Mgogoro wa maji Mto Mang’ola utakuwa wa kudumu – Wananchi

Jamii Africa

WANANCHI wa Kata ya Mang’ola na Kata ya Baray wamedai kwamba kama Serikali haitaingilia kati mgogoro wa maji yanayotoka kwenye chanzo cha Mto Mang’ola basi vita ya kugombania maji hayo itakuwa ni ya kudumu.

Kata hizo mbili zinaundwa na vijiji sita ambavyo ni Mang’ola Barazani, Malekchand, Laghangareni vilivyopo Kata ya Mang’ola na vijijini vya Jobaj, Dumbechand na Qangdenda vilivyopo kata ya Baray.

Wananchi wa vijijini hivyo wanaodaiwa kufikia 30,000 wameingia katika mgogoro wa kugombania maji ya Mto Mang’ola yanayotumika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji cha vitunguu pamoja na mazao mengine.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake waliokuwa wakiendelea kuchimba mfereji mpya wa kupitisha maji baada ya maji kuzuiliwa kuelekea kwenye mashamba yao, Francis Mbago  mkulima wa vitunguu alisema, wameamua kuchukua sheria mkononi baada ya kuona mzao yao yanaanza kukauka.

“Tumepiga yowe vijana, wazee na akina mama wote wapo hapa kuhakikisha mfereji unachimbwa na maji yanakwenda mashambani.

“Viongozi wameziba masikio na hawataki kutusikia na huu mradi wa mfereji wa serikali ndio umesababisha vijiji sita kukosa maji, halafu kijiji kimoja cha Mbuganyekundu ndio kinapata maji mpaka yanakosa kazi.

“Sisi tunasema kama watakuja kufukia huu mfereji tunaouchimba hivi sasa basi vita ya kugombania haya maji kwa hapa Mang’ola itakuwa ni ya kudumu.

“Tupo tayari kumwaga damu kwa ajili ya haya maji kwani watu wote wanaoishi Mang’ola wa kutegemea maji haya kwa kilimo, mifugo na mambo mengine iweje wachache wapewe maji halafu watu wengi wanyimwe? alihoji Mbago.

 

Karatu, Arusha, Maji, Mang'ola
Baadhi ya wananchi wanaotumia maji ya Mto Mang'ola akishiriki zoezi la kuchimba mtaro mpya baada ya kudai kwamba mfereji uliojengwa na serikali kwa ajili ya kupeleka maji kwenye kijiji cha Mbuganyekundu umesababisha maeneo yao yenye vijiji vitano kukosa maji na kuanza kusababisha mazao yaliyopo kwenye zaidi ya hekari 3,700 kuanza kukauka. Asilimia kubwa ya wananchi wa Kata ya Mang'ola Tarafa ya Eyasi wilayani Karatu mkoani Arusha wamekuwa wakijishughulisha na kilimo cha vitunguu kwa njia ya umwagiliaji maji kwa kutumia Mto Mang'ola

Kwa upande wake akijibu  baadhi ya madai hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Karatu Clement Berege alisema, tayari alikwisha kutuma wataalamu wake kukutana na pande mbili zinazogombani maji hayo.

“Taarifa niliyoletewa hapa ni kwamba walikubaliana kusitisha kuchimba mfereji mpya ili idara husika ichukue hatua za kufanya na kesho (leo) tunatarajia kumpatia Mkuu wa wilaya taarifa ya suala hilo,” alisema Berege.

Hata hivyo mpaka mwandishi wa FikraPevu anaondoka eneo la tukio ulipokuwa ukichimbwa mfereji mpya baadhi ya wananchi waliendelea kusisitiza kwamba ujenzi wa miundombinu ya kupeleka maji kijiji kimoja cha Mbunganyekundu ulifanywa kwa upendele na bila kushirikisha wananchi wa upande wemnye vijiji sita.

1 Comment
  • Hii inaashiria upunguaji wa vitunguu vinavyolimwa maeneo haya.. Sijaelewa izuri ni kuwa maji yame pungua, au Mtaro umesababisha maji kwenda sehemu nyingine?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *