Machali amfananisha Kafulila na gonjwa la ‘Kansa’

Jamii Africa

MBUNGE wa Jimbo la Kasulu Mjini kupitia NCCR-Mageuzi, Moses Machali ameibukia jijini Mwanza na kumsema Mbunge Kigoma Kusini kupitia chama hicho, David Kafulila, akisema kwamba chama kitamchukulia hatua kwa kuendelea kujitambulisha kuwa ni mwanachama wake.

Machali ametoa kauli hiyo alipokuwa akihutubia akihutubia mkutano wa hadhara wa wananchi katika uwanja wa Sahara jijini Mwanza, siku kadhaa baada ya viongozi wenzake wa NCCR-Mageuzi kupata aibu mkoani Kigoma, anakotoka mbunge huyo pamoja na Kafulila.

Kwa upande wake Kafulila amekataa kumjibu Machali kwa maelezo kwamba suala la kufukuzwa kwake uwanachama liko mikononi mwa mahakama na kwamba yeye anaendelea na shughuliza Kibunge ikiwamo kushiriki vikao vya kamati hadi hapo mahakama itakapoamua hatima yake.

“Mtu kama Machali hakuna sababu ya kubishana naye kwa kua ana matatizo yake binafsi ambayo yanamchanganya, lakini kama ni suala la nafasi yangu ya Ubunge, suala hilo liko mahakamani na mwanasiasa makini hawezi kulijadili kwa sasa,” alisema Kafulila Jumapili, Januari 14, akiwa Tabata, Dar es Salaam katika msiba wa Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Regia Mtema.

Katika mkutano huo wa hadhara, Machali alisema kamwe chama chake cha NCCR-Mageuzi hakitafumbia macho kumuona Kafulila akiendelea kutamba kwa kufanya mikutano ya hadhara na kujitangaza kwamba yeye bado ni mbunge na ni mwanachama.

“Ninamuonya Kafulila aache mara moja kufanya mikutano na kujitangaza kuwa ni mbunge halali na ni mwanachama wa NCCR-Mageuzi. Akiendelea kufanya hivyo tutamchukulia hatua za kisheria kwa kumkamata.

“NCCR-Mageuzi ilishamfukuza Kafulila uanachama. Hilo linafahamika na halina ubishi…kwa maana hiyo asiwe na kiburi na kuendelea kujinadi kwamba yeye ni mbunge”, alisema Machali.

Aidha, Machali alisema, Kafulila hafai kuwa mwanachama wa chama hicho kwa vile amekuwa mtomvu wa nidhamu, ikiwa ni pamoja na kutokuwa na dhamira nzuri kwa mstakabali na maendeleo ya chama chetu, na kwamba ni bingwa wa kuzungumza bila vitendo.

“Hatutaki viongozi ambao ni mabingwa wa kuongea bila vitendo. Kafulila hakuwa na dhamira nzuri kwa chama chetu na alikuwa tatizo ndani ya chama!. Na tunamfananisha na gonjwa hatari la kansa,” alisema.

Alisema suala la kutimua wanachama wa vyama vya siasa halikuanzia NCCR-Mageuzi, na kwamba hatua hizo zilishawahi kuchukuliwa hata na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho mwaka jana kiliwavua uanachama madiwani watano wa Mkoa wa Arusha.

“Chadema kiliwafukuza ndani ya chama waliokuwa madiwani wake watano, baada ya kuonekana kutaka kuleta ujinga.

“Ni bora wabaki wachache wanaochanja mbuga kupigania maendeleo na si kuwa na watu wasiokuwa na mwelekeo mzuri wa kuwasaidia wananchi wetu,” alisema Machali.

Akisisitiza zaidi, Machali alisema Tanzania itajengwa na siasa imara na uzalendo wa Watanzania wenyewe, vinginevyo maendeleo ya kweli hayatapatikana iwapo nchi itaendelea kuwa na wanasiasa wasiokuwa na dira thabiti.

Hata hivyo, alisema anakusudia kufanya ziara ya kuzunguka nchi nzima kuwashtaki kwa wananchi wabunge CCM, kwa kile alilichodai walipitisha muswada wa Sheria ya mabadiliko ya Katiba Mpya ya mwaka 2011 bila kujali mapungufu yaliyokuwamo ya muswada huo.

Hata hivyo, habari kutoka Kigoma zinaeleza kwamba Machali kwa sasa anasubiriwa na wananchi wa jimboni kwake kutoa maelezo kuhusiana na mgogoro uliopo kati ya NCCR-Mageuzi na Kafulila.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *