Mtaala wa elimu unavyoakisi ufaulu wa wanafunzi katika shule za msingi Tanzania

Jamii Africa

Elimu ni mfumo wa maarifa unaomwezesha mwanafunzi kupata ujuzi na stadi ambazo zitamsaidia kumudu mazingira yanayomzunguka. Lakini elimu huwa katika mfumo maalumu ambao unajulikana kama mtaala ulio na mpangilio wa masomo ambayo mwanafunzi hujifunza hatua kwa hatua mpaka anapohitimu.

Ubora wa elimu kwa wanafunzi wa elimu ya msingi hupimwa kwa vigezo mbalimbali ikiwemo kujua kusoma na kuandika; stadi za msingi ambazo mwanafunzi anazipata kuukabili ulimwengu wa ajira.

Wengine hupima elimu kwa kuchambua uwezo wa kufikiri, kuhoji, kutambua na kuibua njia mbadara za kutatua matatizo yaliyopo katika jamii, pia huangalia ufaulu wanafunzi.  Lakini vigezo hivyo lazima viandaliwe na mtaala wa elimu ambao humwongoza mwanafunzi kukamilisha ndoto zake.

 Mtaala hujumuisha maarifa, kile kinachofundishwa shuleni, orodha ya kozi, seti ya masomo, programu ya masomo na kozi ya kujifunza. Maana halisi ya mtaala ni orodha ya maarifa ambayo mwanafunzi anatarajiwa ayapate na jinsi maarifa hayo yalivyopangiliwa. Mtaala na ujifunzaji vinaenda pamoja, kama mtaala ni mbovu unaweza kuathiri ubora wa elimu.

Mitaala inayotumika Tanzania imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali za kiufundi ambzo aziendani na mabadiliko ya sayansi na teknolojia. Mtaala wa elimu wa mwaka 2005 ulikuwa ukilalamikiwa na wadau wa elimu kuwa haukidhi matarajio ya wanafunzi katika kujifunza na kupokea maarifa mapya.

Katika kipindi hicho, elimu ilikumbana na matatizo mbalimbali ya kushuka kwa ufaulu katika shule za msingi na sekondari na kusababisha anguko kubwa la ubora wa elimu waliyokuwa wanaipata wanafunzi. Sababu mojawapo ilikuwa ni kutotekelezwa ipasavyo kwa mtaala wa elimu.

Takwimu za wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (2010) zinaonyesha kuwa idadi ya wanafunzi  wanaofaulu mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi imekuwa ikishuka tangu mwaka 2005. Kwa mfano, kiwango cha ufaulu kilishuka kutoka asilimia 70.5 katika mwaka 2006 na kufikia asilimia 54.2 mwaka 2007. Ufaulu huo uliendelea kushuka ambapo mwaka 2008 ulikuwa asilimia 52.7 na ilipofika 2009 ikiwa asilimia 49.4.

Tathmini ya matokeo ya mitihani ya shule za sekondari pia inaonyesha kuwa ufaulu wa wanafunzi umekuwa ukishuka. Kwa mfano, katika kipindi cha miaka saba iliyopita, kati ya mwaka 2005 na 2009, asilimia ya watahiniwa waliopata Daraja la I na II katika mitihani ya kidato cha nne ilishuka kutoka asilimia 12 hadi asilimia 6 mwaka 2009. Lakini takwimu za mwaka 2010 zinaonyesha asilimia 80 ya watahiniwa wa kidato cha nne walipata daraja IV na asilimia 12 tu ndio waliopata daraja I, II na III.

Wanafunzi wakiwa kwenye makundi kujadili masomo

 

Ili kukabiliana na anguko hilo la elimu serikali ilifanya mabadiliko katika mtaala wa elimu wa zamani na kuja mtaala mpya wa mwaka 2016 ambao ulilenga kuiboresha elimu kuwa ya vitendo zaidi kuliko nadharia.

Tangu mabadiliko hayo yafanyike kwa kiasi kikubwa ubora wa elimu umeanza kuongezeka ambapo wanafunzi wanajengewa uwezo wa kujiamini na kutumia stadi muhimu za maisha kuendeleza rasilimali zilizopo nchini.

Mabadiliko ya mtaala yamejumuisha baadhi ya mambo muhimu ikiwemo  kuthamini mila, desturi na Utamaduni, umoja wa kitaifa, maadili mema na kujitambua mwenyewe. Kuwasiliana kwa ufasaha katika muktadha mbalimbali kwa kutumia lugha ya Kiswahili na Kiingereza. 

Pia kuthamini na kuheshimu lugha ya Kiswahili ambayo ni alama ya Umoja wa Taifa na alama ya kujitambulisha. Kujiheshimu na kuheshimu wengine, kutambua utu wake na kuwa Mzalendo. 
 

Kutambua na kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano na teknolojia nyingine kwa ufanisi ili kufikiri kimantiki na kwa tija katika kujitegemea, uvumilivu na kuheshimu tofauti za kiimani na kiitikadi. 

Kubuni, kupenda Sanaa, kuthamini mazingira na kushiriki katika shughuli za Sanaa na kutunza mazingira  kwa kuchunguza, kuchambua na kutafsiri mambo kwa majaribio ya kisayansi. Kutumia fikra za kihisabati katika kutatua matatizo katika maisha ya kila siku pamoja na kutumia stadi za awali za kazi kuingia katika Ulimwengu wa kazi na Ujasiriamali. 

Mtaala huu Mpya wa Elimu Tanzania unamuandaa mwanafunzi kujitegemea pindi atakapo hitimu hatua fulani ya Elimu. Mtaala huu ukitekelezwa vizuri na wadau wote wa elimu nchini utapunguza changamoto cha ufundishaji na ujifunzaji katika shule za msingi.

Hata hivyo, uwekezaji na uboreshaji wa sekta ya elimu ni muhimu ili kujenga jamii iliyostaarabika yenye kuhoji na kubuni njia mbalimbali za kukabiliana na matatizo yaliyopo katika jamii.     

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *