JESHI la polisi wilayani Bunda linamshikilia afisa tabibu Michael Msimu 43 kwa tuhuma za kudaiwa kumtoa mimba mhudumu wa Club ya pombe za kisasa (bar) ijuliknayo kwa jina la Savana iliyopo mtaa wa benki katikati ya mji mdogo wa Bunda mkoani Mara.
Hali hiyo imepelekea Salome Bugunda kuwa mahututi kwa zaidi ya siku tano.
Hali hiyo ilibainika baada ya mwandishi wa habari hizi kupata taarifa za kuwepo tukio hilo na kufika katika hospitali teule ya wilaya ya Bunda (DDH) jumapili ya Februari 24 mwaka huu na kumkuta mwanamke huyo akiwa mahututi huku hakuna mhudumu anayejali hali yake.
Mhudumu huyo, anadaiwa kutolewa mimba kiholela katika moja ya duka la dawa za binadamu analodaiwa kulimikili Dr.Msimu lililopo mtaa wa benki kisha kupelekwa katika kituo cha afya cha Manyamanyama na hatimaye DDH baada ya hali yake kuwa mbaya Februari 19, mwaka huu.
Taarifa za uchunguzi zimeeleza kuwa baada ya kumtoa mimba, Dr. Msimu alimchukua na gari yake na kumpeleka hospitalini hapo kwa ajili ya msaada zaidi kisha akatoa taarifa kwa wahudumu wa bar ya Savana kuwa waende kumwona mwenzao hospitalini hapo.
Akizungumza huku akiwa ameshikilia mpira wa maji yanayopitishwa kwa njia ya pua kwa mgonjwa huyo ndani ya wodi ya wanawake ya hospitali teule ya wilaya hiyo, rafiki wa mgonjwa Regina Benard alisema kuwa alifuatwa na Dr. Msimu akiambiwa kuwa aende hospitali kumwangalia mwenzake kwasababu alikuwa amefanyiwa upasuaji.
Alisema alipouliza kuwa kulikoni mganga huyo alisema kuwa mgonjwa alikuwa hospitali ya Manyamanyama na baada ya kuona hali yake inazidi kuwa mbaya ndipo alipelekwa hospitali teule na kufanyiwa upasuaji ambapo mpaka muda huo hakuweza kujitambua na hali yake kuzidi kuwa mbaya.
Naye mhudumu mwingine wa Bar hiyo ya Savana Mwanaidi Idd, alisema kuwa siku hiyo wakati yeye na wahudumu wenzake wakiwa kazini, alienda Dr. Msimu na kuwataka waende haraka hospitalini.
‘’Siku hiyo tulipoamka na kuanza kufanya kazi alikuja Dr. Msimu na kutuambia kuwa tuje hospitalini DDH kwa ajili ya kumuona mwenzetu amefanyiwa Oparation kisha akaondoka akiwa na mashaka na tulipofika hapa tukamkuta mwenzetu ana hali mbaya hajitambui’’ alisema Mwanaid.
Kwa upande wake mke wa mwenye Bar hiyo Suzana Samwel alisema kuwa hajui kama mhudumu wao alikuwa anaumwa au alikuwa na mimba na alifika hospitalini hapo baada ya kupata taarifa kuwa mhudumu wake amelazwa na yupo mahututi.
Mganga wa zamu aliyekutwa katika wodi hiyo na kujitambulisha kwa jina la Dr. Maganga alikataa kueleza chochote licha ya kukubali kuwa wakati mgonjwa huyo akipelekwa hospitalini hapo alikuwepo.
Jitihada za kuwapata viongozi wakuu wa hospitali hiyo akiwemo muuguzi mkuu Revocatus Kato hazikuzaa matunda kwasababu ilikuwa siku ya Jumapili ambapo mpaka waandishi wanatoka katika hospitali hiyo hali ya mgonjwa iliendelea kuwa mbaya zaidi huku hakuna mganga au muuguzi aliyekuwa akionesha kujali uhai wa mgonjwa huyo ikiwa ni pamoja na kumwekea mashine ya kupumulia.
Hata hivyo taarifa zilifikishwa katika kituo kikuu cha polisi cha wilaya ya Bunda ambapo askari wawili walifika hospitalini hapo na kuendelea kuchukua maelezo ya tukio hilo.
Mganga mkuu wa wilaya ya Bunda Dr. Rainer Kapinga alithibitisha kukamatwa kwa mganga wake huyo na kwamba alipojariu kupitia jalada la mgonjwa alikuta sababu ya kusafishwa kizazi ambapo kwa bahati mbaya kiliguswa na kutolewa.
Hata hivyo alisema hawezi kulitole taarifa zaidi suala hilo kwasababu lipo katika mikono ya sheria.