Saa mbili kwenye ‘handaki la utajiri’

Kulwa Magwa

MACHIMBO ya Sambaru yapo takriban kilometa 83 kutoka Singida mjini, ambapo kijiji hicho kimepakana na vijiji vya Mang’onyi katika wilaya ya Ikungi na Londoni kilichopo Manyoni. Sambaru yenyewe ipo katika wilaya ya Ikungi.

Kijiji hicho ni miongoni mwa vijiji vingi vya mkoa wa Singida ambavyo vimejaaliwa kuwa na madini ya aina mbalimbali, hivyo sio jambo la ajabu sehemu hiyo kuwaona wachimbaji wengi wadogo wakiwa na dhana zao duni za uchimbaji.

Sambaru imezungukwa na migodi mikubwa, midogo na wachimbaji pamoja na watu wanaojihusisha na shughuli zinazoendana na madini ya dhahabu. Nami nimebahatika kuwa mmoja wao japokuwa sipo huku kwa ajili ya uchimbaji, ununuzi, ukusanyaji au upembuaji wa dhahabu. Nipo Sambaru kwa shughuli za ‘utafiti’.

Katika utafiti wangu nimebahatika kufika katika eneo linalotumiwa na wachimbaji wadogo, ambalo wenyewe wanaliita ‘Namba mbili’ wanalosema wamepewa kwa muda wajitafutie riziki na kampuni kubwa ya uchimbaji madini ya Shanta Mining. Kampuni hiyo ndiyo inayomiliki leseni ya uchimbaji katika eneo hilo.

Kwa ujumla katika mazingira haya ya wachimbaji hawa wadogo pamejaa mambo! Yapo matusi, fujo za hapa na pale, kupigana na matumizi ya bangi. Vyote hivyo ni vyao. Nami najichanganya nao kupata uzoefu wa maisha yao, ingawa hapa sijapata mwenyeji wa kuniongoza kwa lolote.

Kwa kuwa eneo lenyewe linahusisha watu wengi (takriban 100 na ushei) napata wawili- watatu wa kuwa nao karibu. Kwanza tunaongea mambo mengine ya kimaisha nan i vipi nimefika hapa. Nawaambia nipo sehemu hii kujifunza.

Baadaye nawauliza mambo mbalimbali kuhusu shughuli zao hasa wanavyochimba dhahabu ili nami niwapo huko mtaani, hususan mjini – niwe na chochote cha kusimulia.

Wananiambia mambo kadhaa wanayofanya kabla, wakati na baada ya kuingia shimoni, yaani ndani ya mgodi wanaochimba. Wananipa A, B, C ambazo usipozifuata hutaifurahia kazi yako chini ya ardhi, ikizingatiwa kwamba mashimo wanayochimba yana urefu wa kati ya futi 300 hadi 700 hivi. Huo ni umbali ambao ni hatari iwapo mhusika hatachukua tahadhari.

Baada ya darasa, nafarijika kwamba kumbe hata mimi naweza kuchimba dhahabu kama wao wanavyofanya. Hata hivyo naonywa kwamba, iwapo niko tayari kushuka chini ya ardhi niwe tayari kwenda kushika sululu, kupiga ponchi, kupandisha udongo juu na kuupeleka mahali wanapoukusanyia.

Onyo hilo linanisukuma kukubali maana nataka kujifunza kazi yao. Naulizwa iwapo nimekunywa pombe kwa kuwa wao hawataki mtu aingie shimoni akiwa amekunywa pombe hata kama hakulewa. Jibu nalowapa ni kuwa sijanywa chochote isipokuwa maji.

Naambiwa sasa naweza kushuka umbali wa futi 600, lakini huko chini hakuna shangazi wala mama wa kumdekea kwa kuwa kila aliyepo sehemu hiyo ni ‘baba’. Kauli hiyo sikupata ufafanuzi wake mpaka nilipoondoka sehemu hiyo.

kushuka2

PICHA: Mwandishi wa makala haya akishuka chini ya mgodi

Taratibu tunaanza kushuka chini tukitumia ngazi zilizotengenezwa kwa miti. Naambiwa niwe makini maana miti ile inateleza na iwapo nitajitia mwenyeji naweza kuporomokea chini, ambako kufika ukiwa hai ni nadra.

Kwa muda wa dakika 35 hivi tunakuwa chini kabisa ya mgodi. Giza nene naliona lakini kwa mbali nauona mwanga wa tochi japokuwa hauridhishi.  Nauliza kwa mwenyeji aliyekuwa mbele yangu ambaye ananijibu “usiwe na wasiwasi, watu wako kazini”.

Umbali wa futi 130 kutoka juu hadi tulipo unanitisha. Hapa naambiwa hata mwanga naouona wa tochi ni watu wanaokusanya mchanga, lakini uchimbaji wenyewe unaendelea mbali kidogo na mahali hapo. Kumbuka tulipo ni katika ‘kituo’ cha kupandishia juu mchanga au lango kuu la kupandia juu.

Mwenyeji wangu ananielekeza taratibu jinsi ya kupishana na watu tuliowakuta wakikusanya mchanga, huku akinimulikia mwanga kwa tochi ili niweze kupita. Kumbuka kwamba kwa hapa tunatembea na siyo kushuka. Tunatembea taratibu huku nikijigonga mara kwa mara kwenye vifusi vya mchanga vilivyolundikwa sehemu hiyo, lengo likiwa nifike mahali walipo wanaochimba.  

hassan

PICHA: Hassan Said akimmulikia mwandishi na kumwelekeza jinsi ya kushuka mgodini

Baada ya dakika chache tunafika sehemu wanapochimba. Hapa nashangazwa jinsi wanaume wale wanavyofanya kazi katika mazingira yenye ubaridi, ingawa kutokana na ugumu wa kazi yao wanatoka jasho – tena jingi. Nasalimiana nao na wao wananikaribisha kwa kunipatia sululu.

Kwa kuwa sijui wanavyotumia kifaa hicho kwa kazi yao, naelekezwa. Mmoja kati yao anaona kama nafanya mzaha vile, ananinyang’anya. Natupiwa tusi na kuombwa niondoke mahali pale. Natoka kwa unyonge japo najiona shujaa walau kwa kushika tu sululu, tena katika mazingira yale.

Mwenyeji wangu ananitaka tuondoke ili upepo usinibadilikie, ikizingatiwa kwamba wachimbaji wengi wadogo akili zao ‘wanazijua wenyewe’ kwa kuwa si ajabu kwao kumtwanga mtu kwa sululu.

 

kushuka

PICHA: Mwandishi wa makala haya akipanda juu kutoka chini ya mgodi

Tunaondoka taratibu na ‘jamaa’ yangu hadi kwenye lango kuu. Hapa tunakuta mifuko (viroba) vya kilo 50 vikiwa tayari vimejazwa mchanga na vimepangwa huku vingine vinafungwa kwa ajili ya kupandishwa juu. Hapa pia nakutana na amri nyingine; “hakuna kutoka mpaka tumalize kazi hii”.

viroba

PICHA: Mifuko yenye mchanga ikisubiri kupelekwa kusagwa ili kupata dhahabu.

Kauli hiyo inamsukuma jamaa yangu kuingilia kati na kuwaambia; “huyu ni mgonjwa, namtoa nje akapate dawa”. Anawadanganya. Wanakubali na kuturuhusu kupita. Kwa ujumla kazi ya kupandisha mchanga juu kutoka chini ni ngumu na wengi wao hawaipendi, naambiwa kwamba kila mara hubadilishana au kupangiana zamu.

Wazoefu wanasema kuupandisha mchanga japokuwa hutumia nyenzo, lakini ni duni na lolote linaweza kutokea. Nyenzo tegemeo ni ‘winchi’ ya miti na kamba za mkonge zilizosokotwa. Naambiwa kazi hiyo wengi hawaipendi maana kamba inaweza kukatika na kiroba kuporomoka; na iwapo kitafikia mwili wa mtu huo unaweza kuwa mwisho wa maisha au ulemavu wa kudumu.

Tunapanda taratibu na mwenyeji wangu hadi juu, umbali unaotugharimu tariban saa moja hivi. Mpaka hatua hii, jasho jingi limenitoka ikizingatiwa kwamba wakati nashuka chini nilikuwa nimevaa koti, tena zito. Naangalia simu yangu inaonyesha kuwa muda huo ni saa 7:23 ilhali wakati tunashuka ilikuwa saa 5:17, hivyo naambulia uzoefu wa takriban saa mbili chini ya mgodi mojawapo wa wachimbaji wadogo wa Sambaru.

site-dhahabu

PICHA: 'Saiti' ya wachimbaji wa Sambaru inavyoonekana

Kwanini wanatumia vifaa duni? Nauliza swali hilo baadaye tukiwa nje. Mmoja wa wachimbaji anasema, serikali haijatekeleza mpango wa kuwawezesha kwa vifaa, lakini wamekuwa wakisikia kila mara viongozi wanazungumzia jambo hilo. Anaponda na kusema “hizo ni siasa na wamezizowea”.

Anasema katika kijiji jirani cha Londoni kilichoko jirani na Sambaru, kuna kampuni moja iliyozinduliwa kwa mbwembwe na waziri mmoja wa zamani kwa ajili ya kuwaazimisha vifaa wachimbaji hao, lakini wameshindwa kumudu kuvikodi.

“Vifaa vyao ni ghali kuviazima ndiyo maana tunatumia hivi vya kienyeji kujifanyia mambo yetu, “anasema mchimbaji huyo.

4 Comments
  • Kaka nakupongeza sana kwa kazi nzuri, Makala yako imenikumbusha mbali niliwahi kufika mgodi huo wa Sambaru mwaka 2010 kwa ajili ya kazi kama hii nikiwa na HAKI MADINI kazi ambayo ilifadhiliwa na TMF pia.

    Big Up sana imekaa vizuri na imenikumbusha mbali nikiwa hapo mgodini.

  • hongera kaka nimeipenda sana hii coz mimi napenda sana vitu vya kusismua kama hivi

     

  • We Kurwa uliwezaje kuingia huko mbona kunatisha? ila hongera kwa ujasiri nimependa kazi yako.

  • Stella, unajua unapokwenda katika mazingira mengine ambayo hukutarajia kuwa ungefika na kupata access kama hizo za kukutana na wachimbaji wadogo; na wakawa willing kukufanya uwe kama wao, ni vyema ukajitahidi kupata wala experience ambayo utakuja kusimulia kuhusu ugumu na changamoto ya kazi wanayofanya. Binafsi nafasi hiyo niliitumia hivyo, ndiyo maana nikapata uzoefu kiasi fulani

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *