Mitandao ya Kijamii inavyowanyima usingizi viongozi Afrika Mashariki

Jamii Africa

Licha matumizi ya intaneti kuongezeka katika ukanda wa Afrika Mashariki, watumiaji wa mitandao ya kijamii hawatafaidika na huduma hiyo kutokana vikwazo vya kisheria vilivyowekwa na serikali za nchi zao.

Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya mpaka Desemba 2017 imeonesha kuwa idadi ya watumiaji wa intaneti imeongezeka kufikia watu milioni 23 ambayo ni sawa na asilimia 45 ya Watanzania wote. Kwa upande wa Uganda matumizi hayo yamefikia asilimia 22.

Hivi karibuni marais wa nchi za Uganda, Yoweri Museveni na Tanzania, John Magufuli wamenukuliwa wakitoa kauli ambazo zinaashiria kuminya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni unaofanywa na watumiaji wa majukwaa na mitandao ya kijamii.

Kwa nyakati tofauti marais hao wawili ambao ni sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekuwa wakidai kuwa uhuru wa watu umevuka mipaka na kuna haja ya kudhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii ili kuhakikisha usalama wa mataifa yao.

Lakini wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema udhibiti huo wa mitandao ni kuwanyamazisha wananchi ambao wamekuwa na muamko wa kuhoji, kukosoa mwenendo wa viongozi wa serikali ambao wanapaswa kuwajibika kwa wapiga kura kwa kutoa huduma bora za kijamii.

Rais Yoweri Museveni (kushoto)  akiwa na rais John Magufuli (kulia) katika moja ya shughuli za kiserikali jijini Arusha

 

Nini kinaendelea Uganda…

Serikali ya Uganda imesema kuanzia Julai mwaka huu itawatoza kodi ya sh. 200 za Uganda wateja wa kampuni za simu wanaotumia mitandao ya kijamii ya WhatsApp, Viber, Twitter na Skype ili kukabiliana na ‘umbea’ unaoendelea katika mitandao hiyo.

Hatua hiyo imekuja baada ya rais Yoweri Mseveni kuiandikia barua ofisi ya Hazina, Machi, 2018 akielezea jinsi mijadala isiyo na tija kama ‘umbea’ inavyolikosesha taifa lake mapato na muda wa uzalishaji mali.

Ikiwa ni sehemu ya kodi mpya, makampuni ya simu yanayotoa huduma ya vifurushi vya intaneti yatawajibika kuwa na takwimu za wateja wao  wanaotumia intaneti ili kuhakikisha kila mtumiaji analipa  kodi ya ongezeko la thamani.

Waziri wa Fedha wa nchi hiyo, Matia Kasaija tayari ameanza mchakato wa kuifanyia marekebisho Sheria ya Kodi ya mwaka 2014 na mswada umepelekwa bungeni kwa mapitio baada ya kupitishwa na Baraza la Mawaziri.

Akihojiwa na wanahabari, Waziri Kasaija alisema kodi itakayotozwa kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii itasaidia kuimarisha usalama wa taifa na kuongeza uzalishaji wa umeme. “Kodi hii itasaidia kuimarisha usalama wa nchi na kuongeza umeme ambao nyinyi watu mtatumia kufurahia zaidi mitandao ya kijamii.”

Kawaida, watumiaji wa mitandao ya kijamii hununua vifurushi vya intaneti kupitia simu lakini bado haijafahamika wazi jinsi serikali itakavyokata kodi hiyo kwa watumiaji hao au namna watakavyoweza kujua watu walioingia kwenye mitandao kama Facebook na Twitter. Kimsingi kila mtu mwenye simu ya mkononi inayotumia intaneti atatozwa kodi.

Mabadiliko hayo yamewashangaza watu wengi hasa watumiaji wa teknolojia ya mawasiliano ikizingatiwa kuwa  upatikanaji wa intaneti nchini humo ni wa asilimia 22 na ziko juhudi mbalimbali za kukuza teknolojia ya mawasiliano.

Wengine wakihitimisha kuwa ni mkakati wa kuwanyamazisha wakosoaji wa rais Museveni ambaye anakusudia kufanya mabadiliko ya sheria ili kumruhusu kugombea tena nafasi ya urais baada ya muda wake wa kukaa madarakani kumalizika.

Siyo mara ya kwanza kwa viongozi wa Uganda kuweka mikakati ya kisheria inayokusudia kudhibiti uhuru wa kujieleza. Februari, 2016 wakati wa uchaguzi mkuus, serikali ilizima mitandao ya Facebook na Twitter sambamba kuzuia huduma za kifedha kwa njia ya mtandao. Baada ya uchaguzi mitandao iliendelea kufanya kazi kama kawaida.

Miezi michache baadaye serikali ilinunu mtambo kubaini maudhui ya picha za ngono (pornography detecting machine) yenye thamani ya Dola za Marekani 88,000 kwa lengo la kulinda maadili na tunu za taifa.

June mwaka jana, Kituo cha Habari cha Uganda kilitangaza kuwa kimeanzisha kitengo maalum cha kupitia wasifu wa watumiaji wa mitandao ya kijamii ili kubaini mabandiko yenye maudhui ya ukosoaji. Mwezi uliofuata wa Julai, gazeti la Daily Monitor liliripoti kuwa serikali imeomba usaidizi kutoka China katika utekelezaji wa mpango kazi wa usalama mtandaoni ambao unalenga kusimamia na kuzuia matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.

 

Tanzania nayo haiko nyuma

Hatua inazochukua Uganda hazitofautiani sana na za Tanzania. Tumesikia matamko na kauli mbalimbali za viongozi wa serikali wakilalamikia uhuru wa uliovuka mipaka wa mitandao ya kijamii.

Aprili 21, mwaka huu, rais John Magufuli alijitokeza kwenye runinga wakati akiwaapisha Majaji 10 wa mahakama, ambapo alisema uhuru wa watumiaji wa mitandao kijamii umevuka mipaka na watu wanatumia uhuru huo kupotosha baadhi ya mambo yanayofanywa na serikali yake.

“Kuna ugonjwa tumeupata Tanzania wa kufikiri kila kinachoandikwa kwenye mitandao ni cha ukweli. Sasa sifahamu huu ugonjwa umetoka wapi? Lakini ni kwasababu hii mitandao hatuicontrol (hatuisimamii) sisi, wako huko wenye mitandao yao, wao interest (maslahi) yao ni kutengeneza biashara hawajali madhara mtakayoyapata.” Alinukuliwa rais Magufuli.

Kauli ya rais imekuja wakati kukiwa na mjadala mpana wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali ya mwaka 2017 ambayo inaonyesha kuwa trilioni 1.5 hazijulikani zimetumikaje.

Licha ya rais kukerwa na uhuru wa kujieleza na kutoa maoni ambao unatambulika na katiba ya nchi na mikataba ya kimataifa, Tanzania ilipitisha Sheria ya Maudhui ya Mtandaoni ya Mwaka 2015 ambayo imewatia hatiani baadhi ya watu kwa makosa mbalimbali ikiwemo ‘uchochezi’.

Ili kuipa nguvu sheria hiyo, mapema mwaka huu serikali imepitisha Kanuni Mpya za Maudhui ya Mtandaoni za mwaka 2018 ambapo katika kifungu cha 4 kinawataka wamiliki wa blogu, tovuti, majukwaa, radio na runinga za mtandaoni kujisajili ili wapate leseni za kuendesha shughuli zao.

Waliopewa mamlaka ya kusimamia maudhui ya mtandaoni ambao ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) watakuwa na uwezo wa kuwalazimisha wamiliki wa blogu au tovuti kuondoa maudhui yanayodhaniwa kuwa hayafai ndani ya saa 12 na kama hawajatimiza maagizo hayo wanaweza kulipa fidia isiyopungua milioni tano  au kifungo kisichopungua mwaka mmoja jela.

Akizungumza Septemba 28, 2016 wakati wa uzinduzi wa ndege mbili aina ya Bombadier Q400 katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, rais Magufuli alinukuliwa akisema, “Natamani siku moja malaika washuke waizime hii mitandao yote ili baada ya mwaka mzima itakapokuja kufukunga wakute sisi tumeisha tengeneza Tanzania yetu mpya.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *