Mgombea Igunga azuiwa kumsalimia mwalimu wake

Jamii Africa

MGOMBEA ubunge jimbo la Igunga kupitia tiketi ya Chama cha Wananchi CUF Leopold Mahona amejikuta kwenye wakati mgumu baada ya mfuasi anayedaiwa kuwa ni wa CHADEMA kumzuia asimsalimie mwalimu wake wa zamani wa somo la Historia.

Tukio la aina yake lilitokea jana jioni Kata ya Simbo nyumbani alipozaliwa na kusomea mgombea huyo.

Akiwa amemaliza kufanya mkutano wa hadhara kijijini hapo na kuanza safari ya kurejea mjini Mahona aliyekuwa ndani ya gari alimuona mwalimu wake na kuamua kushuka kwenda kumsalimia.

“Licha ya kumuona mwalimu wangu wa somo la Historia hapa Simbo ni nyumbani kwangu ndipo nimezaliwa na kusomea hapa.

“Sasa nashangaa huyu mamluki wa CHADEMA ameletwa huku kwanza si mkazi wala mwenyeji wa Simbo, na anadiriki kunizuia kumsalimia ndugu zangu.

“Siasa gani wanatuletea Igunga licha ya mwalimu, pembeni ya nyumba niliyokwenda ile ni nyumba yetu. Inakuwaje watu wanatoka mikoa mingine kuja kutuzuia kusalimia ndugu zetu?” aliuliza Mahona.

Hatua hiyo ya kujibizana na mtu huyo ambaye aligoma kujitambulisha jina lake, ilimfanya meneja kampeni wa mgombea ubunge huyo, Anthony Kayange kushuka kwenye gari na kuanza kujibizana na mtu huyo

Katika hatua hiyo, Kayange alisikika akimweleza mtu huyo asijaribu kuleta siasa za vurugu Igunga kwa wananchi wa eneo hilo hawana tabia za kuvurugu.

“Sikiliza wewe, hao CHADEMA waliokuleta huku na kujifanya wewe mwamba wa kuzuia watu wasisalimie ndugu zitakugharimu mwenyewe.

“Igunga na Simbo ni nyumbani kwetu uchaguzi utapita wewe utaondoka tutabaki na ndugu zetu unaozuia tusiwasalimie,” alisikika akilalamika meneja kampeni ambaye jina lake halikufahamika mara moja.

Baadae mgombea huyo aliamua kumpuuza mtu huyo kwa kuamua kuondoka kuelekea mjini. Mtu huyo na wenzake wanadaiwa kusambazwa maeneo mbalimbali Jimbo la Igunga kwa ajili ya kufanya kampeni za nyumba kwa nyumba.

CUF WAPATA AJALI

WATU watano wamenusurika kufa baada ya gari aina ya Mitsubishi Canter lenye namba T. 779 BLF kung’oka bodi yake na kuanguka chini.

Ajali hiyo ilihusiha gari la muziki linalotumiwa na Chama cha Wananchi (CUF) ambapo kwa wakati huo lilikuwa likielea kwenye mkutano wa kampeni Kata ya Simbo Jimbo la Igunga.

Dereva wa gari hilo Saidi Mchemba alisema, ajali hiyo ilisababishwa na mzigo wa vyombo vya muziki kukimbilia upande mmoja na kusababisha bodi kung’oka.

“Nilikuwa napishana na basi sasa mazingira ya barabara kama unavyoyaona yanavituta vikubwa “rasta kali” kwa hiyo wakati tunapishana kumbe mzigo ukakimbilia ubande mmoja,” alisema Machemba.

AJALI YA PIKIPIKI

Faume Jumanne (26) ambaye ni DJ wa gari la muziki la CUF amenusurika kupoteza maisha baada ya pikipiki aliyokuwa akiiendesha kumtupa nje ya barabara.

Tukio la ajali hiyo lilitokea jana hiyo hiyo muda mchache baada ya lile la gari, ambapo DJ huyo alikuwa akipeleka “Booster” ya muziki eneo la mkutano.

Akizungumza jana kwenye Hospitali ya Nkinga alipolazwa kwa ajili ya matibabu Faume aliliambia Mtanzania kuwa amechanika sehemu ya kichwa mbele pamoja na mguu wa kushoto chini.

“Kulikuwa na gari mbele yangu tunapishana sasa kutokana na barabara kuwa na vumbi kubwa nikiwa najiandaa kupunguza mwendo ili gari lipite hapo ndipo pikipiki ilipohama njia na kunitupa porini,” alisema Faume.

“Nashukuru tangu nimnefika hapa nimepata matibabu haraka na dawa za kutuliza maumivu na tayari nimepiga X-Ray na majibu nimeambiwa nitapewa kesho (jana),” alisema Faume akiwa kitandani Hospital ya Kinga.

4 Comments
  • KUTOJIAMINI ni tatizo hata kwenye siasa kama hujiamini utakuja na kila aina ya vibondo bahati mbaya igunga hamna magazeti kabla !

  • hao cuf tunawajua,hawashindwi kujizuia wenyewe ili waambiwe ni chadema,wao si wamefunga ndoa bwana.

  • Uchaguzi Zambia!
    Tayari hodi imepigwa kwa vyama vya siasa vinavyoshika madaraka kama ccm,hodi imepigwa na vyama pinzani.CCM ikae chonjo kwa kuwaweka kiti moto kina nape mnaeye na katibu mkuu Mkama kuacha zengwe la kufukuzana ccm sanjari na kutatua kero za wananchi ktk mfumuko wa bei,bomoabomoa,matatizo ya ardhi,ubinafsishaji,ememe,mikopo ya wanafunzi,ukosefu wa ajira kwa vijana.yote haya yasipofanyiwa kazi haraka ni dalili tosha kwa ccm kudondoka uchaguzi ujao.
    naomba kuwakilisha vinginevyo tukubali mabadiliko.
    Theo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *