Mpwapwa: Wanaochimba madini bila leseni kusakwa

Kulwa Magwa

WATU wanaofanya shughuli za uchimbaji na utafiti wa madini katika wilaya ya Mpwapwa bila vibali, wako hatarini kukamatwa na kufikishwa mahakamani kutokana na kukiuka sheria za nchi.

Mkuu wa wilaya hiyo, Christopher Kangoye, alisema kuna watu wengi wanaoendesha shughuli hizo ambao utafiti wa awali umeonyesha kwamba hawana leseni wala vibali vya kufaya hivyo.

Christopher_Kangoye

Mkuu wa wilaya ya Mpwapwa, Christopher Kangoye

Kangoye alisema utafiti wao wa awali umeonyesha watu hao wako katika maeneo mbalimbali ambako wamekuwa wakifanya shughuli zao bila kutambuliwa.

“Kwa sasa tunakusudia kufanya msako mkali utakaokuwa na utaratibu wa kuwaadhibu wahusika palepale, tutafanya hivyo bila kumuonea mtu, “alisema Kangoye.

Mkuu huyo wa wilaya alisema ofisi yake inakusudia kufanya msako huo kwa kushirikisha idara ya mazingira, misitu, Jeshi la Polisi na mahakama – ambapo watuhumiwa watakuwa wanakamatwa na kusomewa mashitaka palepale na kisha kuhukumiwa.

Kangoye alisema, wameamua kufanya hivyo baada ya kubaini kwamba watu wengi wamekuwa wakitumia rasilimali za taifa kujinufaisha bila kujali zinalindwa kwa mujibu wa sheria.

Alisema, wanachotaka kufanya kuhusu suala hilo waliwahi kukifanya miezi michache iliyopita, pale walipoendesha msako dhidi ya waharibifu wa misitu katika vijiji mbalimbali na miongoni mwao walitiwa hatiani.

“Hivi karibuni tuliwakamata watu wengi wanaharibu misitu na wengine wanakata miti hovyo misituni ambao sheria ilichukua mkondo palepale kwa kuwa hakimu tulikuwa tunatembea naye, “alisema Kangoye.

Kwa mujibu wa sheria ya madini ya mwaka 2010, ni kosa kwa mtu kufanya utafiti au uchimbaji wa madini ya aina yoyote bila kuwa na leseni inayotolewa na Wizara ya Nishati na Madini, ambapo imetaja adhabu kwa wanaotiwa hatiani kuwa faini isiyozidi sh. milioni tano au kifungo cha miaka mitatu au vyote viwili kwa pamoja.

Sheria hiyo pia inasema iwapo inayotiwa hatiani inakuwa kampuni inapaswa kulipa faini ya sh. milioni 50 pamoja na kutaifishwa kwa madini husika na vifaa vilivyotumika kuchimba au kufanyia utafiti.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *