Na Daniel Samson
“Nilipomaliza shule nikaanza mahusiano na huyo mwanaume, basi katika kipindi cha wiki tano nikajigundua sijielewi kutokana na mabadiliko niliyopata”, hayo ni maneno ya msichana Aisha Juma (17) aliyepata mimba muda mfupi baada ya kumaliza darasa la 7 katika shule moja kata ya Pwani mkoa wa Mtwara.
Aisha (Jina sio halisi) ni miongoni mwa wasichana wengi wanaopata mimba nchini na kukatisha masomo huku wakishindwa kutimiza ndoto zao za kielemu.
Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 , sehemu ya pili (II) ya sheria hiyo inatamka “Mtoto ni mtu aliye na umri chini ya miaka 18”, na kifungu kidogo cha 12 kinatamka kuwa, “Mtu yeyote hataruhusiwa kumfanya mtoto apate mateso, au adhabu ya kikatili, ya kinyama au afanyiwe matendo yenye kumshushia hadhi”.
Mimba za utotoni zinatajwa kuwa miongoni mwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo vinawatesa na kuwadhalilisha watoto wa kike na kuwa kikwazo kwa wao kufikia ndoto zao za kielimu
Baada ya kugundulika kuwa ana mimba, Aisha alifukuzwa myumbani kwao, hata alipomtafuta mwanaume aliyempa mimba anayejulikana kwa jina la Daudi Mitishamba hakufanikiwa kumpata. Binti huyo aliondoka Mtwara akiwa mjamzito na kuelekea Dar es Salaam kumtafuta dada yake aitwaye Salma Maulid ambaye alikuwa anaishi Kata ya Makumbusho, Wilaya ya Kinondoni ili aepukane na kile alichodai ni kutengwa na jamii inayomzunguka.
Aisha anasema alikuwa na kiasi kidogo cha fedha ambacho kisingeweza kumfikisha Dar es salaam,na hivyo safari yake iliishia Mkuranga, hapo alitelemshwa ambapo alikutana na dada mmoja anayeitwa Monica. Dada huyo alimchukua na kukaa naye kwenye chumba kimoja mpaka alipojifungua mtoto wa kiume mwezi Aprili 2017.
Ugumu wa maisha wamtoa Mkuranga hadi Dar es Salaam
Kutokana na ugumu wa maisha alikimbilia Dar es salaam kwa dada yake Salma Maulid anae ishi kata ya Makumbusho lakini hakumkuta kwani alikuwa amehama katika nyumba aliyokuwa anaishi hapo awali.
Watu aliokutana nao walimpeleka kwa Mjumbe wa Mtaa wa Sindano kata ya Makumbusho, Mwanahamisi Majid ambaye alimpokea na kukaa naye wakati mchakato wa serikali ya Mtaa kumrudisha nyumbani kwao Mtwara ukifanyika.
Mwanahamisi anasema alimpeleka binti huyo Ofisi ya Afisa Ustawi wa Jamii kata ya Mwananyamala B ambako huko Asha alihojiwa na ameendelea kuishi Makumbusho. Kutokana na madhira yaliyompata binti huyo ameshindwa kuendelea na masomo na sasa anamlea mtoto wake huku akiwa ametengwa na ndugu zake.
Aisha, msichana aliyepata mimba na kukatiza ndoto za kupata elimu
Hali Halisi ya Mimba za Utotoni
Kulingana na utafiti wa Shirika la Afya Duniani (2016), Tanzania inatajwa kuwa ni nchi ya tatu barani Afrika kwa matukio ya ndoa za utotoni na mimba kwa asilimia 28, ambapo kila mwaka wasichana 8,000 hupata mimba na kukatisha masomo.
Tatizo hilo bado ni kubwa katika nchi za Afrika Mashariki. Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Watu na Makazi (UNFPA) linaeleza kuwa msichana 1 kati ya 6 mwenye umri wa miaka 15 hadi 19 hupata mimba katika nchi hizo.
Inakadiriwa kuwa kila mwaka wasichana milioni 15 wanalazimishwa kuolewa katika umri mdogo na kupata ujauzito. Wasichana walio katika hatari ya kupata mimba ni wale wenye umri miaka 10 hadi 13.
Mwanaharakati Anena
Kwa msaada wa chama cha wanahabari wanawake TAMWA, mwandishi wa makala haya alifanikiwa kuzungumza na wadau mbalimbali akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Wanawake Katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJUKI) ambayo inafanya kazi za kutetea haki za wanawake katika kata ya Makumbusho, Janeth Mawinza yeye anasema matukio ya wasichana kupewa mimba na kutekelezwa yamekuwa kikwazo kwa wasichana kufikia ndoto zao.
“Kuna uozo huko mitaani, vipigo kwa watoto, vipigo vya majumbani baba na mama, ulawiti, ubakaji. Zaidi ni kushirikiana kuongeza nguvu na tukifanya wote kwa nguvu ya pamoja amani itapatikana na vitendo vya ukatili wa kijinsia havitakuwepo”, amesema.
Hata hivyo anaeleza kuwa ukatili wa kijinsia katika kata yake bado upo lakini sio kwa kiasi kikubwa ikizingatiwa kuwa wanashirikiana na wananchi kupinga vitendo hivyo ikiwemo kutoa elimu na kuwasaidia wale waliothirika warejee katika maisha ya kawaida.
Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Wanawake Katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJUKI), Janeth Mawinza akiwa ofisini Dar es Salaam baada ya kufanya mahojiano juu ya ukatili wa kijinsia kata ya Makumbusho, wilaya ya Kinondoni.
Athari za Kisaikolojia
Mtaalamu na Mshauri wa Masuala ya Saikolojia kutoka Taasisi ya Ustawi wa Jamii Tanzania, Zainabu Rashidi amesema mimba za utotoni zinaathiri mwenendo na tabia za msichana ambapo asipopata matibabu ya kisaikolojia uwezekano wa kufanya ukatili akiwa mtu mzima ni mkubwa.
“Mimba ina madhara mengi zaidi, msichana anaweza kumtupa au kumkimbia mtoto. Na mara nyingi anapokuwa na yule mtoto uchungu unazidi kwa hiyo anaweza akaendeleza tabia ambazo sio nzuri dhidi ya yule mtoto ikiwemo kumpiga”, anaeleza Mtaalamu wa Saikolojia na kuongeza kuwa hali hiyo husababishwa na mtazamo hasi wa jamii juu ya wasichana waliozaa katika umri mdogo ambapo hujiona ni wakosaji na waliotengwa na jamii yao.
Anasema ikiwa msichana aliyepata mimba akipata matibabu anaweza kurejea katika hali ya kawaida na kuendelea na maisha yake. Anaishauri jamii kutoficha ukatili wa kijinsia lakini wawasaidie waathirika kupata matibabu.
“Kuhakikisha wanapata huduma za kisaikolojia na ushauri ili kurudi katika hali ya kawaida. Ni jukumu la jamii kujua kwamba mtoto anapopata mimba sio kuficha lakini kuhakikisha anapata huduma za kijamii”, amesema, Mtaalamu huyo.
Mkakati wa Serikali kutokomeza Mimba za Utotoni
Serikali imezifanyia maboresho Sera na Sheria ili kumlinda mtoto wa kike dhidi ya mimba za utotoni pamoja na marekebisho ya Sheria ya Elimu sura 353 ambayo inatoa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka 30 kwa mtu yeyote atakayempa mimba mwanafunzi wa shule ya Msingi na Sekondari.
Katika kutokomeza ndoa na mimba za utotoni Serikali imeanza utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya wanawake na watoto unaojumuisha sekta zote zinazohusu wanawake na watoto kwa lengo la kupinga aina zote za ukatili na kupunguza mimba za utotoni kutoka asilimia 47 hadi 10 ifikapo mwaka 2020.
Malengo ya Maendeleo Endelevu
Katika Lengo la 5 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s 2030) linasisitiza Usawa wa Kijinsia katika jamii na linakusudia kuondoa aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na wasichana katika sekta binafsi na Umma ikiwemo usafirishaji wa watoto, udhalilishaji kingono na aina zote za unyanyasaji.
Ili lengo hilo litimie linazitaka nchi wahisani kutunga na kuimarisha sera madhubuti na sheria zinazolenga kukuza usawa wa kijinsia na kumuwezesha mwanamke na msichana katika nyanja zote.