Miaka 56 baada ya Uhuru, Daraja la Mto Momba sasa kujengwa mwaka huu

Jamii Africa

KWA wakazi wa Kata ya Kipeta, Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, ujenzi wa Daraja la Mto Momba unaotarajiwa kuanza mwaka huu unaonekana kuwa ukombozi mpya kwao baada ya mateso ya miaka mingi ambayo yamekwamisha hata shughuli za maendeleo.

FikraPevu imeelezwa kwamba, upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii, hususan matibabu, kwa wakati wa Kipeta na Kilyamatundu umekuwa kama anasa kwao kwa miaka mingi tangu Tanzania ilipopata Uhuru miaka 56 iliyopita.

Daraja la Kamba katika Mto Momba

Miundombinu mibovu ya barabara na madaraja pamoja na umbali wa zaidi ya kilometa 150 kutoka huko hadi mjini Sumbawanga umekuwa ukiwafanya wajitoe muhanga kuvuka daraja la kunesanesa (daraja la kamba) katika Mto Momba kwenda kwenye Kituo cha Afya Kamsamba kilichoko Wilaya ya Momba mkoani Songwe.

Siyo mbali kutoka Kipeta, lakini kukosekana kwa daraja la uhakika katika Mto Momba unaogawanya mikoa ya Rukwa na Songwe kumewafanya wabebe roho zao mikononi kila wakati wanapovuka daraja hilo lenye urefu wa meta 75 – iwe usiku au mchana.

“Ni hatari sana, unaweza kupata kizunguzungu na kuanguka mtoni na inakuwa hatari zaidi pale unapokuwa na mgonjwa asiyejiweza ambaye mnalazimika kumbeba kwenye machela kwa sababu kwa wengi ni vigumu kuvuka na baiskeli au pikipiki ukiwa umepanda kutokana na kunesa kwa daraja hilo,” Clement Mwakatobe, mkazi wa Kipeta, aliieleza FikraPevu katika mahojiano maalum.

Kipeta ni miongoni mwa Kata 15 zinazounda Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na ni ya sita kwa kuwa na idadi kubwa ya wakazi licha ya kwamba iko pembezoni kabisa wa wilaya hiyo.

FikraPevu inafahamu kwamba, kati ya wakazi 305,846 wa halmashauri hiyo (kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012), wakazi 25,755 (wanaume 12,639 na wanawake 13,116) wanatoka Kata ya Kipeta, idadi ambayo ni kubwa kulinganisha na Kata ya Laela iliyoko kwenye barabara kuu ya Tunduma-Sumbawanga ambayo ina wakazi 23,729 (wanaume 11,244 na wanawake 12,485).

Kata nyingine zinazounda halmashauri hiyo na idadi ya watu kwenye mabano ni Kaengesa (wakazi 28,917), Muze (27,441), Kaoze (26,306), Mtowisa (26,143), Ilemba (26,078), Kalambanzite (20,786), Sandulula (18,755), Milepa (15,762), Mfinga (15,072), Mpui (14,831), Miangalua (14,419), Lusaka (13,866), na Msanda Muungano (7,986).

Tayari serikali imekwishatangaza kwamba ujenzi wa Daraja la Mto Momba utaanza mwaka huu ili kuunganisha mikoa ya Rukwa na Songwe.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani, akiwa ziarani mkoani Rukwa hivi karibuni, alisema daraja hilo lenye urefu wa meta 75 litajengwa ili kurahisisha mawasiliano kwa wakazi wa mikoa hiyo.

Mhandisi Ngonyani alitoa kauli hiyo mara baada ya kukagua barabara ya Kasansa-Kilyamatundu na eneo litakapojengwa daraja la Momba na kusema kuwa Serikali imeshampata mkandarasi atakajenga daraja hilo.

Serikali imeshatoa kiasi cha Shs. 3 bilioni katika mwaka wa fedha 2016/2017, fedha hizo zimetusaidia kutangaza zabuni na kumpata mkandarasi, tayari mkandarasi ameshapatikana na mkataba wa makubaliano ya ujenzi umeshakamilika,” alisema Mhandisi Ngonyani.

Alimtaka Meneja Wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Rukwa kuhakikisha anatoa ajira kwa wakazi waliopo Kata ya Kipeta ambako ujenzi wa daraja hilo utafanyika.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo kutakuwa kiungo muhimu katika barabara ya Kibaoni-Kasansa-Muze-Ilemba-Kilyamatundu-Kamsamba hadi Mlowo ambayo inaunganisha mikoa mitatu ya Katavi, Rukwa na Songwe.

Barabara hiyo ni kiungo muhimu kati ya mikoa hiyo kwani inapita katika Bonde la Ziwa Rukwa ambalo ni maarufu kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo

Mbunge wa Jimbo la Kwela, Ignas Malocha, aliishukuru Serikali ya awamu ya tano ya Dkt. John Magufuli kwa kutekeleza ahadi ya ujenzi wa daraja hilo ambalo kukamilika kwake kutawaletea maendeleo wakazi hao kwa vile litaufungua Mkoa wa Rukwa na kuunganisha na Songwe na Katavi.

“Kukamilika kwa ujenzi wa daraja hili kutarahisisha usafirishaji wa mazao ya biashara kutoka mkoa wetu kwenda mikoa mingine inayopakana na mkoa huu na kuokoa maisha ya wananchi ambapo awali walikuwa wa wakiliwa na mamba na wengine kusombwa na maji wakati kuvuka kwenye mto huu,” alisisitiza Malocha.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Msuka Mkina, aliwahakikishia wakazi Kijiji cha Kilyamatundu kuwa Wakala utasimamia ujenzi huo ili ukamilike kwa wakati na viwango na kupitia mradi huo wananchi hao watapata ajira.

“Naomba niwahakikishie wakazi wa hapa kuwa daraja hili sasa litaaanza kujengwa na nyinyi mtakuwa sehemu ya wafanyakazi katika ujenzi wa mradi huu nawaomba mtoe ushirika kwa mkandarasi pindi mradi huu utakapoanza,” alisema Mkina.

Madaraja ya Kalambo na Kavuu yakamilika

Daraja la Kavuu mkoani Katavi

Wakati Serikali ikijikita katika ujenzi wa Daraja la Mto Momba, tayari ujenzi wa madaraja mengine mawili katika mikoa ya Rukwa na Katavi yamekamilika na kuondoa changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili wakazi wa maeneo hayo.

FikraPevu inafahamu kwamba, ujenzi wa Daraja la Mto Kalambo limekamilika na barabara ya Sumbawanga-Matai-Kasanga Port yenye urefu wa 112km inaendelea kukamilishwa ambapo 71.4km tayari zimekwishawekwa lami.

Kukamilika kwa daraja na barabara hiyo kutawapunguzia wananchi changamoto ya usafirishaji wa abiria na mzigio lakini pia kutafungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa mkoa Rukwa na nchi jirani za Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Burundi.

"Tuliwaahidi wananchi kujenga darala na barabara hii ili wafanyabiashara na wakulima waweze kusafirisha bidhaa na mazao yao kwenda katika masoko kwa wakati na hivyo kukuza uchumi wao binafsi na taifa kwa ujumla,” alisema Naibu Waziri Ngonyani.

Aidha, Daraja la Kavuu lenye urefu wa meta 89 linalounganisha Halmashauri ya Wilaya ya Mlele na Halmashauri ya Wilaya ya Mpwimbwe mkoani Katavi ujenzi wake umekamilika na litaanza kutumika ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wa Julai.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *