KILIO cha miaka mingi cha tatizo la usafiri wa Reli ya Kati kinaonekana kinakaribia kwisha, baada ya serikali za Tanzania na China kufikia makubaliano ya ujenzi wa reli hiyo.
Taarifa iliyotolewa Ikulu ya Dar es Salaam, Tanzania baada ya Rais John Magufuli kukutana na Balozi wa China nchini Tanzania Bw Lu Youqing, imesema kufikiwa kwa makubaliano hayo kunatokana na juhudi za muda mrefu, kwenye hatua za kutafuta vyanzo vya fedha za mradi na mkandarasi.
Makubaliano haya yamefikiwa wakati Tanzania inaendelea kunufaika na wakandarasi wa China ambao hutoa bei zisizo za kuumiza kwenye kandarasi zao, na wakati imani ya umma wa Tanzania kuhusiana na ubora wa miradi ya miundombinu inayojengwa na kampuni za China ikizidi kuimraika, hasa baada ya kukamilika na kuanza kazi kwa mradi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara hadi Dar es salaam, na kufunguliwa kwa daraja la Nyerere linaliounganisha Magogoni na Kivukoni.
Kukamilika kwa miradi hiyo kwa viwango vya kuridhisha, siyo tu kumefurahisha watu wanaonufaika moja kwa moja na miradi hiyo, bali pia kumeonyesha ufuatiliaji zaidi kuhusu maendeleo ya China kwenye teknolojia za ujenzi wa miundombinu.
Lakini pia kumeonyesha kuchangamka na kutotaka kubaki nyuma kwa serikali yetu, hasa wakati tunashuhudia nchi nyingine za Afrika zikiendeleza miradi ya kisasa na kupiga hatua kwenye maendeleo ya ujenzi wa miundo mbinu.
Kuna sababu nyingi zinazofanya kuwe na matumaini makubwa kuhusiana na ujenzi wa mradi huu. Kwanza, kwenye mazingira ya sasa ambayo vijana wengi wanasumbuliwa na tatizo la ajira, kampuni ya China kupewa kandarasi ya ujenzi wa reli hiyo, kunatarajiwa kuleta unafuu wa tatizo la ajira na hata kuleta maendeleo ya kijamii katika maeneo ambapo reli hiyo itapita.
Mfano mzuri kwa upande huu ulioonyeshwa na makampuni ya China, ni kama ule wa ujenzi wa reli ya kutoka Mombasa hadi Nairobi, ambapo wenyeji zaidi ya elfu 25 walipata ajira za moja kwa moja, na wengine walipata ajira zisizo za moja kwa moja.
Pili, ni kuwa mradi huu unakuja wakati kinara wa usimamizi wa ujenzi wa miundombinu kwenye serikali ya awamu ya nne, sasa ni mkuu wa nchi.
Kuna imani kuwa mchanganyiko wa kasi ya ujenzi wa miradi inayotekelezwa na kampuni za China, na usimamizi mkali wa serikali ambayo sasa iko chini ya kinara wa usimamizi wa ujenzi wa miundombinu, vitakuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania.
Na tatu, ni kuwa Tanzania imeamua kutobaki nyuma kati ya nchi marafiki wa China, kunufaika na miradi ya kiwango cha juu ya ujenzi wa reli za kisasa.
Ni wazi kuwa China kwa sasa ni moja ya nchi zenye teknolojia ya juu kwenye ujenzi wa reli, tukiangalia kilomita 112,000 za reli nchini China, na kilomita 19,000 ni reli ya kasi.
China inaweza kuweka uwiano kati ya kasi ya ujenzi wa mradi, gharama na ubora.
Kuna mifano iliyo hai ya reli zilizojengwa na makampuni ya China kama mradi wa reli ya Kaduna- Abuja wa nchini Nigeria wenye kilomita 187, na mradi wa ujenzi wa reli ya usafiri wa umma mjini Addis Ababa, nchini Ethiopia AA-LRT, miradi ambayo tayari imeanza kufanya kazi na kuwanufaisha wa tu wa nchi hizo.
Lakini wakati tunajiandaa kupokea mradi mkubwa namna hii, pia tunatakiwa kukumbuka na kurekebisha udhaifu uliokuwepo wakati wa ujenzi wa reli ya TAZARA kutokana na kuwa reli hiyo ilijengwa muda mfupi baada ya Tanzania kupata uhuru, hakukuwa na msingi imara wa kupokea teknolojia ya ujenzi wa reli au hata kuisimamia reli yenyewe.
Wafanyakazi wa reli hiyo wengi walikuwa ni wale wasio na elimu na walioshirki kwenye ujenzi, sehemu kubwa ya mafunzo waliyopata yalitokana na uzoefu kazini, na wachache walikwenda kupata mafunzo China.
Kwa sasa Tanzania ina mazingira mazuri ya kupokea teknolojia zinazohusiana na mambo ya reli kutokana na kuwa na vyuo vinavyotoa mafunzo hayo. Kwanza ni Chuo cha Usafirishaji cha Taifa NIT, Chuo cha Reli cha Tabora, na pia kuna chuo kingine cha mambo ya reli kilichoko nchini Kenya jirani na Tanzania.
Vyuo hivi siyo tu vitaondoa hali kama ya zamani wakati wa ujenzi wa reli ya TAZARA wakati China ililazimika kuja na wafanyakazi wengi hata wale wa kufanya kazi ndogo ndogo, na hata baada ya ujenzi wa reli kukamilika kubakiza wataalamu wa kusimamia reli.
Pamoja na kuwa Balozi wa China Bw Lu Youqing aliipongeza serikali ya Rais Magufuli kwa kuweka maandalizi mazuri kabla ya ujenzi kuanza, kinachotarajiwa kwa sasa ni kuhakikisha kuwa dosari zilizokuwepo wakati wa ujenzi wa reli ya TAZARA na hata dosari za usimamizi zilizofanya reli hiyo ikumbwe na matatizo, hazitatokeza kwenye reli ya Kati.