Baada ya China kufunga biashara ya pembe za ndovu, mtandao wa watumiaji wa teknolojia duniani wameungana kukomesha biashara hiyo haramu na bidhaa zake inayofanyika mtandaoni.
Hatua hiyo ni kuunga mkono juhudi za mashirika ya kimataifa na Serikali ikiwemo ya Tanzania katika kukabiliana na ujangili wa Tembo ambao wako katika hatari ya kutoweka kabisa duniani .
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2016 unakadiria kuwa mpaka sasa kuna Tembo 352,000 ambapo idadi hiyo imepungua kutoka milioni 1.3 mwaka 1979. Takwimu za sensa ya Tembo zinaeleza kuwa idadi ya Tembo barani Afrika imepungua kwa 30% kati ya mwaka 2007 na 2014. Tanzania nayo imekumbwa na anguko kubwa la idadi ya Tembo ambapo inakadiriwa kuwa wamepungua kwa 80%.
Kundi la wafanyabiashara ya mtandao, teknolojia na mitandao ya kijamii duniani watashirikiana na shirika la uhifadhi wa wanyamapori (WWF), Shirika la kimataifa la usafiri na Mfuko wa kimataifa wa Masuala ya wanyamapori (Ifaw).
Lengo la mtandao huo wa kutokomeza biashara ya wanyamapori ni kuzuia na kupunguza biashara hiyo kwenye majukwaa ya intaneti kwa asilimia 80 ifikapo 2020 na kuhakikisha biashara ya mtandao haihujumiwi na majangili na wafanyabiashara wasiofuata taratibu za kimataifa.
Kupitia mtandao huo utatengenezwa mfumo wa data za mienendo ya wanyamapori kwenye hifadhi, biashara ya bidhaa za tembo. Pia miongozo na taratibu za kufuata katika biashara ya wanyamapori inayofanyika mtandaoni ili kuepusha majangiri na watu wasio na nia njema kutumia teknolojia kufanya uhalifu dhidi ya wanyamapori.
Mashirika na makampuni yaliyojiunga na mtandao huo ni Mall for Afrika, eBay, Alibaba, Etsy, Baidu, Baixing, Huaxia Collection, Qyer, Kuaishou, Pinterest, Ruby Lane, Shengshi Collection, Tencent, Wen Wan Tian Xia, Zhongyikupai, Zhuanzhuan, 58 Group, Google na Microsoft.
Katika orodha hiyo utagundua kuna kampuni nyingi kutoka China, sababu kubwa ni kuwa kampuni hizo zinaunga mkono juhudi za Serikali ya nchi yao ambayo imepiga marufuku na kufunga biashara yoyote inayohusika na bidhaa za pembe za ndovu.
Kila kampuni itatengeneza na kutekeleza sera na mikakati yake ili kusaidia kukomesha biashara ya wanyamapori mtandaoni kwa kushirikiana na WWF na Ifaw; mashirika ambayo yanasimamia na kudhibiti biashara ya wanyama walio katika hatari ya kutoweka duniani.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa WWF, Cawford Allan amesema wahalifu na majangili wanaua na kuuza wanyamapori na bidhaa zake kwasababu hakuna sera za pamoja kwenye mtandao wa intaneti.
“Kukosekana kwa chombo cha pamoja kunatengeneza tatizo. Haya makampuni yameona tatizo na wameungana kuhakikisha intaneti haitumiwi vibaya na wafanyabiashara haramu”, alisema Allan.
Kinachoendelea Tanzania
Serikali kwa kushirikiana na WWF, Machi mwaka huu walizindua kampeni ya kuwavalisha tembo kola ili kuhakikisha tembo waliobaki wanalindwa dhidi ya majangiri katika hifadhi za taifa.
Kampeni hiyo itaanza kutekelezwa kwenye hifadhi ya wanyamapori ya Selous, ambayo kwa miaka 40 iliyopita imepoteza asilimia 90 ya tembo wote wanaopatikana Tanzania. Kampeni hiyo itawasaidia askari wa wanyamapori kukabiliana na majangiri na kuhakikisha idadi ya tembo inaongezeka katika hifadhi za taifa.
Tembo aliyevalishwa kola maalum kufuatilia mienendo yake
Mradi huo ambao utatekelezwa kwa miezi 12 ambapo tembo 60 katika hifadhi ya Selous watafungwa kola shingoni. Hatua hiyo itawawezesha wasimamizi wa hifadhi kufuatilia mienendo ya tembo, kubaini na kukabiliana na hatari yoyote dhidi ya wanyama hao.
Kola hizo zitaunganishwa na mfumo wa ‘satellite’ ikiwa ni njia iliyohakikiwa na wanasayansi katika kufuatilia mienendo na ulinzi wa Tembo. Kabla ya Tembo kuvalishwa kola maalumu anapewa dawa ya usingizi na kuchukuliwa taarifa zake za kiafya. Atafuatiliwa kokote aendako na ikiwa atakabiliwa na hatari, askari watajitokeza mara moja kumsaidia.
Kwa miaka 40 iliyopita ujangili wa Tembo katika hifadhi ya Selous ilichochewa na biashara ya pembe za ndovu ambazo zilikuwa zinahitajika sana katika bara la Asia hasa nchini China. Inakadiriwa idadi ya Tembo katika pori hilo ilishuka kutoka 110,000 hadi 15,200.
Mwaka 2014, Shirika la Elimu na Utamaduni (UNESCO) liliiweka Selous katika orodha ya urithi wa dunia ambao uko katika hatari ya kutoweka kwasababu ya matukio yasiyo ya kawaida ya ujangiri wa tembo.