Mjadala mpya: Wanasheria wataka wanawake waruhusiwe kutoa mimba

Jamii Africa

CHAMA cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kimedhamiria kuibua mjadala mpana kutetea utoaji mimba salama nchini.

Mkurugenzi wa TAWLA, Tike Mwambipile, anasema mjadala unapaswa kulenga kuzuia utoaji mimba usio salama unaowasababishia wanawake matatizo mbalimbali na vifo.

“Uanzishwe mchakato wa kuingizwa kwenye sheria za Tanzania, vipengele vinavyoruhusu haki ya afya ya uzazi wa mpango vilivyomo kwenye Mkataba wa Nyongeza wa Afrika (Maputo Protocol) kuhusu haki za wanawake,” anasema.

Ibara ya 14 ya Maputo Protocol kuhusu “afya ya jinsia na haki ya kizazi” inazitaka nchi zinazosaini ikiwamo Tanzania, kupitia Kifungu 2c kulinda haki ya kizazi kwa wanawake kwa kuruhusu utoaji mimba kitabibu, endapo mimba imetokana na mwanamke kubakwa, kushiriki ngono na ndugu (maharimu), au mimba inahatarisha afya na uhai wa mama.

TAWLA inasema mimba 405,000 hutolewa nchini kila mwaka. Asilimia 40 ya wanawake wanaotoa mimba hupata madhara yanayohitaji huduma za kitabibu ikiwamo kuvuja damu nyingi.

 

HOJA

TAWLA inasema kuruhusu kisheria utoaji mimba salama, kutaokoa maisha ya wanawake wanaoangamia kwa utoaji mimba usio salama vichochoroni.

“Hatusemi kila anayejisikia atoe mimba; hapana, yaainishwe mazingira na sababu maalumu… Wanawake wengi wanateseka na kufa; tatizo ni kubwa; tuanze kulizungumzia,” anasema.

Dk. Pasiens Mapunda wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), anasema utafiti uliotolewa Machi 2016 na Taasisi ya Guttmacher (New York); Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na Chuo Kikuu cha Muhimbili unaonesha wanawake 47,000 (asilimia 13-15) hufariki dunia kwa mwaka kwa utoaji mimba katika nchi zinazoendelea zinazozuia utoaji mimba ikiwamo Tanzania ambapo ni wastani wa mimba 36 kwa kila wanawake 1000.

Anasema; “Utoaji mimba usio salama unashika nafasi ya pili kusababisha vifo kwa wanawake kuhusiana na uzazi nchini huku kutokwa damu nyingi wakati wa kujifungua kukiongoza.”

 

SABABU ZA UTOAJI MIMBA

Baadhi ya sababu za wanawake kutoa mimba zinahusisha kukwepa aibu kwa mimba zitokanazo na ngono katika umri mdogo na kabla ya ndoa; hofu ya kukatisha masomo na kupanga uzazi kupishanisha watoto.

Pendo Mashauri wa Sabasaba Tarime anasema, “Wengi walitaka nitoe mimba; eti nina mtoto mdogo ni aibu; inabidi nitoe ili wapishane, nikakataa nimejifungua…”

Nyingine ni hofu ya ugumu wa maisha, kubakwa na wanawake kutumia utoaji mimba kuwakomoa wenza.

Kabla mwandishi hajafunga ndoa, Elizabeth aliyeishi Tabata wakiwa na mahusiano, alimwambia, “Kama hunioi mimi, ‘nakichomoa’ hiki ki-mimba nilicho nacho.” Hawakuoana; wakakata mawasiliano.

 

VICHOCHEO VYA UTOAJI MIMBA USIO SALAMA

Kaimu Mkurugenzi wa Programu, Uzazi na Malezi Tanzania (UMATI), Dk. Saili Mbukwa anasema hofu ya kushtakiwa wanawake na watoa huduma za afya, huchochea utoaji mimba wa siri usio salama.

Dk. Bahati Maxwell wa Kituo cha Afya cha Buguruni-Anglican Ilala, anasema, “Kisheria, utoaji mimba salama, unaruhusiwa kwa sababu maalum za kitababu jopo la madaktari wasiopungua watatu linapojadili na kuafikiana kuwa hilo ndilo suluhisho pekee kuokoa uhai wa mama.”

Mambo yanayosababisha uamuzi wa madaktari kufanya utoaji mimba kisheria na kimiongozo yanahusisha mimba kutungwa nje ya kizazi, matatizo yanayoongezeka mimba inapokua na kuhatarisha maisha kama kifafa cha mimba, shinikizo la damu na kisukari.

Mwenyekiti wa Shirika la Kutetea Uhai (Pro-Life) Tanzania, Emil Hagamu, anasema mimba moja kati ya 1,000 hutolewa kila mwaka kwa ushauri wa jopo la madaktari.

 

USIRI MKUBWA

Wilayani Ilala, baadhi ya maduka ya dawa yanauza vidonge vya majira na kuwauzia watu wanaowafahamu dawa zinazotumika kihalali na kitaalam kuwasaidia wanaoharibikiwa mimba (misoprostol) hata wasipokuwa na cheti cha daktari.

Irene anayeishi Madizini Ukonga anasema, “Mwaka jana rafiki yangu alikwenda Buguruni kununua miso (misoprostol) ili atoe. Wakasema hazipo. Aliporudi na kwenda rafiki yake aliyemwelekeza duka hilo, wakauziwa Shs. 60,000.”

 

DAWA ZA KIENYEJI HADHARANI

Kadhalika, utoaji mimba hufanywa kwa dawa za kienyeji zikiwamo zinazouzwa na watu wa makabila mbalimbali wakiwamo Wamasai.

Kati ya wauza dawa saba wa Kimasai wa Mnazi Mmoja, Lumumba, Shaurimoyo na Buguruni Sokoni wilayani Ilala, watano wamekiri kuuza dawa iitwayo, “orkiloriti” kwa Shs. 30,000 hadi 100,000 kutegemea umri wa mimba na maelewano.

Charlie (33), anasema kwa mwezi huwauzia dawa takriban wanawake watatu; wastani wa utoaji mimba 36 kwa mwaka.

 

UPINZANI MKUBWA

Pro-Life inasema utoaji mimba ni mauaji ya watoto ambao hawajazaliwa hivyo, katika kumsaidia mama, juhudi ziwekwe kuwaokoa mama na mtoto.

Maputo Protocol na sheria za Tanzania zinaweka juhudi zaidi kumuokoa mwanamke anayekuwa hatarini kupoteza maisha na kupuuza haki ya mtoto kuishi.

“Zikitungwa sheria kuruhusu kutoa mimba kwa sababu yoyote, hospitali zitakuwa bucha za kuwachinjia watoto,” inasema.

Mratibu wa taasisi ya ULINGO, Dk. Avemaria Semakafu anasema, umma uzingatie uadilifu na elimu sahihi kulinda uhai. Anahoji, “Mwanamke akipata mimba na VVU, akitoa mimba atatoa na ukimwi?”

Nsachris Mwamwaja, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, upande wa Afya, anasema, “Mambo ya kisheria na kisera yana taratibu zake hadi kujadiliwa bungeni… kwa sasa kutoa mimba ni kosa la jinai.”

 

NINI KIFANYIKE?

Wadau wanataka mjadala mpana kitaifa kuona kama kuna haja kutunga sheria zinazoruhusu utoaji mimba salama kwa sababu na mazingira maalum kitabibu. Wauzaji wa dawa za kutoa mimba wabainike na kudhibitiwa.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *