Mgomo wa Madaktari waanza; Hospitali zaidi zajiunga!

Jamii Africa

Katika hali inayoonesha kuwa uvumilivu umewashinda madaktari nchini wameanzisha mgomo ambao umeanza kushika kasi taratibu baada ya juhudi zote za kudai maslahi bora zaidi na mazingira bora ya kazi kushindwa. Mgomo wa madaktari umekuja baada ya mgogoro kati yao na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kushindwa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo.

Madaktari walitangaza kuwa wataanza kugoma siku ya Jumanne na kama vile utani mgomo huo umeanza licha ya juhudi kubwa za serikali kujaribu kuonesha kuwa mgomo haujaanza huku baadhi ya vyombo vya habari vikipigwa marufuku kutangaza au kutoa habari za mgomo huo. Baadhi ya vyombo vya habari vilijaribu kutangaza kuwa hali inaendelea kama kawaida lakini uchunguzi wa FP unaonesha kuwa madaktari wameanza kwa mgomo baridi huku wachache wakiwekwa kama dharura.

“Madaktari siyo wanyama wanajali utu kwa hiyo hatuwezi kugoma wote; ila kwamba mgomo baridi umeanza ndiyo umeanza; mtu akienda akiwa hana dharura kubwa hatopata daktari” amesema mmoja wa madaktari hao akizungumza kwa masharti ya kutokutajwa jina.

Wakati huo huo jioni ya leo kulikuwa na tetesi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Bi. Blandina Nyoni alikuwa ameitwa Ikulu. Bi. Nyoni ni mmoja wa viongozi wa wizara hiyo ambao madaktari nchini wanataka aondolewe kwani amekuwa ni mojawapo ya sababu za mgomo huo.  Haijajulikana kama kuna jambo lolote kwani taarifa nyingine zimedokeza kuwa Rais Kikwete ameondoka nchini kuelekea Uswisi. Na kuondoka kwa Rais wakati mgomo huu mkubwa unaanza kunaweza kuleta tafsiri hasi ya uongozi wake.

Hadi jioni hii baadhi ya hospitali tayari zimeshatangaza kushiriki katika mgomo huo, hii ni pamoja na taasisi ya saratani ya Ocean Road pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mbeya. Hospitali za Dodoma nazo zimeingia katika mgomo na kama utatuzi hautapatikana mapema kuna uwezekano mkubwa hospitali zote za mikoa na wilaya nchini kabla ya mwisho wa wiki zitakuwa zimeingia katika mgomo.

Madaktari wa Tanzania ni miongoni mwa madaktari wanaopata mafao duni zaidi duniani huku wakifanya kazi katika mazingira hatarishi zaidi na vitendeo vibovu. Wakati mgomo huu unaanza hospitali ya rufaa ya Muhimbili ilikuwa haina huduma ya uchunguzi wa CT Scan baada ya mashine pekee hospitalini hapo kuharibika na kusababisha wagonjwa kupelekwa kwenye taasisi nyingine. Hali hii ya ukosefu wa vifaa vya kisasa vya huduma ya afya vimefanya huduma hiyo kuwa duni nchini na vile vile ya gharama ya juu huku walio na uwezo wakiendelea kujipeleka au kupelekwa ng’ambo.

Mmoja wa wanasheria wakongwe nchini na mwanaharakati wa haki za binadamu akizungumza na Fikra Pevu kufuatia kuanza mgomo huu amehoji ni kwa nini Tanzania inaonekana imetelekeza sekta ya afya na hususan ubora wa huduma katika sekta hiyo. “HIvi Nairobi wana kitu gani ambacho sisi Tanzania hatuna? Hivi hao wanaotutibu huko India wana kitu gani ambacho hakiwezi kupatikana Tanzania” amehoji mwanasheria huyo ambaye kutokana na nafasi yake serikalini hakutaka kutajwa jina lake.

Hadi hivi sasa mwitikio wa wananchi umekuwa ni kuwaunga mkono madaktari kinyume na mwaka 2006 ambapo walijaribu kugoma. Uchunguzi unaonesha kuwa wananchi wengi wako upande wa madaktari wakiamini kuwa endapo maslahi na maisha ya madaktari yataboreshwa basi na hudumwa kwa wagonjwa nazo zitaboreshwa kwani madaktari watakuwa na vitu vichache zaidi vya kuhofia. “Unajua hutaki kwenda kwa daktari ambaye anakuhudumia wakati anafikiria ataendaje nyumbani wakati hana usafiri” amesema mmoja wa wananchi waliozungumza na mwandishi  kutoka hospitali ya Muhimbili. Mwana mama mwingine ambaye alikuwepo eneo hilo la Muhimbili alielezea kuunga mkono mgomo huo akidai kuwa “hali tayari ni mbaya; mgomo wa madaktari hautafanya hali yetu kuwa nzuri kwani tayari ni mbaya sasa ni bora wapewe mastahili yao na wapewe vitendea kazi na mazingira bora ya kazi ili wanawake na watoto waweze kupata huduma nzuri.”

Wakati huo huo, uchunguzi wa FikraPevu u naonesha kuwa licha ya serikali kutangaza kuwa itaondoa vipimo vibovu vya HIV vya SB Bioline ambavyo mtandao huu ulikuwa wa kwanza kuripoti kuwa vinatoa majibu ya uongo, vifaa hivyo bado vipo na vinaendelea kutumiwa na hakujawekwa utaratibu unaoeleweka wa kuondoa au kubadilisha. Vile vile uchunguzi unaonesha kuwa vifaa hivyo vinauzwa kwa bei ghali zaidi katika Tanzania kuliko katika nchi nyingine za Kiafrika. Kushindwa huku kwa serikali kuondoa vifaa hivi kunazidi kuweka afya za Watanzania katika rehani huku uongozi wa Wizara na serikali ukiwa umekwama pasi kujua la kufanya.

 

Fikra Pevu inaendelea kufuatilia masuala yote mawili na ya kuyatolea taarifa.

Na Fikra Pevu

4 Comments
  • Naunga mkono kinachoendelea kwa sababu ni mgomo halali na serikali imeshindwa/kukataa kushuhulikia suala hilo.

  • siasa haina nafasi kabisa katika mgomo wa madaktari cha msingi madaktari wapewe madai yao,mbona wabunge(wanasiasa)bila hata migomo wameongezewa mafao kwa asilimia zaidi ya 100,wapeni haki zao acheni blaa blaa wagonjwa wanapoteza maisha hpspitalini

  • Viongozi wetu waangalie tatizo kuliko kuangalia mtu/watu. Kwanini wanaongea na wandishi wa habari baadala ya kukutana na hao madaktari? au kwa vile hawatibiwi kwenye hizi hospitali? Nawaunga mkono madaktari lakini tunaoumia nisisi wanyonge! hashira zetu zitakuwa kwente sanduku la kura.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *