Msingi wa kuelewa maadili ya Mgomo wa Madaktari wa Tanzania

Jamii Africa

Hakuna mgomo unaoitishwa na wafanyakazi ambao unawagawa wananchi mara moja tena kwa ukali kama mgomo wa madaktari. Mara moja mgomo wa madaktari unapoitishwa pande mbili zinazokinzana hujitokeza kwa haraka kama kufuatana kwa radi na ngurumo. Pande hizi zinakuwa na tofauti kubwa sana kiasi kwamba kwa haraka haraka ni vigumu kuona ni jinsi gani pande hizo mbili zinaweza kupatana au hata kukaribiana na kutafuta suluhu.

 

Upande mmoja kunakuwepo na wale ambao mara moja wanachukulia uamuzi wa madaktari kugoma kuwa ni mashambulizi dhidi ya afya za wagonjwa. Hawa huamini kuwa hakuna mazingira yanayoruhusu madaktari kugoma kwa sababu kufanya hivyo ni kupitisha sentensi ya kifo kwa wagonjwa ambao wanawategemea madaktari hao. Hivyo, upande huu mara nyingi hujenga hoja kuwa madaktari waendelee na kazi wakati “matatizo yao yanashughulikiwa” kwani kutofanya hivyo “ni kuhatarisha maisha ya wagonjwa na watu wasio na uwezo”.

 

Hoja ya hawa pia inaupande unaotokana na kile kinachoitwa “wito wa udaktari” yaani ni miongoni mwa kazi ambazo toka enzi na enzi zilionekana zina wito wa pekee. Miongoni mwa kazi nyingine zilizoonekana ni za wito ni zile za kidini, uwakili na ualimu. Kiongozi wa dini anatakiwa kutoa huduma ya kiroho bila kujali anayempatia huduma hiyo ni mtu wa namna gani, wakili anatakiwa amtetee mtu kwa uaminifu wa hali ya juu na mwalimu anatakiwa kumfundisha mtu mjinga na kumwondolea ujinga wake hata kama kufundishika kwa mtu huyo ni kugumu kupita kiasi.

 

Hata hivyo, tofauti na kazi hizo nyingine za wito ni kazi ya udaktari kwa namna ya pekee ambayo ina kitu kingine kinachokosekana kwenye hizi kazi nyingine – uhai na kifo. Madaktari wanahusika na afya za wagonjwa na hivyo maamuzi yao (mazuri au mabaya) yana matokeo ya moja kwa moja kwa mwanadamu mwingine au wanadamu wengine. Daktari akigoma kusaidia mama mja mzito anayejifungua ambaye mtoto wake amekabwa na kitovu (umbilical cord) mama na mtoto maisha yao yanaweza kuwa hatarini.

 

Wakili akikataa kumtetea mtu au akimtetea mtu vibaya kuna uwezekano uamuzi mbaya (adverse decision) kwa mtu huyo unaweza kugeuzwa katika rufaa na kumpa nafasi nyingine. Mtu aliyefundishwa na mwalimu mbaya ana uwezo wa baadaye  kupata nafasi ya kufundishwa na mwalimu mzuri; mtu ambaye amechukizwa na mafundisho ya kiongozi wa dini yake anaweza akaamua kwenda na kukumbatia mafundisho ya dini nyingine. Mtu ambaye amekufa kwa sababu daktari ameshindwa kufanya kitu au amekifanya vibaya hana rufaa wala nafasi ya pili.

 

Ni kutokana na hili ndio maana watu wanaoamini katika kiapo cha Hippocriti wanaamini kabisa kuwa madaktari hawatakiwi kuchukua uamuzi wowote ambao utasababisha madhara kwa mgonjwa kwani ameapa “kutomsababishia madhara mgonjwa”. Hivyo, kwa msingi wa hoja hii mgomo wa madaktari ni mwiko kabisa na hakuna mazingira yoyote ambayo mgomo unaruhusiwa. Kwamba, hata kama madaktari wanafanya kazi katika hali mbaya kiasi gani, hata kama madaktari wana matatizo ya namna gani yanayotokana na maslahi yao, na hata kama madaktari wananyanyaswa vipi na mwajiri wao jukumu lao la kwanza ni kwa mgonjwa na wanatakiwa kufanya lolote lile kuhakikisha kuwa wagonjwa hawadhiriki. Mgomo unavunja utakatifu (the sacredness) wa kiapo chao.

 

Upande mwingine hata hivyo, wapo wale ambao wanaona kuwa madaktari nao kama wanadamu wengine wanaishi kwa kutegemea jasho lao. Kwamba, madaktari licha ya kwamba wanashughulikia afya wanatarajia kuwa na wao waweze kuishi maisha yanayoendana na utu na kutegemea ujuzi wao. Lakini vile vile madaktari wanatarajiwa kuwa katika hali inayowafanya  waweze kufanya kazi yao kwa ufanisi bila kuwa na sababu ya kutokuwa makini.

 

Kundi hili la pili linaangalia pia kiapo cha Hippokriti na ndani yake linaona kuwa hoja yao pia imefichika. Kwamba, kama daktari atakuwa na matatizo mengi ya binafsi, kikazi au hata ya kiakili basi hatoweza kuwa makini na mwadilifu katika kazi yake na hivyo kuwa tishio la maisha ya mgonjwa. Kundi hili linachukulia kiapo cha udaktari cha kutomdhuru mgonjwa kwa uzito zaidi! Kwamba, daktari anapokuja kazini kukutana na mgonjwa au anapoingia kwenye chumba cha upasuaji tunataka awe anafikiria mgonjwa na tiba siyo awe anafikiria gari lake mkweche, nyumba yake inayovuja, au deni lake analomdai mwajiri! Daktari wa aina hiyo ni wa hatari!

 

Mgomo kama hatua ya mwisho

Wakati sekta nyingine wanaweza kuchukulia mgomo kama kitu cha kawaida cha kudai maslahi kwa daktari mgomo ni lazima uwe hatua ya mwisho na unapochukuliwa usiachiliwe kirahisi – kwani ukiachiliwa kirahisi ni rahisi kurudiwa tena baada ya muda mfupi. Mgomo wa madaktari ni lazima uwe na malengo ambayo yanaeleweka, yanayotimilizika na ambayo yanaweza kubadilisha hali yao kwa haraka. Hauwezi kuwa mgomo wa jumla wa kudai “maslahi” tu.

 

Ni kwa sababu hiyo madaktari wanapoamua kugoma hasa kwa nchi nzima basi ni lazima taifa lishtuke. Ni lazima wanasiasa na viongozi wajiulize imekuwaje tumefika mahali madaktari wa nchi nzima wanagoma. Kwamba, kuna kitu kimeshindikana kwa njia ya mazungumzo hilo ni dhahiri na kwamba watawala na wanasiasa wameshindwa kuweka uzito kwenye hoja za muda mrefu za madaktari nalo ni dhahiri. Madaktari wanapoitisha mgomo wa nchi nzima ni lazima watu wawajibishwe (heads must roll!).

 

Hii ni kwa sababu matokeo ya mgomo wa madaktari kwa muda mfupi ni msukumo (pressure) kwenye sekta ya afya ambayo kwa kweli haistahili kuwepo kwani matokeo yake mara zote ni makubwa sana. Mara nyingi matokeo ya mgomo wa madaktari hayaondoki mara moja. Nchini Malta mgomo wa madaktari uliwahi kudumu kwa miaka kumi! Huko New Zealand mgomo wa madaktari ulisababisha madhara ambayo hadi leo bado mwangwi wake unasikika katika huduma ya afya. Mgomo wa madaktari kinyume na migomo ya kada nyingi matokeo yake hudumu kwa muda mrefu ndio maana tunaposikia madaktari wamegoma tusichukulie kiurahisi – manake ni kuwa wamelazimika kugoma.

 

Madaktari wa Tanzania na migomo

Mwaka 2006 mgomo wa madaktari wa Muhimbili haukuungwa mkono kitaifa. Kwa kiasi kikubwa ulihusiana na ongezeko la posho na mishahara. Wakati ule kwa wanaokumbuka niliunga mkono upande wa serikali. Niliamini kwa serikali ambayo ilikuwa imeingia madarakani miezi michache nyuma yake ilikuwa siyo nafasi nzuri ya kudai ongezeko kubwa kabla serikali hiyo haijakaa chini kupitisha bajeti mpya. Hivyo, mgomo ule kwa kiwango kikubwa ulikuja wakati usiofaa.

 

Hata hivyo, leo hii miaka zaidi ya mitano baadaye ninaamini kabisa kuwa kama serikali yetu ingetaka kushughulikia tatizo la maslahi na mafao ya madaktari ingeweza kufanya hivyo. Hakuna tatizo ambalo linazungumzwa leo hii ambalo lilikuwa halijulikani miaka minne nyuma au miaka mitatu nyuma. Niruhusu kufafanua.

 

Mwaka 2008 utafiti ulichapwa katika Jarida la East African Journal of Public Health Volume 5 Number 1 April 2008 ukiwa na kichwa cha habari “Motivation of Health Care Workers in Tanzania: A Case Study of Muhimbili National Hospital”. Katika utafiti huo mambo mbalimbali yalionekana ambayo naamini yatupasa tuyafikirie kidogo kabla hatujaamua kuchukua upande mmoja au mwingine katika mjadala wa mgomo huu unaoendelea.

 

Utafiti huu ulifanyika kati ya 2003-2004 ukihusisha watumishi 462 walihusishwa katika pool ya watumishi wapatao 2310. Watafiti waligundua mambo yafuatayo (kati ya mengine mengi)

 

  • Asilimia 88 ya watumishi waliamini kuwa mwajiri wao hawajali (kati yao madaktari asilimia 82.4, Manesi asilimia 90.7 na Watumishi wengine 87.9)
  • Asilimia 63.3 ya madaktari walionesha kutoridhika na mishahara yao huku kwa manesi ikiwa ni asilimia 66.7
  • Sababu tatu kubwa zilizoonekana kuwafanya watumishi hao kutokuwa na motisha mzuri wa kazi – kwa mfuatano wa uzito wake – ni mishahara, mazingira ya kazi, na vifaa duni vya kazi.
  • Karibu asilimia 30 ya manesi walikuwa hawajaridhika na kazi zao kiasi cha kutaka kuacha kazi hizo. Kwa madaktari ni asilimia 29

Je, kuna jambo lolote ambalo tunaweza kusema leo katika mgomo huu halikuwa likijulikana?

 

Ufisadi na maslahi ya madaktari

Mojawapo ya mambo ambayo labda Watanzania hatujakaa chini na kuyahusisha na matatizo mengi tunayoyaona kwenye sekta za elimu, afya, maji na nishati ni suala la ufisadi. Nimewahi kuandika huko nyuma kuwa ufisadi una gharama na gharama yake kubwa hulipwa na maskini! Kinyume na watu wengi wanavyofikiria matajiri na wale wenye uwezo hulipa gharama ya ufisadi lakini wanailipa kwa sababu wanaimudu. Mtu tajiri au mwenye uwezo akiumwa kichwa anakimbilia India; mbunge amejitengenezea sheria inayompa haki ya kufanyiwa uchunguzi nje ya nchi kila mwaka; Rais amepewa haki hiyo kwa maisha yake yote hata akitoka kwenye cheo chake. Maskini hata hivyo mpaka vikao vifanyike na apitie uchunguzi mrefu ndio atapatiwa nafasi ya kwenda kwenye hospitali ambayo imeteuliwa na watu wengine!

 

Maskini ambaye hatopata nafasi hiyo anajikuta anahangaika na hospitali za humu humu nchini au mambo yakiwa magumu zaidi huishia kwenda kunywa kikombe, kupiga ndumba na ramli au kuishia kwenye imani za kidini. Tajiri atatafuta vitu hivyo vingine pale ambapo fedha zake zimeshindwa kumsaidia! Wakati kwa maskini ramli, ndumba na ibada ni vitu vya kwanza kwa tajiri ni vya mwisho (ukiondoa wale ambao wanachanganya mumo kwa  mumo).

 

Kwenye taifa kama la kwetu ambapo ufisadi umetamalaki matokeo yake ni makubwa zaidi. Leo hii serikali inaweza kusimama na kusema kuwa haina uwezo wa kuboresha maslahi ya madaktari au kununua vifaa au kuhakikisha vifaa vinafanya kazi. Kwa kawaida hili linaweza kuwa kweli kama wananchi wangekuwa hawasikii kashfa mbalimbali za ufisadi na upotevu wa mabilioni ya fedha za umma. Siyo kwenye sekta nyingine tu bali pia kwenye sekta ya afya yenyewe.

 

Katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2010 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu aligundua kati ya mambo mengine mengi  kuhusiana na wizara ya Afya

 

  • Kiasi cha sh 1,895,253,371 kililipwa kwa wazabuni kabla ya kupokea vifaa. Hata hivyo, ukaguzi uliofanyika katika idara za Wizara umebaini kwamba vifaa vya thamani ya sh 1,648,407,271 vilikuwa havijaletwa.
  • Kanuni 198 ya sheria ya fedha za umma ya mwaka 2001 inasema kwamba vifaa vyote vilivyonunuliwa lazima viandikwe kwenye daftari la vifaa. Kinyume na kanuni hii Wizara haikuandika kwenye daftari vifaa vya thamani ya Sh 148,293,950
  • Taarifa ya upotevu ilionyesha upotevu wa kiasi cha sh 4,709,461,863.63 ikihusisha upotevu wa vifaa kiasi cha sh. 2,383,792.63 na madawa yaliyopitwa na wakati kiasi cha Sh.4,707,078,078,071 kwenye Idara ya Bohari Kuu ya Madawa katika mikoa mbalimbali.Upotevu huu ni wa tangu mwaka 2003/2004
  • Wizara ya Afya na Usitawi wa Jamii hupeleka fedha katika bohari ya madawa kwa ajili ya hospitali ya mkoa ili kununua madawa na vifaa vya hospitali. Ukaguzi ulibaini kwamba hospitali ya mkoa wa Singida haikuwa na kumbukumbu za fedha zilizoletwa na Wizara ya Afya na Usitawi wa Jamii kwenda hospitali ya mkoa kununua madawa na vifaa vya hospitali ingawa bohari ya madawa ilionyesha kiasi cha 248,990,169 katika taarifa za fedha.
  • Ilionekana kuwa malipo yaliyofanyika kununulia kemikali katika mwaka huu yaliongezeka kufikia Shilingi bilioni 6.7 kutoka shilingi bilioni 2.3 za mwaka uliopita ikiwa ni ongezeko la asilimia 200. Hali hii  inaonyesha kuwa ongezeko limetokana na kutokuwepo udhibiti mzuri wa Kemikali hizo. Kutokuwepo kwa udhibiti wa kemikali za maabara kutoka stoo za hospitali hupelekea Hospital ya Muhimbili kuingia gharama za ziada kununua kemikali ambazo mara nyingi zinatumiwa isivyopaswa.
  • Ukaguzi ulibaini kuwepo kwa tofauti kati ya mishahara inayotoka Hazina na ile inayoandaliwa na baadhi ya Mashirika ya Umma. Katika Hospitali ya Muhimbili, Tume ya Ushindani wa Biashara (FCC) na Chuo Kikuu cha Dodoma ambapo mishahara ilikuwa inalipwa tofauti na ile inayotoka Hazina. Hali hii inaweza kupelekea udanganyifu kwenye malipo ya mishahara ikiwa ni pamoja na kulipwa kwa mishahara hewa.

 

Hiyo ni mifano michache tu ya kuonesha kuwa Wizara ya Afya yenyewe ina matatizo mengi ya msingi ambayo yanajulikana vile vile ambayo gharama yake bila ya shaka inalipwa na hali mbaya ya maslahi ya madaktari.

 

Mgomo ni lazima uwe na matokeo ya kuboresha afya za wananchi

Mgomo huu hauwezi kuwa ni mgomo wa maslahi ya madaktari tu na ndio maana binafsi siamini kuwa unapaswa kumalizika kwa “serikali kukubali kutoa nyongeza” kwani kufanya hivyo ni kujiandaa kwa matatizo mengine. Kuna mambo au vitu ambavyo vinatakiwa kukubaliwa na serikali sasa hivi pamoja na hilo suala la maslahi. Serikali ni lazima iwe tayari kuweka ahadi na kutenga fedha mara moja kwa ajili ya kushughulikia baadhi ya matatizo sugu yanayokabili hospitali zetu.

 

Mgomo huu utakuwa wa manufaa katika matokeo yake endapo tu:

 

Serikali itakubali kuweka viwango vya ubora wa huduma inayotakiwa kutolewa katika hospital zetu, viwango ambavyo wananchi watatarajia kuviona. Je, Mtanzania atakapoenda kwenye hospitali baada ya mgomo huu ataona nini tofauti katika huduma inayotolewa kwake kama mwananchi, mlipa kodi na mteja? Ni lazima kuwe na tofauti.

Vifaa vya msingi kwa huduma ya hospitali vinaanza kupatikana. Iwe mwiko kwa mwananchi kwenda na glovu yake au sindano yake kwenye hospitali. Wananchi wanatarajia kuona kuwa vitu vya kawaida kwa huduma hospitali vinapatikana kama sehemu ya matibabu. Daktari au muuguzi ni lazima awe na vifaa vya msingi tena vya kisasa ambavyo vitamsaidia kutoa huduma kwa mgonjwa. Haiwezekani nesi anapoenda kazini awe amebeba na box la glovu au bandeji!

 

Madaktari pamoja na wauguzi wanapatiwa afueni ya msingi ikiwemo kwenye kodi zao na mishahara yao. Ni lazima tuwape motisha ili kwamba tukitaka daktari aache usingizi na kukimbia kumhudumia mgonjwa asitusonye! Tusimfanye daktari achague kati ya kwenda kusimamia baa yake au kwenda kuhudumia wagonjwa. Wauguzi wasilipe kodi ya mapato!

 

Serikali iamue mara moja kuwekeza katika ujenzi wa nyumba za madaktari katika maeneo yaliyo karibu na mahospitali. Habari kuwa ati katika nchi nzima serikali imeamua kujenga nyumba nane za madaktari ni kuchezea akili za Watanzania! Kwanini hawakujenga nyumba mbili za mawaziri kama majaribio au ofisi moja ya TAKUKURU kama mfano? Kwanini JWTZ au JKT wasihusishwe katika kujenga nyumba za kisasa (flats au bungalows) kwa ajili ya madaktari kutokana na hadhi zao? Binafsi naamini pa kuanzia tu serikali ijicommit katika kujenga nyumba zisizopungua 100 za madaktari mikoani kwa mwaka huu na kabla ya 2015 zifikie nyumba zisizopungua 1000! Kama tumeweza kujenga nyumba ya Gavana kwa bilioni 3 kwa mtu mmoja na nyumba ya Spika na za wabunge nina uhakika serikali inaweza kabisa kuanza ujenzi wa nyumba za madaktari.

Serikali ianze kutekeleza mpango wa kujiondoa kwenye uendeshaji wa baadhi ya hospitali na kuziachilia zianze kuwa hospitali binafsi au zenye ushiriki wa umma. Kwa mfano, miji au halmashauri ziachiliwe ziwe na udhibiti kamili wa hospitali zao (kuanzia ajira, mafao n.k). Serikali yetu imekuwa kubwa sana (inasimamia polisi, walimu, afya, jeshi n.k) kuna mambo mengine yanaweza kufanywa na serikali za mitaa au halmashauri au sekta binafsi.

 

Serikali ifanya haraka kutengeneza ilipoharibu

Mgomo huu unaweza kuisha mara moja na ukaisha vizuri. Lakini, ninaamini hauwezi kwisha bila kumalizika. Hauwezi kumalizika kama ulivyolazimishwa ule wa 2006 ambapo serikali iliamua kuwatimua madaktari kwani tofauti na wa wakati ule huu wa sasa umeenea nchi nzima na tukio lolote la kutishia kuwafukuza madaktari (walioanzisha au walioshiriki) linaweza kuwafanya madaktari kuwa na msimamo mkali ziaid.

 

Serikali ikubali kuwa imefanya makosa mengi kwenye sekta ya afya na kuwa wakati umefika wa kupitia sera yake ili kufanyia mabadiliko na iwaahidi Watanzania kuwa inapokuja bajeti mpya mabadiliko makubwa yanakuja. Kama serikali haina watu wenye uwezo wa kufikiria sera bora za afya basi iajiri watu ambao watasaidia kuwapa mawazo mapya nje ya yale waliyoyazoea – mimi niko tayari kuwasaidia hapo.

 

Kitu pekee ambacho serikali isifanye ni kupuuzia kwa sababu wasiposhughulikia kwa ukamilifu wake vyanzo vya mgomo huu na kutengeneza pale ambapo wao serikali wameharibu wajue kabisa kuwa mgomo huu hautakuwa wa mwisho na utazidisha chuki ambacho wananchi wameanza kuwa nayo dhidi ya serikali yao. Chuki ya namna hii mara zote inasababisha watu kuchukia chama tawala kinachounda serikali hiyo na hatimaye kukikataa kwenye sanduku la kura. Sasa hivi, inaonekana serikali inajaribisha uvumilivu wa wananchi. Uvumilivu una kikomo.

 

Mwisho

Msingi wa maadili ya mgomo wa madaktari ni maslahi ya wagonjwa na utoaji wa huduma bora, ya wakati na nafuu. Kwamba, kama pasipo kuilazimisha serikali kwa mgomo huduma tayari ni mbovu na hatarishi basi kwa kutumia mgomo wananchi (madaktari na wale wanaowaunga mkono) wanaweza kuishinikiza serikali. Wote wanaoshiriki na kuunga mkono huu wanatambua kuwa kutakuwa na gharama na usumbufu mkubwa kwa kadiri mgomo huu unaendelea. Lakini kuharakisha kuutatua kijuu juu ni kuahirisha tatizo la msingi. Ni muhimu basi kuwa tunapotetea maadili ya afya za wafanyakazi ni lazima tuwe tayarikutetea maadili makubwa zaidi ambayo ni kuboreshwa kwa sekta ya afya nchini ili kwamba wagonjwa, madaktari na watumishi wengine wa sekta hiyo wananufaika.

 

Ni msingi huu wa maadili unatukusuma wengi – tukitambua ugumu na uchungu wa madhara ya mgomo – kuunga mkono mgomo wenye malengo makubwa zaidi kuliko mishahara minono ya madaktari. Malengo yenye kutaka kuona sekta ya afya nchini inaingizwa kwenye karne ya ishirini na moja kwa haraka, kwa ufanisi, na kwa kuzingatia manufaa ya taifa kwa ajili yetu sisi na wale wa kizazi kijacho.

Na. M. M. Mwanakijiji

11 Comments
  • Habari wana Jamii Forum.
    Hivi mgomo wa madaktari kuchukua siku nyingi bila kupatiwa ufumbuzi watanzania tunapata somo gani? kwamba hatuna viongozi walio na uwezo wa kutatua matatizo ya jamii? au tuna viongozi ambao hawatilii maanani masuala yanato wagusa wananchi? Ama ni kwasababu wao na familia zao hawahudumiwi na madaktari hao? Nani anaweza kutoa ufumbuzi wa suala hili, serikali au madaktari ama wananchi?

    Inauma sana.

  • Habari wanajamii.

    Hali ya uongozi wa Wizara ya Afya imenishitua na kunisikitisha.

    Nimekuwa nikijiuliza maswali mengi; mojawapo ni, Mawaziri na Katibu mkuu wa Wizara wapo pale kufanya nini? Wanaongoza viti na meza zilizoko Ofisini au watu walioko chini yao wakiwemo madaktari ambao hasa ndio wanaosababisha viongozi hao kuwepo hapo walipo. Tumekuwa na viongozi wa ajabu Tanzania mpoka watu wagome, waandamane ndiyo malalamiko yao yasikilizwe, Hakika tunaviongozi walio kanyaga shule lakini hawakuelimikiwa.

    Wananchi sasa tuchukue hatua kuwakataa viongozi wa namna hii hata kwa kufunga kufuli ofisi zao.

    Ni aibu kwa serikali na hata aliyewateua

  • Napenda kukupongeza mwandishi. Nina ombi kwako kuwa fursa hii wanaipata watu wachache elimu uliyoitoa hapa; kama inawezekana ikawafikia watanziania wengi ingekuwa njema kwani ni kazi nzuri yenye uthibitisho, it’s scientific tofauti na wengi wamekuwa wakilalama bila facts wala kujua kitu kiundani

  • Nimeisoma busara ya mwandishi huyu.Bravo brother!.
    Nimekua nikijiuliza ile sintofahamu ya wagonjwa waliopasuliwa kichwa badala ya mguu na mguu badala ya kichwa yawezekana ni katika mkanganyiko huu ? au ilikua ni dalili za mvua kuwajuza wakubwa kwamba kuna kitu walitakiwa kikishughulikia mapema ?
    Ni vema viongozi wakajua kusoma alama za nyakati ,kuliko kusubiri migomo na kwa sababu ya kulindana ,huchukua rungu na kuwatwanga waliogoma,kama ambavyo tunaona agizo la Waziri mkuu kwa madaktari,linaloashiria ukandamizaji mwingine wa haki.

  • Mkisoma Hippocratic Oath inasema pia watasomeshwa na kulindwa wakati wa kazi zao ili waweze kumsomeshea watoto wake na kumlisha na kumlinda ili afike mahali aweze kuwa daktari bora; ukiisoma vizuri hii inaweka nguvu nyingi katika baba mwalimu (wizara au chuo) na kusahau kwamba kuna mengi zaidi ya kufuatiliwa ili mambo yawe murwa. Chuo Kikuu cha Tufts huko Marekani ina kiapo cha nyakati zetu za sasa. Kinaeleweka zaidi na kukubalika kwani hakimfanyi daktari mtumwa wa waliofundishwa na Hippocrates (walimu na wakuu wetu wa kazi) bali huangalia mazingira halisi ya je tuko wapi 1800 (hippocrates) 1960’s (Tufts). ukiangalia zote bado ni ngumu sana. maamuzi ya haraka ni muhimu kwa wakati wowote ule

  • Mnajua serikali hii ina mambo mengi ya kipuzi viongozi hawana utaifa, serikali inaghara mia vitu visivyo na maana nchi hii, lakini vitu muhimu inaona kama hivipo inanununua ma v8,wakati V 8 moja ni zaidi ya mil 200, ila kuweka vitanda kwenye hosptali zetu vya thamani ya magari 10 tu fikiri ni vitanda vingapi tena visiagizwe nje hapa hapa kuna mafundi hiyo hela izunguke hapa hapa,
    kuna watanzania wanaumwa ugongwa wa figo, wanahitaji wengine kila week kwenda kwenya mashine maalum kwa ajili ya kutoa sumu, hiyo mashine kwa dar hiko regency na Aghakhan, na kwa siku ilikuwa gharama zaidi ya sh laki 2 ila kwa Ulaya watu wanafungiwa nyumbani? sijasema na sisi tufungiwe nyumbani ila kwa nini kila hospitali ya serikali kusiwe na hizo mashine, kwani ghali kama hayo ma V 8 yao, mpk watu wengine wanakufa kwa kukosa tu huduma ya hizo mashine,

  • pale karibu na Muhimbil kuna maghorofa mengi yanaota kama uyoga, ni ya wahindi ya kupangisha. serikali inashindwa nini, kuangusha skyscraper hapo jirani na hospitali au maeneo ya upanga,ili tu accomodate madaktari wote na wafanyakazi wa Muhimbili, ilikuwapunguzia tatizo la nyumba, na si Muhimbili tu, hata hospitali zingine, ni lini tutaanza kujitegemea kimaamuzi au tuna subiri wazungu waje watufanyie

  • tunatatizo la kimaamuzi katika ngazi zote, hivyo kuna haja ya sector zote kujipanga upya na kuzingatia sheria,sera na miongozo ya utekelezaji wa majukumu yetu”mungu ibariki africa na tanzania”

  • unajua ni ngumu sana kwa madktari kufanya kazi ktk mazingira magumu hili linatokana na baadhi ya watendaji wa serikali kutotimiza wajibu wao kwa uaminifu. Maisha ya watanzania yako matatani haswa pale unapokua huna hela.Watanzania tunatakiwa kubadilika na kuacha siasa katika mambo ya muhimu.

  • Mgomo wa madaktari Tanzania, kwanza umeenda kinyume na taratibu na sheria za nchi. Kwa kuwa madaktari wengi ni wasomi, umma mkubwa wa watanzania unawatetea bila kujali athari zilizoachwa na mgomo huo.

    Kwa upande mwingine siko kabisa upande wa serikali iliyojaa mafisadi, wanaojali zaidi maslahi yao binafsi na kutetea maslahi ya chama tawala, kilichokaa madarakani kwa muda mrefu na kilicholewa madaraka, na kujisahau kuwa iko siku kitatolewa madarakani.Nawashangaa sana watetezi wa haki za binadamu wanaotetea tuu, upande wa madaktari!, bila ya kujali upande unaoumia zaidi, yaani walala hoi wa nchi hii, wanaokufa kama kuku, bila ya utetezi kutoka watetezi wa haki za binadamu. Huu ni unafki mkubwa kutoka kwa watetezi wa haki za kibinadamu, kwani wagonjwa waliokufa kwa kukosa huduma za madaktari waliogoma, wao hawakustahili haki ya kuishi?. Au kwa sababu ya uduni wao kimaisha, unaowafanya kushindwa kwenda kwenye vyombo vya habari na kulalamika!, ndio maana wamesahaulika?.

    Sikubaliani hata kidogo na mgomo wa madaktari unaowaumiza walala hoi kwa kosa la watu walio madarakari, wasiojua wajibu wao ipasavyo, kupelekee watu waliopigika maisha, pengine na wengi wao kukata tamaa kabisa, kuendelewa kuazibiwa zaidi!, kwa kunyimwa haki ya msingi ya kuishi, sio halali kabisa. Kitendo cha Madaktari kugoma na kupelekea vifo vya watu wasio na hatia, hakina tofauti na kikundi cha kigaidi cha Al Shababu cha Somalia au Boko Haramu cha Nigeria. Vikundi hivi viwili, vinauwa watu wasio na hatia ili kutekeleza matakwa yao binafsi, kitendo ambacho hakina tofauti na mgomo wa madaktari hapa nchini.

    Madaktari waliogoma na kusababisha vifo vya raia wengi wasio na hatia, hawana budi kufikishwa mahakamani, kwa mujibu wa sheria, na wakikutwa na makosa wahukumiw kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi, na ikiwezekana wanyongwe!, ili familia zao zipate uchungu sawa kama wenzao waliopoteza maisha kutokana na mgomo huo wa madaktari. Serikali inaweza ikalipa madai ya madaktari kwa awamu!, Je ikitokea madai yao yote yamelipwa, wanaweza kurudisha uhai wa watu waliofariki dunia kwa sababu ya mgomo huo!. Ni wajane wangapi, walioachwa na waume zao kwa sababu ya mgomo huo?, nI watoto wangapi waloachwa yatima, kwa sababu ya mgomo huo?.

    Inatubidi tutumie busara zaidi katika kudai na kutatua migogoro yetu, vinginevyo, special profession yaani madaktari, sio kwa kuvaa makoti meupe na kuwaua wasio na hatia, kupitia mgomo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *