Muleba: Kukwama kwa ujenzi wa zahanati kwasababisha vifo

Jamii Africa

KUSHINDWA kukamilika kwa ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Kasindaga, Kata ya Kyebitembe, Wilaya ya Muleba, Kagera  kunasababisha matatizo makubwa ya afya na vifo.

Hiyo inatokana na kukosekana kwa huduma za afya ikiwamo tiba na ushauri kwa wagonjwa.

Wananchi wa kijiji hicho wameiambia FikraPevu katika kijiji hicho kuwa wanalazimika kutembea umbali wa kilomita 18 kwenda makao makuu ya kata  Kyebitembe kutafuta huduma za afya, licha ya kijiji hizo kuwa na jengo la zahanati ambalo linakaliwa na popo na milango kuvunjwa kwa upepo.

Zahanati ambayo haijakamilika ujenzi wake.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Spensioza Simeon alisema wanaoteseka katika kupata huduma za afya ni watoto wadogo, wakiwemo walioko chini ya miaka mitano na walioko katika shule za msingi,  ambao huugua magonjwa mbalimbali, hasa malaria  na kuhara.

Spensioza aliiambia FikraPevu kwamba kijiji hicho hakina hata maduka ya dawa binafsi, achilia mbali yale ya vijiji yanayoweza kusimamiwa na serikali.

Alisema wanawake wajawazito wanalazimika kutembea wakiteseka kwenda Zahanati ya Kyebitembe.

“Tunahimizwa kuchangia huduma za afya na kukata bima lakini hatuna huduma yoyote na kadi zetu hazitumiki katika zahanati za vijiji vingine ambapo kila kukicha wanapatikana wajawazito na kuzaliwa watoto,” alisema Visent Damas, mkazi wa kijiji hicho.

Pikipiki ndiyo usafiri

FikraPevu imebaini kuwa wakazi wengi wanapougua au kuuguliwa, hutumia zaidi usafiri wa pikipiki kwenda kijiji cha jirani kupata huduma za afya. Gharama ya kukodi pikipiki kwenda  huko ni kuanzia Sh. 2,000 kwa mtu, kutegemea na umbali. Pikipiki huweza kubeba abiria hata watatu, ingawa ni kinyume cha sheria za usalama barabarani.

Kwa wale wasiokuwa na uwezo, hutembea kwa umbali mrefu au kwa kutumia wanyama-kazi, kama ng’ombe na punda, ingawa ni wachache mno katika kijiji hicho.

Zahanati ya Kijiji cha Kasindaga ilianza kujengwa mwaka 2012 ambapo wananchi walichangia vifaa; mchanga, kokoto mawe na matofali pamoja na kutoa fedha za kuwalipa mafundi.

Shilingi milioni 120 zatumika

Mwenyekiti wa kijiji cha Kasindaga kata ya Kyebitembe wilaya ya Muleba mkoani Kagera Mathias Bishobo akionesha kibao cha ujenzi wa zahanati hiyo ambayo haijakamilika hadi sasa.

Mwenyekiti wa kijiji hiicho, Mathias Bishobo ameiambia FikraPevu kwamba ujenzi ulianza na kwamba ulifikia hatua nzuri, katika kuezeka, huku Sh. Milioni 120 zikitumika, lakini haukuendelea kutokana na kutokamilika kwa  baadhi ya vifaa, hasa mabati.

Alisema kijiji hicho chenye kaya 526 na wakazi 5,364, bado wakazi wake wanataabika kupata matibabu kwani wengine, wenye uwezo hulazimika kukodi magari kwenda kupata tiba Kituo cha Afya Kimeya, Kata ya Kasharunga, umbali wa kilomita 42.

“Jengo la zahanati hii linahitaji kukamilisha vyumba vya kutolea huduma kufunga milango na madirisha, lakini pia kujenga nyumba ya mganga na kuweka vifaa vya tiba pamoja na dawa zinazoweza kuhudumia wananchi wa kijiji hiki,” anaongeza mwenyekiti huyo akizungumza na FikraPevu.

Aliiomba halmashauri ya wilaya ya Muleba kuharakisha upatikanaji wa fedha za kukamilisha zahanati hiyo na kuweza kusaidia wananchi kupata huduma za afya karibu na makazi yao na kupunguza gharama za kusafiri kwenda mbali kupata matibabu.

Hata hivyo, akusema kiasi kamili kinachohitajika kukamilisha ujenzi wa majengo ya zahanati hiyo ili ianze kutoa huduma na kupunguza adha kwa wananchi.

Mganga Mkuu azungumza

Mganga mkuu wa wilaya ya muleba Dkt. Modest Lwakahemula  kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Emanuel Sherembi aliiambia FikraPevu kwamba zahanati hiyo ilishatengewa bajeti ya kuikamilisha, changamoto ni fedha kutoka serikalini na mapato ya ndani ya halmashauri, ambayo hayatoshi.

Mbunge wa jimbo la Muleba Kusini,Prof. Anna Tibaijuka alisema ameishauri halmashauri kutafuta fedha za dharura na kuwahusisha wahisani , wakiwamo wale wa Mradi wa Huduma ya Mama na Mtoto (MMAM) kusaidia ujenzi wa zahanati hiyo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *