchi yamekuwa kupatikana kwa katiba mpya ambayo itaondoa utata wa mstakabli wa kisiasa nchini na kujenga misingi ya demokrasia inayoheshimu matakwa ya wananchi.