Mji mdogo wa Mererani unakabiliwa na tatizo la maji safi na salama ya kunywa na wakazi wake hununua ndoo kubwa ya lita ishirini kwa shilingi mia sita na ile ya lita kumi kwa shilingi mia nne.
Maji haya yanatoka eneo la Bomang’ombe wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro umbali wa zaidi ya kilometa 30 na kuletwa na magari na kuwafikia wauzaji katika vibanda vyao.
Hali hii ya ukosefu wa maji imeathiri wakazi wa eneo hili kwa kipato na afya zao na hasa wale wa kipato cha chini kwani ugonjwa wa typhod ama homa ya matumbo ni mwingi katika maeneo ya mji mdogo wa Mererani.
Afisa mtendaji wa mji mdogo wa Mererani Nelsoni Msangi amesema kutatua tatizo hilo la maji, Serikali ilichimba kisima na kutandaza mabomba ya maji kwa wananchi lakini iliwachukua miaka kumi toka kutandaza mabomba hayo hadi kuanza kutumika maji hayo.
Pamoja na kuwepo kwa maji hayo bado changamoto ya miundo mbinu kuwa imechakaa na tayari wameanza marekebisho ya mtandao wa maji na mabomba yanaendelea kubadilishwa.
“Aidha watu wengine wanatoboa mabomba na kuilazimu ofisi ya mji mdogo kujenga mbauti mbili kwa ajili ya kunyweshea wanyama katika kata ya Endiamtu na Songambele kwa kuwa walikuwa wanafanya hivyo ili wanyweshee mifugo yao, ameongeza Afisa Msangi.
Amesema hakuna uwiano wa kiwango cha maji na watu wa mji mdogo wa Mererani kwa sasa, pia kukatika katika kwa umeme mara kwa mara nalo ni tatizo jingine kwani unategemewa katika kupampu maji na kusababisha shida ya maji kwa wakazi hapa.
Dr. Emanuel Mushi wa kituo cha afya cha Endiamtu, alisema kama maji yakiwa hayatoki kituoni hapo,basi huchukua jukumu la kuchota na kujaza katika tanki lao la lita 2000.
“Natumia ambulance hii aina ya bajaji,natoa godoro anapotakiwa mgonjwa kulala,najaza ndoo za maji nasomba maji mpaka nione yanatosha sasa”alieleza Dr.Mushi.
Afisa Nelson Msangi tena amesema wanatarajia kununua matanki mawili ya lita 5000 na la zamani likiwepo na hivyo kufikia lita elfu 12 na zitakuwa zinatosha kwa mahitaji ya sasa katika kituo hicho.
Kwa mujibu wa wakazi wa mji mdogo wa Mererani,wamesema Kutokana na tatizo hili,akina mama wanaoeenda kujifungua hulazimika ndugu zao kubeba maji na kwenda nao kituoni hapo kama wakikuta hayapo.
Mji wa mererani una visima zaidi ya mia tatu kutoka kwa watu binafsi na baadhi yake maji sio mazuri kwa matumizi ya bindamu kwa kuwa eneo husika lina madini na hasa florine inayowabadilisha hata rangi ya meno.