Mto Wami/Ruvu: Haya pia ni matumizi yake

Kulwa Magwa

KABLA sijafika tarafa ya Matombo, iliyopo mkoani Morogoro, nilikuwa na mawazo tofauti kuhusu mto Wami/Ruvu ambao baadhi ya vyanzo vyake viko sehemu hiyo.

Akili na mawazo yangu yalinituma niamini huenda mto huo una kazi moja pekee ya kuwahudumia watu kwa maji ya kunywa na matumizi ya nyumbani.

Pia katika fikra zangu nilikuwa nawaza unalindwa saa 24 na ulinzi wake ni wa hali ya juu ambao mifugo na waharibifu wengine wanaweza kutishia uhai wake hawawezi kusogea karibu. Hayo yalikuwa mawazo yangu.

Siku chache zilizopita nilikuwa sehemu hiyo, ambako pamoja na mengine niliyofanya, kazi yangu ilihusisha kujua mambo yanayofanyika kwenye vyanzo vya mto na mto wenyewe.

Kwanza, nilibaini fikra na mawazo yangu hayakuwa sahihi, na kwamba zipo kazi nyingine zinazofanyika katikati au kando ya mto. Hizo ni kazi za kibinadamu, ingawa kwa vile katika baadhi ya maeneo unayopita kuna misitu, basi hata wanyama wa porini nao hufanya vitu vyao mtoni.

Kwa baadhi ya wanyama – nyakati za joto kali, huingia mtoni wakapumzika ili kupunguza hali ya ujoto. Hao ni pamoja na kima, ngedere na nyani.

Hata hivyo, kwa binadamu, mto huo wenye urefu wa kilometa 316 kutoka chanzo chake kilichoko sehemu za Matombo hadi Ruvu, mkoani Pwani – zipo kazi takriban kazi tatu nilizoshuhudia zinafanyika.

Hizo ni pamoja na usafi wa mavazi; kufua nguo na kuoga, kwa maana nyingine watu hufua na kuoga mtoni. Pili, huchimba dhahabu katikati na pembezoni mwa kingo za mto; na tatu, hunywa maji yale na kuyatumia kwa kilimo cha umwagiliaji.

Kazi hizo zote hufanyika bila mpangilio na hufanyika mahali popote mtu anapoona anaweza kufanya anachotaka. Hivyo si ajabu kuwakuta watu wanafua katikati ya mto, wanachimba dhahabu na pia wanaoga na kuchota maji ya kutumia nyumbani.

Vilevile haishangazi kuona wanaofanya hivyo, hususan kuchimba madini na kufua nguo, baada ya muda ndio hao wanaokwenda kuchota maji hayo kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Sina hakika kama wengi iwapo wanapoyachota huzingatia kuyachemsha kabla ya kuyanywa.

kuchenjua

Vijana wakichenjua na kukusanya mchanga katikati ya mto Wami, kwenye kijiji cha Kibangile, mkoani Morogoro

Mzee Shaaban Bilal ameishi miaka 37 katika Kijiji cha Kibangile, akiwa na makazi yake takriban mita 30 kutoka ilipo kingo mojawapo ya mto huo, ambaye anasema wamezowea kufanya shughuli hizo bila kujali maji wanayoyachafua – yaendako kuna watu wengine wanaoyatumia kwa kuyanywa.

“Sisi hatuwezi kuacha kutumia tulivyowea, maana hata hayo mabomba hatuna. Kama kungekuwa na pampu ya kutusambazia maji, nadhani ungekuta wachimba madini pekee mtoni,“anasema mzee Bilal (67).

Anasema ni kazi ngumu kuweza kuzuia watu kufua na kuchimba madini kwakuwa wamezowea na suluhu pekee ya kuwaondolea utamaduni huo ni kwa mamlaka husika kuwatengenezea mabomba.

Kwa upande wake, Zahor Gonja, ambaye nilimkuta anafua nguo kando ya mto, anasema hata mamlaka zinazohusika, hazipigii kelele ufuaji wa nguo wala kuoga mtoni, hivyo hawawezi kuacha kuutumia mto huo kwa matumizi hayo.

“Wakija hao watu wa Bonde (la Maji la) Wami/Ruvu wanaangalia tu kama kuna wachimbaji wa madini, kisha wanaondoka zao. Hata kama unafua au kuoga hawakufanyi lolote, ina maana nao wameridhika hatuchafui maji, “anasema Gonja.

Msimamizi wa Ofisi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu katika kijiji cha Kibangile, Gilbert Ngahimila, anasema matumizi ya mto huo hayawezi kuzuilika, isipokuwa wanachoangalia ni yale yanayohatarisha afya za watumia maji na pia uharibifu wa mto na vyanzo vyake.

Anasema, kwa sasa wanasaka ufumbuzi wa wale wanaochimba dhahabu ambao wamekuwa wakikabiliana nao kwa zaidi ya miaka mitano sasa.

“Pengine baada ya hapo ndipo wadau watakuja na mkakati mwingine wa kukomesha baadhi ya shughuli zinazofanyika ambazo zinachafua maji na kuathiri mto huu, “anasema Ngahimila.

Hata hivyo, Ofisa Mazingira wa wilaya ya Morogoro, Mary Kayowa, anasema shughuli nyingine za kibinadamu zinapaswa kupigwa vita kwa kuwa ni hatari kwa maisha ya watu.

Anasema, iwapo uchimbaji dhahabu utaachwa uendelee, athari za kiafya kwa watumia maji hazitaepukika katika siku za usoni.

“Kazi kama hiyo inaambatana na matumizi ya mekyuri ambayo ni hatari kwa afya ya binadamu. Fikiria watu wangapi wanaokunywa maji huko yanakopita ambayo yanaweza kuwa na kemikali hiyo, “anasema ofisa huyo.

Mto Wami/Ruvu una vyanzo kadhaa katika sehemu hiyo na milima ya Uluguru, ambapo unakadiriwa maji yake kutumiwa na watu zaidi ya milioni nane katika mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *