Sitta atangaza nia kuwania urais ‘akiombwa’

Jamii Africa

HATIMAYE Waziri wa Ushirikiano wa nchi za Afrika Mashariki, Samuel Sitta ametoboa siri kuhusu nia yake ya kutaka kugombea Urais mwaka 2015, ambapo amesema sababu na nia ya kufanya hivyo anazo, kwa lengo jema la kuwatumikia Watanzania kwa maendeleo makubwa.

Amesema, anaamini uchapakazi wake ni silaha na sifa ambazo Watanzania watatoa maamuzi sahihi wakati ukifika, na kwamba kazi alizowafanyia wananchi na Taifa kwa ujumla tangu awe mteule wa Rais wa kwanza hayati mwalimu Julius Kambarage Nyerere hadi sasa, ni kielelezo tosha hivyo iwapo atapata fursa ya kuwa Rais hata kwa miaka mitano atawatumikia wananchi kwa maendeleo makubwa na baadaye kuwaachia vijana.

Waziri Sitta ameyasema hayo leo Jumamosi Machi 31, 2012 Jijini Mwanza, alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa habari hizi katika kikao chake na waandishi wa habari, kilichofanyika La Kairo Hoteli jijini hapa, ambapo aliwaomba wananchi wa Kata ya Kirumba kumchagua mgombea wa udiwani wa kata hiyo, Jackson Robert Masamaki (CCM).

Katika swali hilo, mwandishi wa habari hizi ilitaka kujua msimamo wa Waziri Sitta iwapo ana nia ya kutaka kugombea Urais mwaka 2015 ama la, pamoja na kauli tata juu ya ugonjwa unaomsumbua Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe.

Picha: Waziri Sitta akizungumza na waandishi wa habari leo La Kairo.
Picha: Waziri Sitta akizungumza na waandishi wa habari leo La Kairo.

“Huu ni wakati wa Watanzania kutafakari nani anafaa kuwa Rais wao. Lakini kwangu mimi, Watanzania wenyewe watapima na kuona jinsi ninavyoendesha mambo yangu kwa uwazi zaidi katika kuwatumikia. Nimekuwa mteule wa Rais tangu enzi za mwalimu Nyerere, Mwinyi, Mkapa na sasa mteule wa Rais Kikwete.

“Katika hili, Watanzania wenyewe ndiyo watakaoamua. Kama wataona ninafanana kugombea urais nitafanya hivyo, maana nimewahi kuwa Waziri wa Ujenzi, Katiba na Sheria, Spika wa Bunge na sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, lakini zote nimefanya kazi nzuri sana.

“Kwa mfano, nilipokuwa Spika niliendesha Bunge kwa uwazi bila kuogopa mtu. Kimsingi hii ndiyo rekodi yangu nzuri…hivyo nitagombea urais lakini kwa sasa acha kwanza watu wajitokeze halafu ije ibainike nani wananchi wanamtaka nani awe rais wao”, alisema Waziri Sitta huku akisisitiza kwamba kadri muda unaposogea suala la urais si la kutafuta, bali wananchi wenyewe ndiyo watakaomtaka.

Aidha, alifafanua kwamba yeye atawasikiliza zaidi wananchi wanavyotaka juu ya nafasi hiyo ya juu, na aliwaponda wanasiasa walioanza mapema kufukuzia nafasi hiyo ya kutaka kugombea urais.

Kwa mujibu wa Waziri Sitta, anaamini hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2014, mambo yatakuwa yamebainika, hivyo iwapo wananchi watamhitaji kugombea nafasi hiyo kulingana na uchapakazi wake mzuri na hodari hatasita kugombea nafasi hiyo, kwani malengo yake ni kuwatumikia Watanzania na taifa kwa maendeleo makubwa.

“Mwishoni mwa mwaka 2014 tutaona wale ambao watakuwa wanafanana kuwa rais wa nchi. Watafahamika tu maana wananchi ndiyo wenye mamlaka. Na mimi nitafuata matakwa ya wananchi wangu wa Tanzania, maana kazi nzuri na bora ninazozifanya matunda yake yanaonekana dhahiri”, alisisitiza Waziri Sitta.

Kuhusu ugonjwa wa Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, Waziri Sitta alisema anaheshimu sana kauli ya Dk. Mwakyembe aliyotaka suala hilo iachiwe Serikali yenyewe, na kusisitiza kwamba, upo wakati utafika mambo yote yatawekwa hadharani.

“Hili suala tulipe muda, tusubiri maana nadhani yapo mambo yatatokea. Lolote linaweza kutokea!. Ila nasheshimu sana kauli ya Dk. Mwakyembe mwenyewe anayotaka hili suala liachiwe Serikali ifanye kazi yake”, alisema Waziri huyo wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Waziri Sitta amewahi kunukuliwa na vyombo mbali mbali vya habari akidai kwamba ugonjwa unaomsumbua Naibu Waziri huyo wa Ujenzi unatokana na kulishwa kwake sumu.

Kufuatia kauli hiyo ya Waziri Sitta, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba aliibuka na kukanusha taarifa hizo za Sitta, akidai kwamba Dk. Mwakyembe hajalishwa sumu, kauli ambayo ilikuja baadaye kukanushwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – FikraPevu, Mwanza

5 Comments
  • Hata akigombea hana jipya. Tangu awamu ya kwanza yuko kwenye safu ya uongozi, lakini haonyeshi kama kuna kitu kimebaki alichoshindwa kukifanya kwa muda uliobaki. Kama ameshindwa kuona mchana kweupe atawezaje kuona USIKU? Kwani yeye paka? Apishe mbali huyo akalee wajukuu zake

  • hata akigombea hana mpya yeye mwenyew ni walewale hatutaraji kitu kipya toka kwake alivyojenga nyumba ya spika urambo alitaraji angedumu milele?akipata urais itakuwaje

  • Mzee Sitta kapumzike usije kuabika, huwezi kuwa Mwema kwa Watanzania, ilihali katika Jimbo lako ni utata.

    • kama sita atasimama basi Mwenyekiti  wao Tawi kule Afrika Kusini pia asimame maana ameonekana kukiponya Chama baada ya kutoboa siri nzito ndani ya Chama kuwa kuna CCM aina mbili,ya  KIJAMAA na ILE YA KIBEPARI ya AKINA LOWASA,na mwenzake JK na watoto wao mabilionea akina RIZIWANI KIKWETE mbona baada ya kumuuliza mwenyekiti wa CHama kuhusu kujivua GAMBA mpaka leo CHama kimekaa kimya,huyu ndiye anafaa kusimama kukitetea CHama ili wapinzani wasije kuchukua nchi vinginevyo CCM ya akina LOWASA amna kitu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *