Meya wa Jiji la Mwanza Matatani?

Jamii Africa
  • Adaiwa Kulibeba Kanisa lake
  • Ashindwa kuelezea ujenzi wa kanisa nje ya taratibu
  • Viongozi wa kanisa watupiana mpira na wa serikali

MEYA  wa  Halmashauri  ya Jiji la Mwanza, Josephat  Manyerere (Chadema),  anakabiliwa na kashfa ya kushirikiana na waumini wenzake wa Kanisa la Waadventista  Wasabaton(SDA Church)  ushirika wa Agano ambao  wanajenga kanisa lenye orofa pasipo kibali  wala  wataalamu.

Chanzo  cha habari  kimeliambia  gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina gazetini kwamba ujenzi huo umeanza  zaidi ya mwaka mmoja uliopita, huku kiongozi mkuu  wa wazee wengine wanne  wa kanisa  hilo ambaye pia ni  mfanyakazi   katika halmashauri ya Jiji la mwanza, Gervas  Kataga  akiwa ndiye  msimamizi  wa ujenzi huo.
Kashfa hiyo imetokea  huku   serikali  kuu  ikiendelea  kuamini  kazi zinazofanywa na madhehebu ya dini  na kusababisha   kutoa  msamaha wa kodi  katika  manunuzi  ya bidhaa.
Kwa  mujibu wa habari, Manyerere ndiye mwenyekiti wa kamati ya Fedha na Uchumi kanisani hapo.
Meya huyo ambaye ni diwani wa kata ya Nyakato  katika jimbo la Ilemela  anadaiwa kuwa miongoni mwa washauri  wa waumini wenzake  zaidi ya  100  ambao  wameamua  kukiuka   taratibu  na sheria  za ujenzi.
Inadaiwa jengo hilo halina bango(sign board),ramani  iliyochorwa  na kuthibitishwa na wataalamu wa halmashauri, mkandarasi, Mshauri  wala  Msimamizi mwenye  taaluma; na kwamba kazi hizo zinafanywa na waumini  wenyewe.
“ Ni jambo la kushangaza kwamba  badala ya kusimamia   taratibu  pamoja na sheria  za  nchi, Manyerere  ndiye  anaokenaka  mshauri  na kinga   ya waumini wenzake  kwa kuvunja  taratibu na  sheria  za ujenzi” kilidai chanzo chetu cha habari  na kuongeza kuwa
Kwa   mujibu wa habari, Manyerere   ni muumini  wa  Agano Seventh Day Adventist Church ,  hata  kabla ya kuchaguliwa kuwa  Meya  wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza  mwishoni mwa  mwaka jana.
“ huku  akijua fika kwamba kufanya hivyo ni  kosa kisheria na mbele za Mungu  kwa sababu hata maamndiko matakatifu yanasema kuwa ya Mungu mpeni  Mungu na  ya  Kaisali mpeni Kaisali” .
Habari zinadai  kwa kutumia wadhifa  wake,  Meya  amewazuia   watendaji wa halmashauri  ya Jiji ili  wasivunje  orofa  hilo  ili kanisa lianze  kufanya  taratibu za kupatiwa kibali cha ujenzi.
Habari hizo  ambazo pia  zimethibitishwa na  Manyerere  pamoja na Mhandisi  wa  Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Bonephace  Nyambele,  zinadai  kwamba  ujenzi huo  unasimamiwa na Mzee  wa kanisa hilo, Gervas  Richard  Kataga  ambaye  pia ni  muumuni wa muda mrefu  katika kanisa hilo.
Inadaiwa  Kataga  hana taaluma  yoyoye kuhusiana na ujenzi, isipokuwa  ni dereva   katika  ofisi za Halmashsuri ya Jiji la Mwanza.
Habari zinasema  Manyerere  kwa kushirikiana na  Kataga  ndio wahamasishaji wakuu  wa ujenzi huo.
“ Ni  kwa kutumia  wadhifa wake  ndio maana wataalamu wa ujenzi  kutoka ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji  wa Halmashauri ya Jiji  wameshindwa kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuzuia ujenzi huo usiendelee  au  kubomoa  jengo hilo kwa sababu linaweza kusababisha madhara  hapo  baadaye” chanzo cha habari  kilidai.
Gazeti hili   limeambiwa kuwa  orofa hiyo ni kwa ajili ya kanisa jingine la  kisasa  ambalo pamoja na mambo mengine litakuwa na uwezo kwa kutumiwa na watu 700  kwa  wakati mmoja.
Habari  zaidi zinadai  kwamba  eneo  la  sehemu ya  chini ya jengo hilo litatumika kwa ajili ya  watoto na kuongeza kuwa  orofa ya kwanza  itatumiwa na watu wazima.
Inadaiwa  kwamba  kanisa linatumia mafundi  wa ‘mitaani’  ambao  wanalipwa  ujira  wa kati ya shilingi 4,000  hadi  shilingi 5,000  kwa kila  mita  ya eneo.
Habari zinaendelea  kudai kwamba  ili kuharakisha ujenzi huo,   miezi michache iliyopita Manyerere  aliwaalika  madiwani  wenzake kutoka  nje  ya Jiji la Mwanza  kwa ajili ya harambee.
Alipoulizwa  kwa njia ya simu, Manyerere  alikiri kuwepo kwa ujenzi huo na kwamba yeye ni miongoni mwa waumini wa muda mrefu  katika kanisa hilo.
“ Kwani wewe  hizo namba za simu za viongozi wa kanisa umezipata  wapi hadi ukawapigia; mmoja wao  ameniambia kuwa umempgia  kumuuliza habari za ujenzi. Mimi ninakusahauri  ukamwone  mzee  wa kanisa ama mchungaji wa mtaa” alidai Manyerere.
Hata hivyo, Meya  huyo hakutaka  kutoa ufafanuzi  juu ya madai kuwa  amewazuia  wataalamu  wa ofisi ya Mhandisi wa Jiji  ili wasichuke hatua  kutokana na mapungufu  yanayokabili ujenzi huo.
 “  … kwani tatizo liko wapi bhwana;  hata kama mimi ninasali  katika kanisa hilo!. Hebu ninakushauri  ukamuone  mzee  wa kanisa (Gervas Kataga)  ama Mchungaji  wa mtaa  wa Mabatini ambaye ofisi  yake iko Mabatini SDA  Church”  alidai  Manyerere  wakati alipohojiwa  na mwandishi wa habari hizi  kwa njia ya simu.
Kabla  ya kuwasiliana  na  Mzee  wa kanisa hilo, mwandishi wa habari hizi  alimtafuta  mwenyekiti wa shughuli za ujenzi  katika  ushirika wa Agape SDA, Yusuf Mwita,  kwa njia ya simu ambaye pia  alikataa  kuzungumzia suala hilo kwamba siyo msemaji.
Mwita  alilishaur mwandishi  huyo ajaribu  kuwasiliana na  Mzee  wa kanisa hilo  ama mchungaji wa mtaa  wa Mabatini.
Alidai  pia  kwamba  atawasilaiana na muumini mwenzake  ambaye ni Meya  wa Halmashauri  ya Jiji la Mwanza ili  amweleze kuwa kuna waandishi wa habari  wamempigia simu  wakihoji kuhusu uhali  wa ujenzo wa  orofa kinyume na taratibu pamoja  na sheria za ujenzi.
“ Sawa  ujenzi huo  upo; lakini wewe  ni  Mwandishi wa habari  au Injinia  wa Halmashauri?. Kwa  nini unafuatilia  mambo  ya ujenzi wa kanisa  la  Mungu! Tafadhali,  kamuulize  Meya  au Injinia  wa Jiji” alisema Kataga..
 Mzee  huyo wa kanisa  alishauri  suala hilo  aulizwe  mchungaji wa mtaa  wa Mabatini kwa vile yeye ndiye msemaji.
Katika  hatua nyingine, mchungaji  wa mtaa  wa Mabatini, Daniel  Maiga  alikataa  kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa  mtaa hauhusiki  na ujenzi huo.
Alidai kuwa  kanisa la Agano   ndilo  lenye uwezo  wa kuzungumzia mambo yote  yanayohusiana na ujenzi  kwa sababu wao ndio  wenye jengo.
Mchungaji wa mtaa  wa Mabatini, Daniel Maiga  pia  aligoma kutoa ufafanuzi juu ya ujenzi huo  kwa madai kwamba yeye siyo msemaji.
“ Kwanza mimi ni mgeni katika mtaa  huu; hebu nenda ukamuulizee  Mwenyekiti wa Conference( South  Nyanza  Conference), Joseph Bulengeya”  alisema mchungaji Maiga  wakati  alipohojiwa  ofisini  kwake mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika  hatua nyingine, Bulengeya hakupatikana ofisini kwake ili aweze kuzungumzia suala hilo kwa madai  kwamba  alikuwa  kwenye kikao.
 Mhandisi wa Jiji, Bonephace Nyambele  alidai kuwa ofisi yake haina taarifa za kuwepo kwa ujenzi huo.
Hata hivyo, aliahidi kuwa atafuatilia  na kwamba ikibainika  lazima atachukua hatua za kiuhandisi  ikiwemo  kuzuia  ujenzi huo usiendelee.
Manyerere  alichaguliwa kuwa diwani  wa kata ya Nyakato kupitia  Chama  cha Demokrasia na Maendeleo  katika  jimbo la Ilemela  kupitia uchaguzi  Mkuu uliofanyika  Oktoba 31 mwaka jana.
Na. Juma Ng’oko
Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *