Baraza la mitihani Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya kidato cha pili yaliyofanyika Novemba 2017 na kuonyesha kuwa asilimia 89.93 ya wanafunzi wamepata ujuzi na maarifa kuwawezesha kuendelea na masomo ya kidato cha tatu ambapo ufaulu huo umeshuka kwa asilimia 1.09.
Matokeo hayo yanafikirisha juu mstakabali wa elimu nchini ikizingatiwa kuwa serikali inatekeleza sera ya viwanda na kufikia 2025 nchi inakusudia kuwa uchumi wa kati ambapo rasilimali watu iliyoelimika ni muhimu kufikia malengo hayo muhimu kitaifa.
Licha ya ufaulu huo kuonyesha idadi kubwa ya wanafunzi kufaulu lakini changamoto inabaki kwenye ubora elimu inayotolewa kwasababu mafanikio ya elimu yanapimwa kwa vigezo mbalimbali ambavyo hujumuisha ujuzi na maarifa wanayopata wanafunzi baada ya kumaliza masomo.
Wanafunzi waliofanya mitihani huo walikuwa 486,742 na waliofaulu kuingia kidato cha tatu ni 433,453 ambapo wanafunzi 51,087 sawa na asilimia 10.68 hawakupata alama za kuridhisha na watalazimika kukariri. Kwa muktadha huo zaidi ya robo tatu ya wanafunzi wamefaulu na wana sifa ya kuendelea na masomo ya kidato cha tatu.
Akitangaza matokeo hayo, Katibu Mkuu wa NECTA, Dkt. Charles Msonde amesema, “Kati ya hao wasichana wapo 224,736 sawa na asilimia 88.55 na wavulana 208,177 sawa na asilimia 90.17 ukilinganisha na mwaka 2016 ambapo watahiniwa 372,288 sawa na asilimia 91.02 walipata alama za kuwawezesha kuendelea na masomo ya kidato cha tatu”.
Wanafunzi wakifanya mtihani
Licha ya ufaulu kushuka ukilinganisha na mwaka 2016, idadi kubwa ya wanafunzi waliofaulu kuingia kidato cha tatu wamepata daraja la nne ambapo kwa kigezo cha kupima ubora wa maarifa waliyoyapata matokeo yao hayaridhishi na uwezekano wa kufeli kidato cha nne ni mkubwa zaidi ikiwa hatua stahiki za kurekebisha kasoro zilizojitokeza hazitachukuliwa.
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa wanafunzi waliopata daraja la kwanza hadi la tatu ni 195,142 sawa na asilimia 40.34 ambapo asilimia 59.36 iliyobaki wamepata daraja la nne na la mwisho. Licha ya asilimia 89.93 kufaulu katika madaraja tofauti kimsingi idadi kubwa ya wanafunzi hawajafanya vizuri katika masomo yao na hatua zisipochukuliwa idadi ya wanaofeli itaendelea kushuka kila mwaka.
Matokeo hayo bado yanafikirisha juu mstakabali wa elimu wanayoipata wanafunzi wakiwa shuleni ikizingatiwa kuwa ufaulu wa baadhi masomo yakiwemo ya hisabati, sayansi na Kiingereza hauridhishi licha ya kupanda ukilinganisha na mwaka 2016 na kutatiza juhudi za serikali kujenga msingi imara kuelekea uchumi wa viwanda ambao unahitaji nguvu kazi iliyobobea kwenye uvumbuzi na utafiti.
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa wanafunzi wamefaulu zaidi kwenye somo la Kiswahili kwa asilimia 91.92 huku ufaulu ukishuka kwenye masomo ya Uraia, Historia na Biologia ambapo somo la hisabati ndilo wanafunzi wamefaulu kwa kiwango cha chini cha asilimia 32 kuliko masomo mengine.
Somo la hisabati ndio msingi wa masomo mengine ya sayansi, lakini muitikio wa wanafunzi katika somo hilo ni mdogo na huchangiwa na uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi na vifaa vya kujifunzia kwenye shule mbalimbali nchini.
Mtihani huo wa kidato cha pili uliofanyika kati ya tarehe 14 na 23 imeibua suala lingine la wanafunzi wanaokatiza masomo kwasababu mbalimbali ikiwemo utoro, mimba na mazingira magumu ya kusomea. Wanafunzi 486,743 ndio walifanya mtihani kati ya 521,759 waliondikishwa ambapo wanafunzi 35,016 sawa na asilimia 6.74 hawakupata fursa ya kufanya mtihani huo.
Kwa matokeo hayo, serikali na wadau wa elimu wanapaswa kutathmini mstakabli wa elimu inayotolewa nchini na kuboresha makosa ambayo yamejitokeza hasa kwenye masomo ya sayansi na ubora wa elimu inayotolewa kwa wanafunzi. Tathmini hiyo itasaidia kupanga mikakati na vipaombele muhimu katika kuboresha sekta ya elimu ambayo inakabiliwa na changamoto mbalimbali za miundombinu, sera na sheria.
Hata hivyo, serikali iwekeze katika kutumia vigezo vya ubora na kiwango cha maarifa wanayopata wanafunzi kuliko kujikita kwenye ufaulu pekee.