Wananchi waikwepa kamati ya shule, maamuzi na mipango ya elimu yatekelezwa na wachache

Jamii Africa

Inaelezwa kuwa kiwango cha ushiriki wa wananchi katika shughuli za jamii hasa za kiutawala nchini Tanzania kiko chini na bado kinashuka, jambo ambalo linaathiri utolewaji wa maamuzi yanayohusu maendeleo ya taifa.

Sekta ya elimu kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali za ubora wa elimu inayotolewa na mazingira yasiyoridhisha wanayosomea wanafunzi. Changamoto hizo kwa kiasi kikubwa zinasababishwa na ushiriki duni wa wananchi katika maendeleo ya shule.

Ripoti ya Shirika la HakiElimu (2017) inaeleza kuwa kiwango cha ushiriki wa wananchi katika sekta mbalimbali za utawala nchini Tanzania, hasa kwa wanawake, kiko chini sana na bado kinashuka.

“ Kwa mfano, ushiriki wa wananchi katika vikao vya kamati za shule ulipungua kutoka asilimia 36 mwaka 2006 hadi kufikia asilimia 15 mwaka 2013, hii ni sawa asilimia 13 ya kushuka kwa ushiriki wa wananchi kwenye huduma hii muhimu ya umma”, inaeleza ripoti hiyo.

Kamati za shule ni sehemu muhimu ambapo wananchi wanajadili changamoto za shule zilizopo katika eneo husika  uhakikisha kunakuwa na matumizi mazuri ya rasilimali fedha zinazoelekezwa katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika shule.

“Mikutano ya vijiji na kata ni fursa muhimu kwa ajili ya kufanya maamuzi yanayoathiri watoto na elimu, kwa viwango hivi vidogo vya ushiriki wa wananchi, kuna uwezekano changamoto za sekta zitaendelea kubaki bila kutatuliwa”, inaeleza sehemu ya ripoti hiyo na kuongeza kuwa,

 “Ni asilimia 22 tu ya wananchi, hasa wanaume, huhudhuria mikutano ya mabaraza ya vijiji ambayo ni fursa muhimu kwa ajili ya kujadili masuala muhimu ya kijiji na kufanya maamuzi yanayoathiri watoto na elimu”.

Licha ya ushiriki mdogo wa wananchi katika mikutano na vikao vya kamati za shule lakini mipango ya maendeleo huandaliwa na watu wachache hasa viongozi waliochaguliwa ambapo na kufanya maamuzi kwa niaba ya wananchi. Baadhi ya viongozi huitumia fursa hiyo kupindisha baadhi ya maamuzi na kutumia fedha za shule kwa matumizi binafsi.

“Na ni asilimia 16 tu ya wananchi ndio hushiriki katika kuandaa mipango ya kata na ya vijiji. Idadi kubwa ya washiriki hawa ni wale waliopata elimu ya msingi tu, hii ina maana kuwa wasomi wengi kwa kiasi kikubwa hawashiriki michakato hii muhimu”.

Ufuatiliaji wa taarifa za matumizi na utendaji wa kamati za shule ni muhimu lakini shughuli za kiuchumi zinawafanya watu wa mjini kukosa muda wa kushiriki katika kamati za shule na kukwamisha mipango ya kukuza elimu nchini.

Haji Hussein, mkazi wa Sinza, jijini Dar es Salaam anasema ana majukumu mengi ya kikazi ambayo yanamfanya akose muda wa kushiriki na kufuatilia maendeleo ya elimu katika Mtaa wake lakini hulazimika kushiriki kama kuna jambo la muhimu.

“Nina majukumu mengi ya kikazi ambayo yananifanya nikose muda, hata hivyo maisha tuliyonayo mjini yanatufanya tuwe bize sana hata kukosa muda wa kufuatilia hayo mambo”, anaeleza mkazi huyo wa Sinza.

Kwa upande wake, Gwamaka Sima wa Kijitonyama anasema suala la maendeleo ya jamii hasa elimu ya watoto linamuhusu kila mwananchi. Ili kujenga jamii iliyoelimika ni muhimu wananchi kutenga muda na kushiriki katika mipango ya shule ili kuongeza ubora wa elimu ambao unaathiriwa na maamuzi yasiyo sahihi ya baadhi ya viongozi.

Kamati ya Shule ni Nini?

Kamati ya shule ni kikundi cha wajumbe waliochaguliwa kwa ajili ya kuongoza na kuangalia shughuli za shule ya msingi kwa msaada wa jamii. Kila shule ya msingi kisheria inatakiwa kuwa na kamati ya shule ikiwa na lengo la kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM).

Majukumu ya Kamati ya Shule

Kulingana na MMEM imeanisha majukumu yafuatayo:

  • Kuhamasiha, kuhusisha na kuwasilisha habari za elimu kwa wazazi wote, wanafunzi,wadau katika jamii na watendaji na mamlaka ya serikali za Mtaa/Kijiji.

 • Kushughulikia masuala ya shule ya kila siku, pamoja na utekelezaji wa vipengele vyote vinne vya MMEM.

• Kushirikiana na mwalimu mkuu na walimu wengine kuweka vipaumbele na kuandaa Bajeti na Mipango ya Maendeleo ya shule.

• Kufungua akaunti na kusimamia kwa uhakika na uangalifu fedha zilizo pokelewa kwa ajili ya utekelezaji, kuhakikisha uwajibikaji wa hali ya juu na uwazi katika mchakato unaotumika,ikiwa ni pamoja na kuweka wazi mapato na matumizi kwa jamii.

 • Kuandaa na kutoa kwa usahihi na kwa wakati mwenendo na ripoti ya fedha kwa jamii, Kata na Halmashauri.

Hata hivyo, HakiElimu inashauri kuwa kila mtu ana haki ya kupata taarifa, na kila mmoja ana haki ya kujua kuhusu utawala katika MMEM. Na kwa kuwa sasa unafahamu MMEM inasema nini kuhusu Kamati za shule, unaweza kuona ni jinsi gani Kamati hizo zinafanya kazi katika jamii yako na kutoa mawazo yakinifu yatakayosaidia kufanya mambo yawe bora zaidi.

Kila mwaka tumekuwa tukishuhudia ubora wa elimu ukishuka na lawama zote tunaitupia serikali lakini kama wananchi tuna nafasi ya kutoa ushauri wa elimu inayotakiwa kutolewa kwa watoto wetu kulingana na mazingira ya jamii zetu. Suala hili haliwezekani mpaka tujitoe kikamilifu kufuatilia na kushiriki katika kamati za maendeleo ya elimu zilizopo katika mitaa yetu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *